[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16]

Chapter 16

1: Baada ya siku ya Sabato, Maria Magdalene, Salome na Maria mama yake Yakobo walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Yesu. 2: Basi, alfajiri na mapema siku ya Jumapili, jua lilipoanza kuchomoza, walienda kaburini. 3: Nao wakawa wanaambiana, "Nani atakayetuondolea lile jiwe mlangoni mwa kaburi?" 4: Lakini walipotazama, waliona jiwe limekwisha ondolewa. (Nalo lilikuwa kubwa mno.) 5: Walipoingia kaburini, walimwona kijana mmoja aliyevaa vazi jeupe, ameketi upande wa kulia; wakashangaa sana. 6: Lakini huyo kijana akawaambia, "Msishangae. Mnamtafuta Yesu wa Nazareti aliyesulubiwa. Amefufuka, hayumo hapa. Tazameni mahali walipokuwa wamemlaza. 7: Nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro ya kwamba anawatangulieni kule Galilaya. Huko mtamwona kama alivyowaambieni." 8: Basi, wakatoka pale kaburini mbio, maana walitetemeka kwa hofu na kushangaa. Hawakumwambia mtu yeyote kitu, kwa sababu waliogopa mno. 9: Yesu alipofufuka mapema Jumapili, alijionyesha kwanza kwa Maria Magdalene, ambaye Yesu alikuwa amemtoa pepo saba. 10: Maria Magdalene akaenda, akawajulisha wale waliokuwa pamoja na Yesu, na wakati huo walikuwa wanaomboleza na kulia. 11: Lakini waliposikia ya kwamba Yesu yu hai na kwamba Maria Magdalene amemwona, hawakuamini. 12: Baadaye Yesu aliwatokea wanafunzi wawili akiwa na sura nyingine. Wanafunzi hao walikuwa wanakwenda shambani. 13: Nao pia wakaenda wakawaambia wenzao. Hata hivyo hawakuamini. 14: Mwishowe, Yesu aliwatokea wanafunzi kumi na mmoja walipokuwa pamoja mezani. Akawakemea sana kwa sababu ya kutoamini kwao na ukaidi wao, maana hawakuwaamini wale waliokuwa wamemwona baada ya kufufuka. 15: Basi, akawaambia, "Nendeni ulimwenguni kote mkahubiri Habari Njema kwa kila mtu. 16: Anayeamini na kubatizwa ataokolewa; asiyeamini atahukumiwa. 17: Na ishara hizi zitaandamana na wale wanaoamini: kwa jina langu watatoa pepo na watasema kwa lugha mpya. 18: Wakishika nyoka au wakinywa kitu chochote chenye sumu, hakitawadhuru. Watawawekea wagonjwa mikono, nao watapona." 19: Basi, Bwana Yesu alipokwisha sema nao, akachukuliwa mbinguni, akaketi upande wa kulia wa Mungu. 20: Wanafunzi wakaenda wakihubiri kila mahali. Bwana akafanya kazi pamoja nao na kuimarisha ujumbe huo kwa ishara zilizoandamana nao.*fi*