[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24] [25] [26] [27] [28]

Chapter 28

1: Baada ya Sabato, karibu na mapambazuko ya siku ile ya Jumapili, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kutazama lile kaburi. 2: Ghafla kutatokea tetemeko kubwa la nchi; malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akalivingirisha lile jiwe, akalikalia. 3: Alionekana kama umeme na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. 4: Walinzi wa lile kaburi wakatetemeka kwa hofu kubwa, hata wakawa kama wamekufa. 5: Lakini yule malaika akawaambia wale wanawake, "Ninyi msiogope! Najua kwamba mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. 6: Hayupo hapa maana amefufuka kama alivyosema. Njoni mkaone mahali alipokuwa amelala. 7: Basi, nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba amefufuka kutoka wafu, na sasa anawatangulieni kule Galilaya; huko mtamwona. Haya, mimi nimekwisha waambieni." 8: Wakiwa wenye hofu na furaha kubwa, hao wanawake walitoka upesi kaburini, wakakimbia kwenda kuwaambia wanafunzi wake. 9: Mara, Yesu akakutana nao, akawasalimu: "Salamu." Hao wanawake wakamwendea, wakapiga magoti mbele yake, wakashika miguu yake. 10: Kisha Yesu akawaambia, "Msiogope! Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, na huko wataniona." 11: Wale wanawake walipokuwa wanakwenda zao, baadhi ya walinzi wa lile kaburi walikwenda mjini kutoa taarifa kwa makuhani wakuu juu ya mambo yote yaliyotukia. 12: Basi, wakakutana pamoja na wazee, na baada ya kushauriana, wakawapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha 13: wakisema, "Ninyi mtasema hivi: `Wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba sisi tukiwa tumelala.` 14: Na kama mkuu wa mkoa akijua jambo hili, sisi tutasema naye na kuhakikisha kuwa ninyi hamtapata matatizo." 15: Wale walinzi wakazichukua zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Habari hiyo imeenea kati ya Wayahudi mpaka leo. 16: Wale wanafunzi kumi na mmoja walikwenda Galilaya kwenye ule mlima aliowaagiza Yesu. 17: Walipomwona, wakamwabudu, ingawa wengine walikuwa na mashaka. 18: Yesu akaja karibu, akawaambia, "Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19: Nendeni basi, mkawafanye watu wa mataifa yote wawe wanafunzi wangu; mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. 20: Wafundisheni kushika maagizo yote niliyowapeni. Nami nipo pamoja nanyi siku zote; naam, mpaka mwisho wa nyakati."