[1]
[2]
[3]
[4]
[5]
[6]
[7]
[8]
[9]
[10]
[11]
[12]
[13]
[14]
[15]
[16]
[17]
[18]
[19]
[20]
[21]
[22]
[23]
[24]
Chapter 241:
Jumapili, alfajiri na mapema, wale wanawake walikwenda kaburini wakichukua yale manukato waliyotayarisha.
2:
Walikuta lile jiwe limeviringishwa mbali na kaburi.
3:
Walipoingia ndani, hawakuona mwili wa Bwana Yesu.
4:
Walipokuwa bado wanashangaa juu ya jambo hilo, mara watu wawili waliovaa mavazi yenye kung`aa sana, wakasimama karibu nao.
5:
Hao wanawake wakaingiwa na hofu, wakainama chini. Ndipo wale watu wakawaambia, "Kwa nini mnamtafuta aliye hai kati ya wafu?
6:
Hayuko hapa; amefufuka. Kumbukeni aliyowaambieni alipokuwa kule Galilaya:
7:
`Ni lazima Mwana wa Mtu atolewe kwa watu waovu, nao watamsulubisha, na siku ya tatu atafufuka."`
8:
Hapo wanawake wakayakumbuka maneno yake,
9:
wakarudi kutoka kaburini, wakawapa mitume wale kumi na mmoja na wengine habari za mambo hayo yote.
10:
Hao waliotoa habari hizo kwa mitume ni: Maria Magdalene, Yoana na Maria mama wa Yakobo, pamoja na wanawake wengine walioandamana nao.
11:
Mitume waliyachukua maneno hayo kama yasiyo na msingi, hivyo hawakuamini.
12:
Lakini Petro alitoka, akaenda mbio hadi kaburini. Alipoinama kuchungulia ndani, akaiona tu ile sanda. Akarudi nyumbani huku akiwa anashangaa juu ya hayo yaliyotokea.
13:
Siku hiyohiyo, wawili kati ya wafuasi wake Yesu wakawa wanakwenda katika kijiji kimoja kiitwacho Emau, umbali wa kilomita kumi na moja kutoka Yerusalemu.
14:
Wakawa wanazungumza juu ya hayo yote yaliyotukia.
15:
Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akatokea, akatembea pamoja nao.
16:
Walimwona kwa macho, lakini hawakumtambua.
17:
Akawauliza, "Mnazungumza nini huku mnatembea?" Nao wakasimama kimya, nyuso zao wamezikunja kwa huzuni.
18:
Mmoja, aitwaye Kleopa, akamjibu, "Je, wewe ni mgeni peke yako Yerusalemu ambaye hujui yaliyotukia huko siku hizi?"
19:
Naye akawajibu, "Mambo gani?" Wao wakamjibu, "Mambo yaliyompata Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii mwenye uwezo wa kutenda na kufundisha mbele ya Mungu na mbele ya watu wote.
20:
Makuhani na watawala wetu walimtoa ahukumiwe kufa, wakamsulubisha.
21:
Lakini sisi tulitumaini kwamba yeye ndiye angeikomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu mambo hayo yalipotendeka.
22:
Tena, wanawake wengine wa kwetu wametushtua. Walikwenda kaburini mapema asubuhi,
23:
wasiukute mwili wake. Wakarudi wakasema kwamba walitokewa na malaika waliowaambia kwamba alikuwa hai.
24:
Wengine wetu walikwenda kaburini wakashuhudia yale waliyosema hao wanawake; ila yeye hawakumwona."
25:
Kisha Yesu akawaambia, "Mbona mu wapumbavu kiasi hicho na mioyo yenu ni mizito hivyo kusadiki yote yaliyonenwa na manabii?
26:
Je, haikumpasa Kristo kuteswa, na hivyo aingie katika utukufu wake?"
27:
Akawafafanulia mambo yote yaliyomhusu yeye katika Maandiko Matakatifu kuanzia Mose hadi manabii wote.
28:
Walipokikaribia kile kijiji walikokuwa wanakwenda, Yesu akafanya kana kwamba anaendelea na safari;
29:
lakini wao wakamsihi wakisema, "Kaa pamoja nasi, maana kunakuchwa, na usiku unakaribia." Basi, akaingia kijijini, akakaa pamoja nao.
30:
Alipoketi kula chakula pamoja nao, akachukua mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.
31:
Mara macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua; lakini yeye akatoweka kati yao.
32:
Basi, wakaambiana, "Je, mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu wakati alipokuwa anatufafanulia Maandiko Matakatifu kule njiani?"
33:
Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemu: wakawakuta wale mitume kumi na mmoja na wale wengine waliokuwa pamoja nao, wamekusanyika
34:
wakisema, "Hakika Bwana amefufuka, amemtokea Simoni."
35:
Basi, hao wafuasi wawili wakawajulisha yale yaliyowapata njiani, na jinsi walivyomtambua katika kumega mkate.
36:
Wanafunzi wote wawili walipokuwa wakiwaambia hayo, Yesu mwenyewe akasimama kati yao, akawaambia "Amani kwenu."
37:
Wakashtuka na kushikwa na hofu wakidhani wameona mzimu.
38:
Lakini yeye akawaambia, "Kwa nini mnafadhaika? Mbona mnakuwa na mashaka mioyoni mwenu?
39:
Angalieni mikono na miguu yangu, ya kwamba ni mimi mwenyewe. Nipapaseni mkanione, maana mzimu hauna mwili na mifupa kama mnionavyo."
40:
Baada ya kusema hayo, akawaonyesha mikono na miguu.
41:
Wakiwa bado katika hali ya kutosadiki kwa sababu ya furaha yao, na wakiwa wanastaajabu, akawauliza, "Mnacho chakula chochote hapa?"
42:
Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa.
43:
Akakichukua, akala, wote wakimwona.
44:
Halafu akawaambia, "Hii ndiyo maana ya maneno niliyowaambia nilipokuwa pamoja nanyi: kwamba ilikuwa lazima kukamilisha yote yaliyoandikwa juu yangu katika Sheria ya Mose na katika vitabu vya manabii na katika kitabu cha Zaburi."
45:
Kisha, akaziangazia akili zao ili wapate kuelewa Maandiko Matakatifu.
46:
Akawaambia, "Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka wafu,
47:
na kwamba ni lazima, kwa jina lake, mataifa yote kuanzia na Yerusalemu yahubiriwe juu ya kutubu na kusamehewa dhambi.
48:
Ninyi ni mashahidi wa mambo hayo.
49:
Nami mwenyewe nitawapelekeeni yule ambaye Baba aliahidi kumtuma, lakini ngojeni huku mjini mpaka mtakapopewa ile nguvu itokayo juu."
50:
Kisha akawaongoza nje ya mji hadi Bethania, akainua mikono yake juu, akawabariki.
51:
Alipokuwa anawabariki, akawaacha; akachukuliwa mbinguni.
52:
Wao wakamwabudu, wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kubwa:
53:
wakakaa muda wote Hekaluni wakimsifu Mungu.
|