[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16]

Chapter 12

1: Kwa hiyo, ndugu zangu, maadam Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: jitoleeni nafsi zenu kwa Mungu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu. 2: Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikira zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu, kutambua jambo lililo jema, linalompendeza na kamilifu. 3: Kutokana na neema aliyonijalia Mungu, nawaambieni ninyi nyote: msijione kuwa ni kitu zaidi kuliko mnavyopaswa kuwa. Fikira zenu na ziwe na kiasi kufuatana na kipimo cha imani Mungu aliyomgawia kila mmoja. 4: Mwili una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake. 5: Hali kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. 6: Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kufuatana na neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake. 7: Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe. 8: Mwenye kipaji cha kuwafariji wengine na afanye hivyo. Mwenye kumgawia mwenzake alicho nacho na afanye hivyo kwa ukarimu. Msimamizi na asimamie kwa bidii; naye mwenye kutenda jambo la huruma na afanye hivyo kwa furaha. 9: Mapendo yenu na yawe bila unafiki wowote. Chukieni jambo lolote ovu, zingatieni jema. 10: Pendaneni kidugu; kila mmoja amfikirie mwenzake kwanza kwa heshima. 11: Msilegee katika bidii, muwe wachangamfu rohoni katika kumtumikia Bwana. 12: Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida na kusali daima. 13: Wasaidieni watu wa Mungu katika mahitaji yao; wapokeeni wageni kwa ukarimu. 14: Watakieni baraka wote wanaowadhulumu ninyi; naam, watakieni baraka na wala msiwalaani. 15: Furahini pamoja na wanaofurahi, lieni pamoja na wanaolia. 16: Muwe na wema uleule kwa kila mtu. Msijitakie makuu, bali jishugulisheni na watu wadogo. Msijione kuwa wenye hekima sana. 17: Msilipe ovu kwa ovu. Zingatieni mambo mema mbele ya wote. 18: Kadiri inavyowezekana kwa upande wenu, muwe na amani na watu wote. 19: Wapenzi wangu, msilipize kisasi, bali mwachieni Mungu jambo hilo; maana Maandiko Matakatifu yasema: "Kulipiza kisasi ni shauri langu; mimi nitalipiza asema Bwana." 20: Tena, Maandiko yasema: "Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe kinywaji. Maana kwa kufanya hivyo utamfanya apate aibu kali kama makaa ya moto juu ya kichwa chake." 21: Usikubali kushindwa na ubaya, bali ushinde ubaya kwa wema.