[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24] [25] [26] [27] [28]
Chapter 141:
Wakati huo, mtawala Herode alisikia sifa za Yesu.
2:
Basi, akawaambia watumishi wake, "Mtu huyu ni Yohane mbatizaji, amefufuka kutoka wafu; ndiyo maana nguvu za miujiza zinafanya kazi ndani yake."
3:
Herode ndiye aliyekuwa amemtia Yohane nguvuni, akamfunga minyororo na kumtia gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake. Sababu hasa ni
4:
kwamba alikuwa amemwambia Herode, "Si halali kwako kuishi na huyo mwanamke!"
5:
Herode alitaka kumwua Yohane, lakini aliogopa watu kwa sababu kwao Yohane alikuwa nabii.
6:
Katika sherehe za sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya wageni. Herode alifurahiwa,
7:
hata akaahidi kwa kiapo kumpa huyo msichana chochote atakachoomba.
8:
Naye, huku akichochewa na mama yake, akaomba, "Nipe papahapa katika sinia kichwa cha Yohane mbatizaji."
9:
Mfalme alihuzunika, lakini kwa sababu ya kile kiapo chake na kwa sababu ya wale wageni karamuni, akaamuru apewe.
10:
Basi, Herode akatuma mtu gerezani amkate kichwa Yohane.
11:
Kichwa chake kikaletwa katika sinia, wakampa yule msichana, naye akampelekea mama yake.
12:
Wanafunzi wa Yohane wakaja, wakauchukua mwili wake, wakauzika. Kisha wakaenda kumpasha habari Yesu.
13:
Yesu alipopata habari hiyo, aliondoka mahali pale kwa mashua, akaenda mahali pa faragha peke yake. Lakini watu walipata habari, wakamfuata kwa miguu toka mijini.
14:
Basi, aliposhuka pwani, aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, akawaponya wagonjwa wao.
15:
Kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea wakamwambia, "Mahali hapa ni nyikani, na saa zimepita. Basi, uwaage watu ili waende vijijini wakajinunulie chakula."
16:
Yesu akawaambia, "Si lazima waende, wapeni ninyi chakula."
17:
Lakini wao wakamwambia, "Tunayo mikate mitano tu na samaki wawili."
18:
Yesu akawaambia, "Nileteeni hapa."
19:
Akawaamuru watu waketi katika nyasi. Kisha akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akamshukuru Mungu. Halafu akaimega hiyo mikate, akawapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu.
20:
Watu wote wakala, wakashiba. Kisha wanafunzi wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu kumi na viwili.
21:
Jumla ya waliokula ilikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto.
22:
Mara, Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie ng`ambo ya ziwa wakati yeye anawaaga watu.
23:
Baada ya kuwaaga, alipanda mlimani peke yake kusali. Ilipokuwa jioni, yeye alikuwa huko peke yake,
24:
na wakati huo ile mashua ilikwishafika karibu katikati ya ziwa, lakini ilikuwa inakwenda mrama kwa sababu upepo ulikuwa unaipinga.
25:
Usiku, karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji.
26:
Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji waliingiwa na hofu, wakasema, "Ni mzimu!" Wakapiga kelele kwa hofu.
27:
Mara, Yesu akasema nao, "Tulieni, ni mimi. Msiogope!"
28:
Petro akamwambia, "Bwana, ikiwa ni wewe kweli, amuru nitembee juu ya maji nije kwako."
29:
Yesu akasema, "Haya, njoo." Basi, Petro akashuka kutoka ile mashua, akatembea juu ya maji, akamwendea Yesu.
30:
Lakini alipouona ule upepo, aliogopa, akaanza kuzama; akalia kwa sauti, "Bwana, niokoe!"
31:
Hapo, Yesu akaunyosha mkono wake, akamshika na kumwambia, "Ewe mwenye imani haba! Kwa nini uliona shaka?"
32:
Basi, wakapanda mashuani, na upepo ukatulia.
33:
Wote waliokuwa ndani ya mashua walimsujudia, wakasema, "Hakika wewe ni Mwana wa Mungu."
34:
Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti.
35:
Watu wa huko walipomtambua, wakaeneza habari pote katika sehemu hizo. Basi, wakamletea Yesu wagonjwa wote,
36:
wakamwomba awaruhusu waguse tu pindo la vazi lake; wote waliomgusa walipona.
|