[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24] [25] [26] [27] [28]

Chapter 10

1: Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa uwezo wa kutoa pepo wachafu na kuponya magonjwa na maradhi yote. 2: Majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya: wa kwanza ni Simoni aitwae Petro, na Andrea ndugu yake; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohane ndugu yake; 3: Filipo na Bartholomayo, Thoma na Mathayo aliyekuwa mtoza ushuru; Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo; 4: Simoni Mkanaani, na Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu. 5: Yesu aliwatuma hao kumi na wawili na kuwapa maagizo haya: "Msiende kwa watu wa mataifa mengine, wala msiingie katika mji wa Wasamaria. 6: Ila nendeni kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo. 7: Mnapokwenda hubirini hivi: `Ufalme wa mbinguni umekaribia.` 8: Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo. Mmepewa bure, toeni bure. 9: Msichukue mifukoni mwenu dhahabu, wala fedha, wala sarafu za shaba. 10: Msichukue mkoba wa kuombea njiani, wala koti la ziada, wala viatu, wala fimbo. Maana mfanyakazi anastahili riziki yake. 11: "Mkiingia katika mji wowote au kijiji, tafuteni humo mtu yeyote aliye tayari kuwakaribisheni, na kaeni naye mpaka mtakapoondoka mahali hapo. 12: Mnapoingia nyumbani wasalimuni wenyeji wake. 13: Kama wenyeji wa nyumba hiyo wakiipokea salamu hiyo, basi, amani yenu itakaa pamoja nao. Lakini ikiwa hawaipokei, basi amani yenu itawarudia ninyi. 14: Kama mtu yeyote atakataa kuwakaribisheni au kuwasikilizeni, basi mtokapo katika nyumba hiyo au mji huo, yakung`uteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao. 15: Kweli nawaambieni, Siku ya hukumu mji huo utapata adhabu kubwa kuliko ile iliyoipata miji ya Sodoma na Gomora. 16: "Sasa, mimi nawatuma ninyi kama kondoo kati ya mbwa mwitu. Muwe na busara kama nyoka, na wapole kama njiwa. 17: Jihadharini na watu, maana watawapeleka ninyi mahakamani na kuwapiga viboko katika masunagogi yao. 18: Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, mpate kutangaza Habari Njema kwao na kwa mataifa. 19: Basi, watakapowapeleka ninyi mahakamani, msiwe na wasiwasi mtasema nini au namna gani; wakati utakapofika, mtapewa la kusema. 20: Maana si ninyi mtakaosema, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. 21: "Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe, na baba atamsaliti mwanawe, nao watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua. 22: Watu wote watawachukieni kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ataokolewa. 23: "Watu wakiwadhulumu katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Kweli nawaambieni, hamtamaliza ziara yenu katika miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Mtu hajafika. 24: "Mwanafunzi si mkuu kuliko mwalimu wake, wala mtumishi si mkuu kuliko bwana wake. 25: Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mkubwa wa jamaa Beelzebuli, je hawatawaita watu wengine wa jamaa hiyo majina mabaya zaidi? 26: "Basi, msiwaogope watu hao. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, na kila kilichofichwa kitafichuliwa. 27: Ninalowaambieni ninyi katika giza, lisemeni katika mwanga; na jambo mlilosikia likinong`onezwa, litangazeni hadharani. 28: Msiwaogope wale wauao mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja na roho katika moto wa Jehanamu. 29: Shomoro wawili huuzwa kwa senti tano. Lakini hata mmoja wao haanguki chini bila kibali cha Baba yenu. 30: Lakini kwa upande wenu, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. 31: Kwa hiyo msiogope; ninyi mu wa thamani kuliko shomoro wengi. ic 32: "Kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, mimi pia nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. 33: Lakini yeyote atakayenikana hadharani, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. 34: "Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga. 35: Maana nimekuja kuleta mafarakano kati ya mtu na baba yake, kati ya binti na mama yake, kati ya mkwe na mkwe wake. 36: Na maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake. 37: "Ampendaye baba au mama yake kuliko anipendavyo mimi, hanistahili. Ampendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. 38: Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata, hanistahili. 39: Anayeyashikilia maisha yake, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata. 40: "Anayewakaribisha ninyi, ananikaribisha mimi; na anayenikaribisha mimi, anamkaribisha yule aliyenituma. 41: Anayemkaribisha nabii kwa sababu ni nabii, atapokea tuzo la nabii. Anayemkaribisha mtu mwema kwa sababu ni mtu mwema, atapokea tuzo la mtu mwema. 42: Kweli nawaambieni, yeyote atakayempa mmojawapo wa wadogo hawa kikombe cha maji baridi kwa sababu ni mfuasi wangu, hatakosa kamwe kupata tuzo lake."