[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24] [25] [26] [27] [28]

Chapter 4

1: Kisha Roho alimwongoza Yesu mpaka jangwani ili ajaribiwe na Ibilisi. 2: Akafunga siku arubaini mchana na usiku, na mwishowe akaona njaa. 3: Basi, mshawishi akamjia, akamwambia, "Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate." 4: Yesu akamjibu, "Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu: `Binadamu hataishi kwa mikate tu, ila kwa kila neno asemalo Mungu."` 5: Kisha Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, mji mtakatifu, akamweka juu ya mnara wa hekalu, 6: akamwambia, "Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, jitupe chini; maana imeandikwa: `Mungu atawaamuru malaika wake kwa ajili yako; watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe."` 7: Yesu akamwambia, "Imeandikwa pia: `Usimjaribu Bwana, Mungu wako."` 8: Kisha Ibilisi akamchukua mpaka juu ya mlima mrefu, akamwonyesha falme zote za ulimwengu na fahari zake, 9: akamwambia, "Hivi vyote nitakupa kama tu ukipiga magoti na kuniabudu." 10: Hapo, Yesu akamwambia, "Nenda zako Shetani! Imeandikwa: `Utamwabudu Bwana Mungu wako na kumtumikia yeye peke yake."` 11: Basi, Ibilisi akamwacha, na malaika wakaja, wakamhudumia. 12: Yesu aliposikia kwamba Yohane ametiwa gerezani alikwenda Galilaya. 13: Aliondoka Nazareti, akaenda Kafarnaumu, mji ulio kando ya bahari ya Genesareti, mpakani mwa wilaya za Zabuloni na Naftali, akakaa huko. 14: Ndivyo lilivyotimia lile neno lililosemwa kwa njia ya nabii Isaya: 15: "Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, kuelekea baharini ng`ambo ya mto Yordani, Galilaya nchi ya watu wa Mataifa! 16: Watu waliokaa gizani wameona mwanga mkubwa. Nao walioishi katika nchi ya giza na kivuli cha kifo, mwanga umewaangazia!" 17: Tangu wakati huo Yesu alianza kuhubiri akisema, "Tubuni, maana ufalme wa mbinguni umekaribia!" 18: Yesu alipokuwa anatembea kando ya ziwa Galilaya, aliwaona ndugu wawili wavuvi; Simoni (aitwae Petro) na Andrea, ndugu yake; walikuwa wakivua samaki kwa nyavu ziwani. 19: Basi, akawaambia, "Nifuateni, nami nitawafanya ninyi wavuvi wa watu." 20: Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. ic 21: Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona ndugu wengine wawili: Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Hao walikuwa ndani ya mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakitengeneza nyavu zao. Basi Yesu akawaita, 22: nao mara wakaiacha mashua pamoja na baba yao, wakamfuata. 23: Yesu alikuwa anakwenda kila mahali wilayani Galilaya, akifundisha katika masunagogi na kuhubiri Habari Njema juu ya ufalme wa Mungu. Aliponya kila namna ya maradhi na magonjwa waliyokuwa nayo watu. 24: Habari zake zikaenea katika mkoa wote wa Siria. Wagonjwa wote wenye maradhi ya kila namna na wale waliosumbuliwa na kila namna ya taabu: waliopagawa na pepo, wenye kifafa na watu waliokuwa wamelemaa, walipelekwa kwake; naye akawaponya wote. 25: Makundi mengi ya watu kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Yudea na ng`ambo ya mto Yordani, walimfuata.