[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22]

Chapter 10

1: Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu, na upinde wa mvua kichwani mwake. Uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake ilikuwa kama moto. 2: Mikononi mwake alishika kitabu kidogo kimefunguliwa. Aliweka mguu wake wa kulia juu ya bahari, na wa kushoto juu ya nchi kavu, 3: na kuita kwa sauti kubwa kama ya mngurumo wa simba. Alipopaaza sauti, ngurumo saba ziliitikia kwa kishindo. 4: Na hizo ngurumo saba ziliposema, mimi nikataka kuandika. Lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni: "Maneno ya ngurumo hizo saba ni siri; usiyaandike!" 5: Kisha yule malaika niliyemwona akisimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu akainua mkono wake wa kulia juu mbinguni, 6: akaapa kwa jina la Mungu aishiye milele na milele, Mungu aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, bahari na vyote vilivyomo, dunia na vyote vilivyomo. Akasema, "Wakati wa kusubiri zaidi umekwisha! 7: Lakini wakati ule malaika wa saba atakapotoa sauti yake, wakati atakapopiga tarumbeta yake, Mungu atakamilisha mpango wake wa siri kama alivyowatangazia watumishi wake manabii." 8: Kisha ile sauti niliyokuwa nimeisikia kutoka mbinguni pale awali ikasema nami tena: "Nenda ukakichukue kile kitabu kilichofunguliwa, kilicho mkononi mwa malaika asimamaye juu ya bahari na juu ya nchi kavu." 9: Basi, nikamwendea huyo malaika, nikamwambia anipe hicho kitabu kidogo. Naye akaniambia, "Kichukue, ukile; kinywani mwako kitakuwa kitamu kama asali, lakini tumboni kitakuwa kichungu!" 10: Basi, nikakichukua kitabu hicho kidogo kutoka mkononi mwa huyo malaika, nikakila; nacho kilikuwa kitamu kinywani mwangu kama asali, lakini nilipokimeza kikawa kichungu tumboni mwangu. 11: Kisha nikaambiwa, "Inakubidi tena kutangaza ujumbe wa Mungu kuhusu watu wengi, mataifa, watu wa lugha nyingi na wafalme!"