[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24] [25] [26] [27] [28]
Chapter 151:
Kisha Mafarisayo na walimu wa Sheria wakafika kutoka Yerusalemu, wakamwendea Yesu, wakamwuliza,
2:
"Kwa nini wanafunzi wako hawajali mapokeo tuliyopokea kutoka kwa wazee wetu? Hawanawi mikono yao kama ipasavyo kabla ya kula!"
3:
Yesu akawajibu, "Kwa nini nanyi mnapendelea mapokeo yenu wenyewe na hamuijali Sheria ya Mungu?
4:
Mungu amesema: `Waheshimu baba yako na mama yako,` na `Anayemkashifu baba yake au mama yake, lazima auawe`.
5:
Lakini ninyi mwafundisha ati mtu akiwa na kitu ambacho angeweza kuwasaidia nacho baba au mama yake, lakini akasema: `Kitu hiki nimemtolea Mungu,`
6:
basi, hapaswi tena kumheshimu baba yake! Ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa kufuata mafundisho yenu wenyewe.
7:
Enyi wanafiki! Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu:
8:
`Watu hawa, asema Mungu, huniheshimu kwa maneno tu, lakini mioyoni mwao wako mbali nami.
9:
Kuniabudu kwao hakufai, maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu."`
10:
Yesu aliuita ule umati wa watu, akawaambia, "Sikilizeni na muelewe!
11:
Kitu kinachomtia mtu najisi si kile kiingiacho kinywani, bali kile kitokacho kinywani. Hicho ndicho kimtiacho mtu najisi."
12:
Kisha wanafunzi wakamwendea, wakamwambia, "Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa waliposikia maneno yako?"
13:
Lakini yeye akawajibu, "Kila mmea ambao Baba yangu aliye mbinguni hakuupanda, utang`olewa.
14:
Waacheni wenyewe! Wao ni vipofu, viongozi wa vipofu; na kipofu akimwongoza kipofu, wote wawili hutumbukia shimoni."
15:
Petro akadakia, "Tufafanulie huo mfano."
16:
Yesu akasema, "Hata nyinyi hamwelewi?
17:
Je, hamwelewi kwamba kila kinachoingia kinywani huenda tumboni na baadaye hutupwa nje chooni?
18:
Lakini yale yatokayo kinywani hutoka moyoni, na hayo ndiyo yanayomtia mtu najisi.
19:
Maana moyoni hutoka mawazo maovu yanayosababisha uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na kashfa.
20:
Hayo ndiyo yanayomtia mtu najisi. Lakini kula chakula bila kunawa mikono hakumtii mtu najisi."
21:
Yesu aliondoka mahali hapo akaenda kukaa katika sehemu za Tiro na Sidoni.
22:
Basi, mama mmoja Mkaanani wa nchi hiyo alimjia, akapaaza sauti: "Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, nionee huruma! Binti yangu anasumbuliwa na pepo."
23:
Lakini Yesu hakumjibu neno. Basi, wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, "Mwambie aende zake kwa maana anatufuatafuata akipiga kelele."
24:
Yesu akajibu, "Sikutumwa ila kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo."
25:
Hapo huyo mama akaja, akapiga magoti mbele yake, akasema, "Mheshimiwa, nisaidie."
26:
Yesu akamjibu, "Si sawa kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa."
27:
Huyo mama akajibu, "Ni kweli, Mheshimiwa; lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka meza ya bwana wao."
28:
Hapo Yesu akamjibu, "Mama, imani yako ni kubwa; basi, ufanyiwe kama unavyotaka." Yule binti yake akapona tangu saa hiyo wakati huohuo.
29:
Yesu alitoka hapo akaenda kando ya ziwa Galilaya, akapanda mlimani, akaketi.
30:
Watu wengi sana wakamjia wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi waliokuwa wagonjwa, wakawaweka mbele ya miguu yake, naye Yesu akawaponya.
31:
Umati ule wa watu ulishangaa sana ulipoona bubu wakiongea, waliokuwa wamelemaa wamepona, viwete wakitembea na vipofu wakiona; wakamsifu Mungu wa Israeli.
32:
Basi, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akasema, "Nawaonea watu hawa huruma kwa sababu kwa siku tatu wamekuwa nami, wala hawana chakula. Sipendi kuwaacha waende bila kula wasije wakazimia njiani."
33:
Wanafunzi wakamwambia, "Hapa tuko nyikani; tutapata wapi chakula cha kuwatosha watu wengi hivi?"
34:
Yesu akawauliza, "Mnayo mikate mingapi?" Wakamjibu, "Saba na visamaki vichache."
35:
Basi, Yesu akawaamuru watu wakae chini.
36:
Akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi, nao wakawagawia watu.
37:
Wote wakala, wakashiba. Kisha wakakusanya makombo, wakajaza vikapu saba.
38:
Hao waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila kuhesabu wanawake na watoto.
39:
Basi, Yesu akawaaga watu, akapanda mashua, akaenda katika eneo la Magadani.
|