[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22]

Chapter 14

1: Kisha nikaona mlima Sioni, na Mwanakondoo amesimama juu yake; pamoja naye walikuwa watu mia moja arobaini na nne elfu ambao juu ya paji za nyuso zao walikuwa wameandikwa jina la Mwanakondoo na jina la Baba yake. 2: Basi, nikasikia sauti kutoka mbinguni, sauti iliyokuwa kama sauti ya maji mengi na kama sauti ya ngurumo kubwa. Sauti niliyosikia ilikuwa kama sauti ya wachezaji muziki wakipiga vinubi vyao. 3: Walikuwa wanaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe hai wanne na wale wazee. Hakuna mtu aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao watu mia moja arobaini na nne elfu waliokombolewa duniani. 4: Watu hao ndio wale waliojiweka safi kwa kutoonana kimwili na wanawake, nao ni mabikira. Wao humfuata Mwanakondoo kokote aendako. Wamekombolewa kutoka miongoni mwa binadamu wengine, wakawa wa kwanza kutolewa kwa Mungu na kwa Mwanakondoo. 5: Hawakupata kamwe kuwa waongo; hawana hatia yoyote. 6: Kisha nikamwona malaika mwingine anaruka juu angani akiwa na Habari Njema ya milele ya Mungu, aitangaze kwa watu wote waishio duniani, kwa mataifa yote, makabila yote, watu wa lugha zote na rangi zote. 7: Akasema kwa sauti kubwa, "Mcheni Mungu na kumtukuza! Maana saa imefika ya kutoa hukumu yake. Mwabuduni yeye aliyeumba mbingu na nchi, bahari na chemchemi za maji." 8: Malaika wa pili alimfuata huyo wa kwanza akisema, "Ameanguka! Naam, Babuloni mkuu ameanguka! Babuloni ambaye aliwapa mataifa yote wainywe divai yake--divai kali ya uzinzi wake!" 9: Na malaika wa tatu aliwafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, "Yeyote anayemwabudu yule mnyama na sanamu yake na kukubali kutiwa alama yake juu ya paji la uso wake au juu ya mkono wake, 10: yeye mwenyewe atakunywa divai ya ghadhabu ya Mungu, ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake bila kuchanganywa na maji. Mtu huyo atateseka ndani ya moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele ya Mwanakondoo. 11: Moshi wa moto unaowatesa kupanda juu milele na milele. Watu hao waliomwabudu huyo mnyama na sanamu yake, na kutiwa alama ya jina lake, hawatakuwa na nafuu yoyote usiku na mchana." 12: Kutokana na hayo, ni lazima watu wa Mungu, yaani watu wanaotii amri ya Mungu na kumwamini Yesu, wawe na uvumilivu. 13: Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, "Andika! Heri watu ambao tangu sasa wanakufa wakiwa wameungana na Bwana." Naye Roho asema, "Naam! Watapumzika kutoka taabu zao; maana matunda ya jasho lao yatawafuata." 14: Kisha nikatazama, na kumbe palikuwapo wingu jeupe hapo. Na juu ya wingu hilo kulikuwa na kiumbe kama mtu. Alikuwa amevaa taji ya dhahabu kichwani, na kushika mundu mkononi mwake. 15: Kisha malaika mwingine akatoka Hekaluni, na kwa sauti kubwa akamwambia yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu, "Tafadhali, tumia mundu wako ukavune mavuno, maana wakati wa mavuno umefika; mavuno ya dunia yameiva." 16: Basi, yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu akautupa mundu wake duniani, na mavuno ya dunia yakavunwa. 17: Kisha malaika mwingine akatoka katika Hekalu mbinguni akiwa na mundu wenye makali. 18: Kisha malaika mwingine msimamizi wa moto, akatoka madhabahuni akamwambia kwa sauti kubwa yule malaika mwenye mundu wenye makali, "Nawe tia huo mundu wako mkali, ukakate vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva!" 19: Basi, malaika huyo akautupa mundu wake duniani, akakata zabibu za dunia, akazitia ndani ya chombo kikubwa cha kukamulia zabibu, chombo cha ghadhabu ya Mungu. 20: Zabibu zikakamuliwa ndani ya hilo shinikizo lililoko nje ya mji, na damu ikatoka katika shinikizo hilo mtiririko mrefu kiasi cha mita mia tatu na kina chake kiasi cha mita mia mbili.