[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24] [25] [26] [27] [28]
Chapter 241:
Yesu alitoka Hekaluni, na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake walimwendea, wakamwonyesha majengo ya Hekalu.
2:
Yesu akawaambia, "Sawa, mnaweza kuyatazama haya yote! Kweli nawaambieni, hakuna hata jiwe moja litakalosalia hapa juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa."
3:
Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni, wanafunzi walimwendea faraghani, wakamwuliza, "Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonyesha kuja kwako na mwisho wa nyakati?"
4:
Yesu akawajibu, "Jihadharini msije mkadanganywa na mtu.
5:
Maana wengi watatokea na kulitumia jina langu wakisema: `Mimi ndiye Kristo,` nao watawapotosha watu wengi.
6:
Mtasikia juu ya vita na fununu za vita; lakini msifadhaike, maana hayo hayana budi kutokea, lakini mwisho wenyewe ungali bado.
7:
Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. Hapa na pale patakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi.
8:
Yote hayo ni kama mwanzo wa maumivu ya kujifungua mtoto.
9:
"Kisha watawatoeni ili mteswe na kuuawa. Mataifa yote yatawachukieni kwa ajili ya jina langu.
10:
Tena, wengi wataiacha imani yao, watasalitiana na kuchukiana.
11:
Watatokea manabii wengi wa uongo watakaowapotosha watu wengi.
12:
Kwa sababu ya ongezeko la uhalifu, upendo wa watu wengi utafifia.
13:
Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ataokoka.
14:
Ila, kabla ya mwisho kufika, hii Habari Njema ya Ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote kama ushuhuda kwa mataifa yote.
15:
"Basi, mtakapoona `Chukizo Haribifu` lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu, (msomaji na atambue maana yake),
16:
hapo, walioko Yudea na wakimbilie milimani.
17:
Aliye juu ya paa la nyumba yake asishuke kuchukua kitu nyumbani mwake.
18:
Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake.
19:
Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo!
20:
Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe siku za baridi au siku ya Sabato!
21:
Maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka leo, wala haitapata kutokea tena.
22:
Kama siku hizo hazingalipunguzwa, hakuna binadamu yeyote ambaye angeokoka; lakini siku hizo zitapunguzwa kwa ajili ya wale walioteuliwa.
23:
"Basi, mtu akiwaambieni siku hizo: `Kristo yuko hapa` au `Yuko pale,` msimsadiki.
24:
Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo. Watafanya ishara kubwa na maajabu ya kuweza kuwapotosha ikiwezekana hata wateule wa Mungu.
25:
Sikilizeni, nimekwisha kuwaonya kabla ya wakati.
26:
Basi, wakiwaambieni, `Tazameni, yuko jangwani,` msiende huko; au, `Tazameni, amejificha ndani,` msisadiki;
27:
maana, kama vile umeme uangazavyo toka mashariki hadi magharibi, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu.
28:
Pale ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.
29:
"Mara baada ya dhiki ya siku hizo, jua litatiwa giza, mwezi hautaangaza, nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa.
30:
Kisha, ishara ya Mwana wa Mtu itaonekana angani, na hapo makabila yote duniani yatalalamika; watamwona Mwana wa Mtu akija juu ya mawingu ya angani mwenye nguvu na utukufu mwingi.
31:
Naye atawatuma malaika wake wenye tarumbeta la kuvuma sana, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, toka mwisho huu wa mbingu hadi mwisho huu.
32:
"Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.
33:
Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo haya yote yakitendeka, jueni kwamba yuko karibu sana.*fk*
34:
Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia.
35:
Naam, mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
36:
"Lakini, juu ya siku au saa hiyo, hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake ndiye ajuaye.
37:
Kwa maana kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu.
38:
Maana nyakati hizo, kabla ya gharika kuu, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka Noa alipoingia ndani ya ile safina.
39:
Hawakujua kuna nini mpaka ile gharika ilipotokea, ikawakumba wote. Ndivyo itakavyokuwa wakati Mwana wa Mtu atakapokuja.
40:
Wakati huo watu wawili watakuwa shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.
41:
Kina mama wawili watakuwa wanasaga nafaka, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.
42:
Basi, kesheni, kwa maana hamjui siku atakayokuja Bwana wenu.
43:
Lakini kumbukeni jambo hili: kama mwenye nyumba angejua siku mwizi atakapofika, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe.
44:
Kwa hiyo, nanyi pia muwe tayari, kwa maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia."
45:
Yesu akaendelea kusema, "Ni nani basi mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watu wake, awape chakula kwa wakati wake?
46:
Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakapokuja atamkuta akifanya hivyo.
47:
Kweli nawaambieni, atamweka mtumishi huyo aisimamie mali yake yote.
48:
Lakini kama mtumishi mbaya akijisemea moyoni: `Bwana wangu anakawia kurudi,`
49:
kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, akaanza kula na kunywa pamoja na walevi,
50:
bwana wake atakuja siku asiyoitazamia na saa asiyoijua.
51:
Atamkatilia mbali na kumweka kundi moja na wanafiki. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.
|