[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16]

Chapter 5

1: Basi, wakafika katika nchi ya Wagerase, ng`ambo ya ziwa. 2: Mara tu Yesu aliposhuka mashuani, mtu mmoja aliyepagawa na pepo mchafu alitoka makaburini, akakutana naye. 3: Mtu huyo alikuwa akiishi makaburini wala hakuna mtu aliyeweza tena kumfunga kwa minyororo. 4: Mara nyingi walimfunga kwa pingu na minyororo lakini kila mara aliweza kuikata hiyo minyororo na kuzivunja hizo pingu, wala hakuna mtu aliyeweza kumzuia. 5: Mchana na usiku alikaa makaburini na milimani akipaaza sauti na kujikatakata kwa mawe. 6: Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia, akamwinamia 7: akisema kwa sauti kubwa, "Una shauri gani nami, wewe Yesu Mwana wa Mungu aliye juu? Kwa jina la Mungu, nakusihi usinitese!" 8: Alisema hivyo kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, "Pepo mchafu, mtoke mtu huyu.") 9: Basi, Yesu akamwuliza, "Jina lako nani?" Naye akajibu, "Jina langu ni `Jeshi`, maana sisi tu wengi." 10: Kisha akamsihi Yesu asiwafukuze hao pepo katika nchi ile. 11: Kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe malishoni kwenye mteremko wa mlima. 12: Basi, hao pepo wakamsihi, "Utupeleke kwa hao nguruwe, tuwaingie." 13: Naye akawaruhusu. Basi, hao pepo wachafu wakatoka, wakawaingia wale nguruwe. Kundi lote la nguruwe wapatao elfu mbili likaporomoka kwenye ule mteremko mkali mpaka ziwani, likatumbukia majini. 14: Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakatangaza jambo hilo mjini na mashambani. Watu wakafika kuona yaliyotukia. 15: Wakamwendea Yesu, wakamwona na mtu yuleyule aliyekuwa amepagawa na jeshi la pepo ameketi chini, amevaa nguo na ana akili yake sawa, wakaogopa. 16: Watu walishuhudia tukio hilo wakaeleza wengine mambo yaliyompata huyo mtu aliyekuwa amepagawa na pepo na juu ya wale nguruwe. 17: Basi, wakaanza kumwomba aondoke katika nchi yao. 18: Yesu alipokuwa anapanda mashuani, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akamwomba amruhusu kwenda naye. 19: Lakini Yesu akamkatalia. Badala yake akamwambia, "Nenda nyumbani kwa jamaa yako, ukawaambie mambo yote Bwana aliyokutendea na jinsi alivyokuonea huruma." 20: Basi, huyo mtu akaenda, akaanza kutangaza huko Dekapoli mambo yote Yesu aliyomtendea; watu wote wakashangaa. 21: Yesu alivukia tena upande wa pili wa ziwa kwa mashua. Umati mkubwa wa watu ukakusanyika mbele yake, naye akawa amesimama kando ya ziwa. 22: Hapo akaja mmojawapo wa maofisa wa sunagogi, jina lake Yairo. Alipomwona Yesu, akajitupa mbele ya miguu yake, 23: akamsihi akisema, "Binti yangu mdogo ni mgonjwa karibu kufa. Twende tafadhali, ukamwekee mikono yako, apate kupona na kuishi." 24: Basi, Yesu akaondoka pamoja naye. Watu wengi sana wakamfuata, wakawa wanamsonga kila upande. 25: Mmojawapo alikuwa mwanamke mwenye ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. 26: Mwanamke huyo alikuwa amekwisha sumbuka sana kuwaendea waganga wengi. Na ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote, hakupata nafuu bali hali yake ilizidi kuwa mbaya. 27: Alikuwa amesikia habari za Yesu, na hivyo akaupenya msongamano wa watu kutoka nyuma, akagusa vazi lake. 28: Alifanya hivyo, maana alijisemea, "Nikigusa tu vazi lake, nitapona." 29: Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, akajisikia mwilini mwake kwamba ameponywa ugonjwa wake. 30: Yesu alitambua mara kwamba nguvu imemtoka. Basi akaugeukia ule umati wa watu, akauliza, "Nani aliyegusa mavazi yangu?" 31: Wanafunzi wake wakamjibu, "Unaona jinsi watu wanavyokusonga; mbona wauliza nani aliyekugusa?" 32: Lakini Yesu akaendelea kutazama amwone huyo aliyefanya hivyo. 33: Hapo huyo mwanamke, akifahamu yaliyompata, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa chini mbele ya Yesu na kusema ukweli wote. 34: Yesu akamwambia, "Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako." 35: Yesu alipokuwa bado anaongea, watu walifika kutoka nyumbani kwa yule ofisa wa sunagogi, wakamwambia, "Binti yako amekwisha kufa. Ya nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?" 36: Lakini, bila kujali walichosema, Yesu akamwambia mkuu wa sunagogi, "Usiogope, amini tu." 37: Wala hakumruhusu mtu yeyote kufuatana naye ila Petro, Yakobo na Yohane nduguye Yakobo. 38: Wakafika nyumbani kwa ofisa wa sunagogi naye Yesu akasikia makelele, kilio na maombolezo mengi. 39: Akaingia ndani, akawaambia, "Mbona mnapiga kelele na kulia? Msichana hakufa, amelala tu." 40: Lakini wao wakamcheka. Basi, akawaondoa wote nje, akawachukua baba na mama ya huyo msichana na wale wanafunzi wake, wakaingia chumbani alimokuwa huyo msichana. 41: Kisha akamshika mkono, akamwambia, "Talitha, kumi," maana yake, "Msichana, nakwambia, amka!" 42: Mara msichana akasimama, akaanza kutembea. (Alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili.) Hapo watu wakashangaa kupita kiasi. 43: Yesu akawakataza sana wasimjulishe mtu jambo hilo. Kisha akawaambia wampe huyo msichana chakula.