[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16]

Chapter 9

1: Nasema ukweli mtupu; nimeungana na Kristo nami sisemi uongo. Dhamiri yangu ikiongozwa na Roho Mtakatifu inanithibitishia jambo hili pia. 2: Nataka kusema hivi: nina huzuni kubwa na maumivu yasiyopimika moyoni mwangu 3: kwa ajili ya watu wangu, walio damu moja nami! Kama ingekuwa kwa faida yao, ningekuwa radhi kulaaniwa na kutengwa na Kristo. 4: Hao ndio watu wa Israeli ambao Mungu aliwateua wawe watoto wake, akawashirikisha utukufu wake; aliagana nao, akawapa Sheria yake, imani ya kweli na ahadi zake. 5: Wao ni wajukuu wa mababu, naye Kristo, kadiri ya ubinadamu wake, ametoka katika ukoo wao. Mungu atawalaye juu ya yote, na atukuzwe milele! Amina. 6: Sisemi kwamba ahadi ya Mungu imebatilika; maana si watu wote wa Israeli ni wateule wa Mungu. 7: Wala, si wazawa wote wa Abrahamu ni watoto wake wa kweli. Ila, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Wazao wake watatokana na Isaka." 8: Nido kusema, wale waliozaliwa kimaumbile ndio watoto wa Mungu, bali wale waliozaliwa kutokana na ahadi ya Mungu ndio watakaoitwa watoto wake. 9: Maana ahadi yenyewe ni hii: "Nitakujia wakati maalum, naye Sara atapata mtoto." 10: Tena si hayo tu ila pia Rebeka naye alipata mapacha kwa baba mmoja, yaani Isaka, babu yetu. 11: Lakini, ili Mungu aonekane kwamba anao uhuru wa kuchagua, hata kabla wale ndugu hawajazaliwa na kabla hawajaweza kupambanua jema na baya, 12: Rebeka aliambiwa kwamba yule mtoto wa kwanza atamtumikia yule wa nyuma. Hivyo uchaguzi wa Mungu unategemea jinsi anavyoita mwenyewe, na si matendo ya binadamu. 13: Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Yakobo nilimpenda, lakini Esau nilimchukia." 14: Basi, tuseme nini? Je, Mungu amekosa haki? Hata kidogo! 15: Maana alimwambia Mose: "Nitamhurumia mtu yeyote ninayetaka kumhurumia; nitamwonea huruma mtu yeyote ninayetaka." 16: Kwa hiyo, yote hutegemea huruma ya Mungu, na si bidii au mapenzi ya mtu. 17: Maana Maandiko Matakatifu yasema hivi kwa Farao: "Nilikufanya mfalme ili kwa njia yako, uwezo wangu ujulikane, na jina langu litangazwe popote duniani." 18: Ni wazi,basi, kwamba Mungu humhurumia yeyote anayetaka kumhurumia, na akipenda kumfanya mtu awe mkaidi, hufanya hivyo. 19: Labda utaniuliza: "Ikiwa mambo yako hivyo, Mungu anawezaje kumlaumu mtu? Nani awezaye kuyapinga mapenzi yake?" 20: Lakini, ewe binadamu, u nani hata uthubutu kumhoji Mungu? Je, chungu chaweza kumwuliza mfinyanzi wake: "Kwa nini umenitengeneza namna hii?" 21: Mfinyanzi anaweza kuutumia udongo apendavyo na kufinyanga vyungu viwili kwa udongo uleule; kimoja kwa matumizi ya heshima, na kingine kwa matumizi ya kawaida. 22: Hivyo ndivyo ilivyo kwa Mungu. Alitaka kuonyesha ghadhabu yake na kujulisha uwezo wake, Basi, alikuwa na saburi sana, akiwavumilia wale ambao walikuwa lengo la ghadhabu yake, ambao walistahili kuangamizwa. 23: Alitaka pia kudhihirisha wingi wa utukufu wake ambao alitumiminia sisi tulio lengo la huruma yake; sisi ambao alikwisha kututayarisha kuupokea utukufu wake. 24: Maana sisi ndio hao aliowaita, si tu kutoka miongoni mwa Wayahudi bali pia kutoka kwa watu wa mataifa mengine. 25: Maana ndivyo asemavyo katika kitabu cha Hosea: "Wale waliokuwa `Si watu wangu` nitawaita: `Watu wangu!` Naye `Sikupendi` ataitwa: `Mpenzi wangu!` 26: Na pale walipoambiwa: `Ninyi si wangu` hapo wataitwa: `Watoto wa Mungu hai."` 27: Naye nabii Isaya, kuhusu Israeli anapaaza sauti: "Hata kama watoto wa Israeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni wachache tu watakaookolewa; 28: maana, Bwana ataitekeleza upesi hukumu yake kamili juu ya ulimwengu wote." 29: Ni kama Isaya alivyosema hapo awali: "Kama Bwana Mwenye Nguvu asingalituachia baadhi ya watoto wa Israeli, tungalikwisha kuwa kama Sodoma, tungalikwisha kuwa ma Gomora." 30: Basi, tuseme nini? Ni hivi: watu wa mataifa ambao hawakutafuta kukubaliwa kuwa waadilifu, wamekubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya imani, 31: hali watu wa Israeli waliokuwa wakitafuta Sheria iletayo kukubaliwa kuwa waadilifu, hawakuipata. 32: Kwa nini? Kwa sababu walitegemea matendo yao badala ya kutegemea imani. Walijikwaa juu ya jiwe la kujikwaa 33: kama yesemavyo Maandiko Matakatifu: "Tazama! Naweka huko Sioni jiwe likwazalo, mwamba utakaowafanya watu waanguke. Mtu atakayemwamini yeye aliye hilo jiwe, hataaibishwa!"