[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24] [25] [26] [27] [28]
Chapter 251:
"Wakati huo, Ufalme wa mbinguni utafanana na wasichana kumi waliochukua taa zao, wakaenda kumlaki bwana arusi.
2:
Watano miongoni mwao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara.
3:
Wale wapumbavu walichukua taa zao, lakini hawakuchukua akiba ya mafuta.
4:
Lakini wale wenye busara walichukua mafuta katika chupa pamoja na taa zao.
5:
Kwa kuwa bwana arusi alikawia kuja, wale wanawali wote wote walisinzia, wakalala.
6:
Usiku wa manane kukawa na kelele: `Haya, haya! Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki.`
7:
Hapo wale wanawali wote wakaamka, wakazitayarisha taa zao.
8:
Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara: `Tupeni mafuta yenu kidogo maana taa zetu zinazimika.`
9:
Lakini wale wenye busara wakawaambia, `Hayatatutosha sisi na ninyi! Afadhali mwende dukani mkajinunulie wenyewe!`
10:
Basi, wale wanawali wapumbavu walipokwenda kununua mafuta, bwana arusi akafika, na wale wanawali waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye katika jumba la arusi, kisha mlango ukafungwa.
11:
Baadaye wale wanawali wengine wakaja, wakaita: `Bwana, bwana, tufungulie!`
12:
Lakini yeye akawajibu, `Nawaambieni kweli, siwajui ninyi."`
13:
Kisha Yesu akasema, "Kesheni basi, kwa maana hamjui siku wala saa.
14:
"Itakuwa kama mtu mmoja aliyetaka kusafiri ng`ambo: aliwaita watumishi wake, akawakabidhi mali yake.
15:
Alimpa kila mmoja kadiri ya uwezo wake: mmoja sarafu tano za fedha ziitwazo talanta, mwingine talanta mbili na mwingine talanta moja, kisha akasafiri.
16:
Mara yule aliyekabidhiwa talanta tano akafanya kazi nazo akapata faida talanta tano.
17:
Hali kadhalika na yule aliyekabidhiwa talanta mbili akapata faida talanta mbili.
18:
Lakini yule aliyekabidhiwa talanta moja akaenda akachimba shimo ardhini, akaificha fedha ya bwana wake.
19:
"Baada ya muda mrefu, yule bwana alirudi, akaanza kukagua hesabu ya matumizi na mapato ya fedha yake.
20:
Mtumishi aliyekabidhiwa talanta tano akaja amechukua zile talanta tano faida, akamwambia, `Bwana, ulinikabidhi talanta tano, hapa pana talanta tano zaidi faida niliyopata.`
21:
Bwana wake akamwambia, `Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.`
22:
"Mtumishi aliyekabidhiwa talanta mbili akaja, akatoa talanta mbili faida, akisema, `Bwana, ulinikabidhi talanta mbili. Chukua talanta mbili zaidi faida niliyopata.`
23:
Bwana wake akamwambia, `Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.`
24:
"Lakini yule aliyekabidhiwa talanta moja akaja, akasema, `Bwana, najua wewe ni mtu mgumu; wewe huvuna pale ambapo hukupanda, na kukusanya pale ambapo hukutawanya.
25:
Niliogopa, nikaificha fedha yako katika ardhi. Chukua basi mali yako.`
26:
"Bwana wake akamwambia, `Wewe ni mtumishi mwovu na mvivu! Unajua kuwa mimi huvuna mahali ambapo sikupanda, na hukusanya pale ambapo sikutawanya.
27:
Ilikupasa basi, kuiweka fedha yangu katika benki, nami ningelichukua mtaji wangu na faida yake!
28:
Basi, mnyang`anyeni hiyo fedha mkampe yule mwenye talanta kumi.
29:
Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.
30:
Na kuhusu huyu mtumishi asiye na faida, mtupeni nje gizani! Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.`
31:
"Wakati Mwana wa Mtu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote wakiwa pamoja naye, hapo ataketi juu ya kiti chake cha enzi kitukufu,
32:
na mataifa yote yatakusanyika mbele yake, naye atawatenganisha watu kama mchungaji anavyotenganisha kondoo na mbuzi.
33:
Atawaweka kondoo upande wake wa kulia na mbuzi upande wake wa kushoto.
34:
"Kisha Mfalme atawaambia wale walio upande wake wa kulia, `Njoni enyi mliobarikiwa na Baba yangu; pokeeni Ufalme mliotayarishiwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu.
35:
Maana nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi mkanipa maji; nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha;
36:
nilikuwa uchi, mkanivika; nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kunitazama; nilikuwa gerezani nanyi mkaja kunitembelea.`
37:
Hapo, hao watu wema watamjibu mfalme `Bwana, ni lini tulikuona mwenye njaa nasi tukakupa chakula, au ukiwa na kiu nasi tukakunywesha maji?
38:
Ni lini tulikuona ukiwa mgeni nasi tukakukaribisha, au bila nguo nasi tukakuvika?
39:
Ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa au mfungwa nasi tukaja kukutazama?`
40:
Mfalme atawajibu, `Kweli nawaambieni, kila kitu mlichomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi.`
41:
"Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, `Ondokeni mbele yangu enyi mliolaaniwa! Nendeni katika moto wa milele aliotayarishiwa Ibilisi na malaika wake.
42:
Maana nilikuwa na njaa nanyi hamkunipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi hamkunipa maji.
43:
Nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha; nilikuwa mgonjwa na mfungwa nanyi hamkuja kunitazama.`
44:
"Hapo nao watajibu, `Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, ukiwa mgeni au bila nguo, ukiwa mgonjwa au mfungwa, nasi hatukuja kukuhudumia?`
45:
Naye atawajibu, `Nawaambieni kweli, kila mlipokataa kumtendea mambo haya mmojawapo wa hawa wadogo, mlikataa kunitendea mimi.`
46:
Basi, hawa watakwenda kwenye adhabu ya milele, lakini wale waadilifu watakwenda kwenye uzima wa milele."
|