[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24]

Chapter 22

1: Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa inakaribia. 2: Makuhani wakuu na walimu wa Sheria wakawa wanatafuta njia ya kumwua Yesu, lakini waliwaogopa watu. 3: Basi, Shetani akamwingia Yuda aitwae Iskarioti, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. 4: Yuda akaenda akajadiliana na makuhani wakuu na walinzi wa Hekalu kuhusu atakavyomsaliti Yesu kwao. 5: Nao wakafurahi na kupatana naye kumlipa fedha. 6: Yuda akakubali, na akawa anatafuta nafasi nzuri ya kumkabidhi kwao bila umati wa watu kujua. 7: Basi, siku ya Mikate Isiyotiwa chachu ikafika. Hiyo ndiyo siku ambayo mwana kondoo wa Pasaka huchinjwa. 8: Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohane, akawaambia, "Nendeni mkatuandalie karamu ili tupate kula Pasaka." 9: Nao wakamwuliza, "Unataka tuiandae wapi?" 10: Akawaambia, "Sikilizeni! Mtakapokuwa mnakwenda mjini, mtakutana na mwanamume anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka ndani ya nyumba atakayoingia. 11: Mwambieni mwenye nyumba: `Mwalimu anakuuliza, kiko wapi kile chumba ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?` 12: Naye atawaonyesheni chumba kikubwa ghorofani ambacho kimepambwa. Andalieni humo." 13: Basi, wakaenda, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia; wakaandaa karamu ya Pasaka. 14: Saa ilipotimia, Yesu akakaa kula chakula pamoja na mitume wake. 15: Akawaambia, "Nimetamani sana kula Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu. 16: Maana nawaambieni, sitaila tena hadi hapo itakapokamilika katika Ufalme wa Mungu." 17: Kisha akatwaa kikombe, akashukuru akasema, "Pokeeni, mgawanye ninyi kwa ninyi. 18: Kwa maana nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka Ufalme wa Mungu utakapokuja." 19: Halafu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema, "Huu ni mwili wangu, unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka." 20: Akafanya vivyo hivyo na kikombe, baada ya chakula, akisema, "Kikombe hiki ni agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu inayomwagika kwa ajili yenu.*fd* 21: "Lakini, tazameni! Yule atakayenisaliti yuko nami hapa mezani. 22: Kweli Mwana wa Mtu anakwenda kuuawa kama ilivyopangwa, lakini ole wake mtu anayemsaliti." 23: Hapo wakaanza kuulizana wao kwa wao ni nani kati yao atakayefanya jambo hilo. 24: Kulitokea ubishi kati ya hao mitume kuhusu nani miongoni mwao anayefikiriwa kuwa mkuu zaidi kuliko wengine. 25: Yesu akawaambia, "Wafalme wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, nao huitwa wafadhili wa watu. 26: Lakini isiwe hivyo kati yenu; bali, yule aliye mkuu kati yenu ni lazima awe mdogo wa wote, na aliye kiongozi lazima awe kama mtumishi. 27: Kwa maana, ni nani aliye mkuu: yule anayeketi mezani kula chakula, ama yule anayetumikia? Bila shaka ni yule anayeketi mezani kula chakula! Hata hivyo, mimi niko hapa kati yenu kama mtumishi. 28: "Ninyi ndio mliobaki nami wakati wote wa majaribu yangu; 29: na, kama vile Baba yangu alivyonikabidhi Ufalme, vivyo hivyo nami nitawakabidhi ninyi Ufalme. 30: Mtakula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu, na mtaketi katika viti vya enzi kuyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. 31: "Simoni, Simoni! Sikiliza! Shetani alitaka kuwapepeta ninyi kama mtu anavyopepeta ngano. 32: Lakini mimi nimekuombea ili imani yako isipungue. Nawe utakaponirudia, watie moyo ndugu zako." 33: Naye Petro akamjibu, "Bwana, mimi niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani, na hata kufa." 34: Yesu akamjibu, "Nakwambia wewe Petro, kabla jogoo hajawika leo utakuwa umenikana mara tatu." 35: Kisha, Yesu akawauliza wanafunzi wake, "Wakati nilipowatuma bila mfuko wa fedha wala mkoba wala viatu, mlitindikiwa chochote?" Wakajibu, "La." 36: Naye akawaambia, "Lakini sasa, yule aliye na mfuko wa fedha auchukue; na aliye na mkoba, hali kadhalika. Na yeyote asiye na upanga, auze koti lake anunue mmoja. 