[1]

Chapter 1

1: Mimi Paulo, mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu, na ndugu Timotheo, ninakuandikia wewe Filemoni mpendwa, mfanyakazi mwenzetu 2: na kanisa linalokutana nyumbani kwako, na wewe dada Afia, na askari mwenzetu Arkupo. 3: Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana yesu Kristo. 4: Kila wakati ninaposali nakukumbuka wewe Filemoni, na kumshukuru Mungu 5: maana nasikia habari za imani yako kwa Bwana wetu Yesu na upendo wako kwa watu wote wa Mungu. 6: Naomba ili imani hiyo unayoshiriki pamoja nasi ikuwezeshe kuwa na ujuzi mkamilifu zaidi wa baraka zote tunazopata katika kuungana kwetu na Kristo. 7: Ndugu, upendo wako yameniletea furaha kubwa na kunipa moyo sana! Nawe umeichangamsha mioyo ya watu wa Mungu. 8: Kwa sababu hiyo, ningeweza, kwa uhodari kabisa, nikiwa ndugu yako katika Kristo, kukuamuru ufanye unachopaswa kufanya. 9: Lakini kwa sababu ya upendo, ni afadhali zaidi nikuombe. Nafanya hivi ingawa mimi ni Paulo, balozi wa Kristo Yesu, na sasa pia mfungwa kwa ajili yake. 10: Basi, ninalo ombi moja kwako kuhusu mwanangu Onesimo, ambaye ni mwanangu katika Kristo kwani nimekuwa baba yake nikiwa kifungoni. 11: Ni Onesimo yuleyule ambaye wakati mmoja alikuwa hakufai kitu, lakini sasa ananifaa mimi na wewe pia. 12: Sasa namrudisha kwako, naye ni kama moyo wangu mimi mwenyewe. 13: Ningependa akae nami hapa anisaidie badala yako wakati niwapo kifungoni kwa sababu ya Habari Njema. 14: Lakini sitafanya chochote bila kibali chako. Sipendi kukulazimisha unisaidie, kwani wema wako unapaswa kutokana na hiari yako wewe mwenyewe na si kwa kulazimika. 15: Labda Onesimo aliondoka kwako kwa kitambo tu, kusudi uweze tena kuwa naye daima. 16: Na sasa yeye si mtumwa tu, ila ni bora zaidi ya mtumwa: yeye ni ndugu yetu mpenzi. Na wa maana sana kwangu mimi, na kwako atakuwa wa maana zaidi kama mtumwa na kama ndugu katika Bwana. 17: Basi, ikiwa wanitambua mimi kuwa mwenzako, mpokee tena kama vile ungenipokea mimi mwenyewe. 18: Kama alikuwa amekukosea kitu, au alikuwa na deni lako, basi, unidai mimi. 19: Naandika jambo hili kwa mkono wangu mwenyewe: yako.) 20: Haya, basi, ndugu yangu, nifanyie jambo hilo kwa ajili ya jina la Bwana; burudisha moyo wangu kama ndugu katika Kristo. 21: Naandika nikitumaini kwamba utanikubalia ombi langu; tena najua kwamba utafanya hata zaidi ya haya ninayokuomba. 22: Pamoja na hayo, nitayarishie chumba kwani natumaini kwamba kwa sala zenu, Mungu atanijalia niwatembeleeni. 23: Epafra, mfungwa mwenzangu kwa ajili ya Kristo Yesu, anakusalimu. 24: Nao akina Marko, Aristarko, Dema na Luka, wafanyakazi wenzangu, wanakusalimu. 25: Nawatakieni ninyi nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.