[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16]

Chapter 13

1: Yesu alipokuwa anatoka Hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, "Mwalimu, tazama jinsi mawe haya na majengo haya yalivyo ya ajabu!" 2: Yesu akamwambia, "Je, unayaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitabomolewa." 3: Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni akielekea Hekalu, Petro, Yakobo, Yohane na Andrea wakamwuliza kwa faragha, 4: "Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonyesha kwamba mambo haya karibu yatimizwe?" 5: Yesu akaanza kuwaambia, "Jihadharini msije mkadanganywa na mtu. 6: Maana wengi watakuja wakilitumia jina langu, wakisema, `Mimi ndiye!` nao watawapotosha watu wengi. 7: Mtakaposikia juu ya vita na fununu za vita, msifadhaike. Mambo hayo lazima yatokee, lakini mwisho wenyewe ungali bado. 8: Taifa moja litapigana na taifa lingine; utawala mmoja utapigana na utawala mwingine; kila mahali kutakuwa na mitetemeko ya ardhi na njaa. Mambo haya ni kama tu maumivu ya kwanza ya kujifungua mtoto. 9: "Lakini ninyi jihadharini. Maana watu watawapelekeni mahakamani, na kuwapigeni katika masunagogi. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu ili mpate kunishuhudia kwao. 10: Lakini lazima kwanza Habari Njema ihubiriwe kwa mataifa yote. 11: Nao watakapowatieni nguvuni na kuwapeleka mahakamani, msiwe na wasiwasi juu ya yale mtakayosema; saa ile itakapofika, semeni chochote mtakachopewa, maana si ninyi mtakaosema, bali Roho Mtakatifu. 12: Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe; baba atamsaliti mwanae; watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua. 13: Watu wote watawachukieni ninyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa. 14: "Mtakapoona `Chukizo Haribifu` limesimama mahali ambapo si pake, (msomaji na atambue maana yake!) Hapo watu walioko Yudea wakimbilie milimani. 15: Mtu aliye juu ya paa la nyumba asishuke kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu. 16: Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake. 17: Ole wao waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo! 18: Ombeni ili mambo hayo yasitukie nyakati za baridi. 19: Maana wakati huo kutakuwa na dhiki ambayo haijatokea tangu Mungu alipoumba ulimwengu mpaka leo, wala haitatokea tena. 20: Kama Bwana asingepunguza siku hizo, hakuna binadamu ambaye angeokolewa. Lakini kwa ajili ya wateule wake, Bwana amezipunguza siku hizo. 21: "Basi mtu akiwaambieni, `Tazama, Kristo yupo hapa!` au `Yupo pale!` msimsadiki. 22: Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo, watafanya ishara na maajabu, ili kuwapotosha wateule wa Mungu, kama ikiwezekana. 23: Lakini ninyi jihadharini. Mimi nimewaambieni mambo yote kabla hayajatokea. 24: "Basi, siku hizo baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza na mwezi hautaangaza. 25: Nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa. 26: Hapo watamwona Mwana wa Mtu akija katika mawingu kwa nguvu nyingi na utukufu. 27: Kisha atawatuma malaika wake; atawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu. 28: "Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. 29: Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo hayo yakitendeka, jueni kwamba Mwana wa Mtu yuko karibu sana. 30: Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia. 31: Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. 32: "Lakini hakuna mtu ajuaye siku au saa hiyo itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye. 33: Muwe waangalifu na kesheni, maana hamjui wakati huo utafika lini. 34: Itakuwa kama mtu anayeondoka nyumbani kwenda safari akiwaachia watumishi wake madaraka, kila mmoja na kazi yake; akamwambia mlinzi wa mlango awe macho. 35: Kesheni, basi, kwa maana hamjui mwenye nyumba atarudi lini; huenda ikawa jioni, usiku wa manane, alfajiri au asubuhi. 36: Kesheni ili akija ghafla asije akawakuta mmelala. 37: Ninayowaambieni ninyi, nawaambia wote: Kesheni!"