37: Maana nawaambieni, haya maneno ya Maandiko Matakatifu: `Aliwekwa kundi moja na wahalifu,` ni lazima yatimie. Naam, yale yanayonihusu yanafikia ukamilifu wake." 38: Nao wakasema, "Bwana, tazama; hapa kuna panga mbili." Naye akasema, "Basi!" 39: Yesu akatoka, na kama ilivyokuwa desturi yake, akaenda katika mlima wa Mizeituni; wanafunzi wake wakamfuata. 40: Alipofika huko akawaambia, "Salini, msije mkaingia katika kishawishi." 41: Kisha akawaacha, akaenda umbali wa mtu kuweza kutupa jiwe, akapiga magoti, akasali: 42: "Baba, kama wapenda, ukiondoe kwangu kikombe hiki; hata hivyo, mapenzi yako yatimizwe, wala siyo yangu." 43: Hapo, malaika kutoka mbinguni, akamtokea ili kumtia moyo. 44: Akiwa katika uchungu mkubwa, alisali kwa bidii zaidi; na jasho likamtoka, kama matone ya damu, likatiririka mpaka chini.*fe* ic 45: Baada ya kusali, aliwarudia wanafunzi wake, akawakuta wamelala, kwani walikuwa na huzuni. 46: Akawaambia, "Mbona mnalala? Amkeni msali, msije mkaingia katika kishawishi." 47: Alipokuwa bado anaongea, kundi la watu likaja likiongozwa na yule aliyeitwa Yuda, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. Yuda akaenda kumsalimu Yesu kwa kumbusu. 48: Lakini Yesu akamwambia, "Yuda! Je, unamsaliti Mwana wa Mtu kwa kumbusu?" 49: Wale wanafunzi wake walipoona hayo wakasema, "Bwana, tutumie panga zetu?" 50: Na mmoja wao akampiga upanga mtumishi wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio lake la kulia. 51: Hapo, Yesu akasema, "Acha! Hii inatosha." Akaligusa sikio la mtu huyo akaliponya. 52: Kisha Yesu akawaambia makuhani wakuu, wakubwa wa walinzi wa Hekalu na wazee waliokuja kumkamata: "Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang`anyi? 53: Nilipokuwa pamoja nanyi kila siku Hekaluni hamkunitia nguvuni. Lakini, huu ndio wakati wenu hasa, ndio wakati wa utawala wa giza." 54: Basi, wakamkamata, wakamchukua na kwenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Petro akawa anamfuata nyuma kwa mbali. 55: Moto ulikuwa umewashwa katikati ya ua, nao wakawa wameketi pamoja Petro akiwa miongoni mwao. 56: Mjakazi mmoja alipomwona Petro ameketi karibu na moto, akamkodolea macho, akasema, "Mtu huyu alikuwa pia pamoja na Yesu." 57: Lakini Petro akakana akisema, "Wee! simjui mimi." 58: Baadaye kidogo, mtu mwingine akamwona Petro, akasema, "Wewe ni mmoja wao." Lakini Petro akajibu "Bwana we; si mimi!" 59: Kama saa moja baadaye, mtu mwingine akasisitiza, "Hakika huyu alikuwa pamoja naye; ametoka Galilaya ati." 60: Lakini Petro akasema, "Bwana wee; sijui hata unachosema!" Na papo hapo, akiwa bado anaongea, jogoo akawika. 61: Bwana akageuka na kumtazama Petro, naye Petro akakumbuka yale aliyokuwa ameambiwa na Bwana: "Leo kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu." 62: Hapo akatoka nje, akalia sana. 63: Wale watu waliokuwa wanamchunga Yesu, walimpiga na kumdhihaki. 64: Walimfunga kitambaa usoni, wakawa wanamwuliza, "Ni nani aliyekupiga? Hebu bashiri tuone!" 65: Wakamtolea maneno mengi ya matusi. 66: Kulipokucha, kikao cha wazee wa watu kilifanyika, ambacho kilihudhuriwa na makuhani wakuu na walimu wa Sheria. Yesu akaletwa mbele ya Baraza hilo. 67: Nao wakamwambia, "Twambie! Je, wewe ndiwe Kristo?" Lakini Yesu akawaambia, "Hata kama nikiwaambieni, hamtasadiki; 68: na hata kama nikiwaulizeni swali, hamtanijibu. 69: Lakini tangu sasa, Mwana wa Mtu atakuwa ameketi upande wa kulia wa Mungu Mwenyezi." 70: Hapo wote wakasema, "Ndiyo kusema wewe ni Mwana wa Mungu?" Naye akasema, "Ninyi mnasema kwamba mimi ndiye." 71: Nao wakasema, "Je, tunahitaji ushahidi mwingine? Sisi wenyewe tumesikia akisema kwa mdomo wake mwenyewe."sw4323