[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16]

Chapter 4

1: Yesu alianza kufundisha tena akiwa kando ya ziwa. Umati mkubwa wa watu ulimzunguka hata ikambidi aingie katika mashua na kuketi. Watu wakawa wamekaa katika nchi kavu, kando ya ziwa. 2: Aliwafundisha mambo mengi kwa mifano, na katika mafundisho yake aliwaambia, 3: "Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. 4: Alipokuwa akipanda, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila. 5: Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi. Mbegu hizo ziliota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina. 6: Jua lilipochomoza, zikachomeka; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka. 7: Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga, nazo hazikuzaa nafaka. 8: Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikakua na kuzaa: moja punje thelathini, moja sitini na nyingine mia." 9: Kisha akawaambia, "Mwenye masikio na asikie!" 10: Yesu alipokuwa peke yake, baadhi ya wale waliomsikia walimwendea pamoja na wale kumi na wawili, wakamwuliza juu ya hiyo mifano. 11: Naye akawaambia, "Ninyi mmejaliwa kujua siri ya Utawala wa Mungu, lakini wale walio nje wataambiwa kila kitu kwa mifano, 12: ili, `Watazame kweli, lakini wasione. Wasikie kweli, lakini wasielewe. La sivyo, wangemgeukia Mungu, naye angewasamehe."` 13: Basi, Yesu akawauliza, "Je, ninyi hamwelewi mfano huu? Mtawezaje basi, kuelewa mfano wowote? 14: Mpanzi hupanda neno la Mungu. 15: Watu wengine ni kama wale walio njiani ambapo mbegu zilianguka. Hawa hulisikia hilo neno lakini mara Shetani huja na kuliondoa neno hilo lililopandwa ndani yao. 16: Watu wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa penye mawe. Mara tu wanapolisikia hilo neno hulipokea kwa furaha. 17: Lakini haliwaingii na kuwa na mizizi ndani yao; huendelea kulizingatia kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya hilo neno mara wanakata tamaa. 18: Watu wengine ni kama zile mbegu zilizoanguka penye miti ya miiba. Huo ni mfano wa wale wanaolisikia hilo neno, 19: lakini wasiwasi wa ulimwengu huu, anasa za mali na tamaa za kila namna huwaingia na kulisonga hilo neno, nao hawazai matunda. 20: Lakini wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa katika udongo mzuri. Hawa hulisikia hilo neno, wakalipokea, wakazaa matunda: wengine thelathini, wengine sitini na wengine mia moja." 21: Yesu akaendelea kuwaambia, "Je, watu huwasha taa wakaileta ndani na kuifunika kwa pishi au kuiweka mvunguni? La! Huiweka juu ya kinara. 22: Basi, kila kilichofichwa kitafichuliwa, na kila kilichofunikwa kitafunuliwa. 23: Mwenye masikio na asikie!" 24: Akawaambia pia, "Sikilizeni kwa makini mnachosikia! Kipimo kilekile mnachowapimia watu wengine, ndicho mtakachopimiwa; tena mtazidishiwa. 25: Aliye na kitu atapewa zaidi; asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa." 26: Yesu akaendelea kusema, "Ufalme wa Mungu ni kama ifuatavyo. Mtu hupanda mbegu shambani. 27: Usiku hulala, mchana yu macho na wakati huo mbegu zinaota na kukua; yeye hajui inavyofanyika. 28: Udongo wenyewe huiwezesha mimea kukua na kuzaa matunda: kwanza huchipua jani changa, kisha suke, na mwishowe nafaka ndani ya suke. 29: Nafaka inapoiva, huyo mtu huanza kutumia mundu wake, maana wakati wa mavuno umefika." 30: Tena, Yesu akasema, "Tuufananishe Utawala wa Mungu na nini? Tuueleze kwa mifano gani? 31: Ni kama mbegu ya haradali ambayo ni ndogo kuliko mbegu zote. 32: Lakini ikisha pandwa, huota na kuwa mmea mkubwa kuliko mimea yote ya shambani. Matawi yake huwa makubwa hata ndege wa angani huweza kujenga viota vyao katika kivuli chake." 33: Yesu aliwahubiria ujumbe wake kwa mifano mingine mingi ya namna hiyo; aliongea nao kadiri walivyoweza kusikia. 34: Hakuongea nao chochote bila kutumia mifano; lakini alipokuwa pamoja na wanafunzi wake peke yao alikuwa akiwafafanulia kila kitu. 35: Jioni, siku hiyohiyo, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, "Tuvuke ziwa, twende ng`ambo." 36: Basi, wakauacha ule umati wa watu, wakamchukua Yesu katika mashua alimokuwa. Palikuwapo pia mashua nyingine hapo. 37: Basi, dhoruba kali ikaanza kuvuma, mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikaanza kujaa maji. 38: Yesu alikuwa sehemu ya nyuma ya mashua, amelala juu ya mto. Basi, wanafunzi wakamwamsha na kumwambia, "Mwalimu, je, hujali kwamba sisi tunaangamia?" 39: Basi, akaamka, akaukemea ule upepo na kuyaamrisha mawimbi ya ziwa, "Kimya! Tulia!" Hapo upepo ukakoma, kukawa shwari kabisa. 40: Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Mbona mnaogopa? Je, bado hamna imani?" 41: Nao wakaogopa sana, wakawa wanaulizana, "Huyu ni nani basi, hata upepo na mawimbi vinamtii?"