[1]
[2]
[3]
[4]
[5]
[6]
[7]
[8]
[9]
[10]
[11]
[12]
[13]
[14]
[15]
[16]
Chapter 131:
Yesu alipokuwa anatoka Hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, "Mwalimu, tazama jinsi mawe haya na majengo haya yalivyo ya ajabu!"
2:
Yesu akamwambia, "Je, unayaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitabomolewa."
3:
Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni akielekea Hekalu, Petro, Yakobo, Yohane na Andrea wakamwuliza kwa faragha,
4:
"Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonyesha kwamba mambo haya karibu yatimizwe?"
5:
Yesu akaanza kuwaambia, "Jihadharini msije mkadanganywa na mtu.
6:
Maana wengi watakuja wakilitumia jina langu, wakisema, `Mimi ndiye!` nao watawapotosha watu wengi.
7:
Mtakaposikia juu ya vita na fununu za vita, msifadhaike. Mambo hayo lazima yatokee, lakini mwisho wenyewe ungali bado.
8:
Taifa moja litapigana na taifa lingine; utawala mmoja utapigana na utawala mwingine; kila mahali kutakuwa na mitetemeko ya ardhi na njaa. Mambo haya ni kama tu maumivu ya kwanza ya kujifungua mtoto.
9:
"Lakini ninyi jihadharini. Maana watu watawapelekeni mahakamani, na kuwapigeni katika masunagogi. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu ili mpate kunishuhudia kwao.
10:
Lakini lazima kwanza Habari Njema ihubiriwe kwa mataifa yote.
11:
Nao watakapowatieni nguvuni na kuwapeleka mahakamani, msiwe na wasiwasi juu ya yale mtakayosema; saa ile itakapofika, semeni chochote mtakachopewa, maana si ninyi mtakaosema, bali Roho Mtakatifu.
12:
Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe; baba atamsaliti mwanae; watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua.
13:
Watu wote watawachukieni ninyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa.
14:
"Mtakapoona `Chukizo Haribifu` limesimama mahali ambapo si pake, (msomaji na atambue maana yake!) Hapo watu walioko Yudea wakimbilie milimani.
15:
Mtu aliye juu ya paa la nyumba asishuke kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu.
16:
Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake.
17:
Ole wao waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo!
18:
Ombeni ili mambo hayo yasitukie nyakati za baridi.
19:
Maana wakati huo kutakuwa na dhiki ambayo haijatokea tangu Mungu alipoumba ulimwengu mpaka leo, wala haitatokea tena.
20:
Kama Bwana asingepunguza siku hizo, hakuna binadamu ambaye angeokolewa. Lakini kwa ajili ya wateule wake, Bwana amezipunguza siku hizo.
21:
"Basi mtu akiwaambieni, `Tazama, Kristo yupo hapa!` au `Yupo pale!` msimsadiki.
22:
Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo, watafanya ishara na maajabu, ili kuwapotosha wateule wa Mungu, kama ikiwezekana.
23:
Lakini ninyi jihadharini. Mimi nimewaambieni mambo yote kabla hayajatokea.
24:
"Basi, siku hizo baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza na mwezi hautaangaza.
25:
Nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa.
26:
Hapo watamwona Mwana wa Mtu akija katika mawingu kwa nguvu nyingi na utukufu.
27:
Kisha atawatuma malaika wake; atawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu.
28:
"Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.
29:
Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo hayo yakitendeka, jueni kwamba Mwana wa Mtu yuko karibu sana.
30:
Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia.
31:
Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
32:
"Lakini hakuna mtu ajuaye siku au saa hiyo itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye.
33:
Muwe waangalifu na kesheni, maana hamjui wakati huo utafika lini.
34:
Itakuwa kama mtu anayeondoka nyumbani kwenda safari akiwaachia watumishi wake madaraka, kila mmoja na kazi yake; akamwambia mlinzi wa mlango awe macho.
35:
Kesheni, basi, kwa maana hamjui mwenye nyumba atarudi lini; huenda ikawa jioni, usiku wa manane, alfajiri au asubuhi.
36:
Kesheni ili akija ghafla asije akawakuta mmelala.
37:
Ninayowaambieni ninyi, nawaambia wote: Kesheni!"
|