[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24]

Chapter 21

1: Yesu alitazama kwa makini, akawaona matajiri walivyokuwa wanatia sadaka zao katika hazina ya Hekalu, 2: akamwona pia mama mmoja mjane akitumbukiza humo sarafu mbili ndogo. 3: Basi, akasema, "Nawaambieni kweli, mama huyu mjane ametia zaidi katika hazina kuliko wote. 4: Kwa maana, wengine wote wametoa sadaka zao kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu mama, ingawa ni maskini, ametoa kila kitu alichohitaji kwa kuishi." 5: Baadhi ya wanafunzi walikuwa wanazungumza juu ya Hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe ya thamani, pamoja na sadaka zilizotolewa kwa Mungu. Yesu akasema, 6: "Haya yote mnayoyaona--zitakuja siku ambapo hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa." 7: Basi, wakamwuliza, "Mwalimu, mambo hayo yatatokea lini? Na ni ishara gani zitakazoonyesha kwamba karibu mambo hayo yatokee?" 8: Yesu akawajibu, "Jihadharini, msije mkadanganyika. Maana wengi watatokea na kulitumia jina langu wakisema: `Mimi ndiye`, na, `Wakati ule umekaribia`. Lakini ninyi msiwafuate! 9: Basi, mtakaposikia habari za vita na misukosuko, msitishike; maana ni lazima hayo yatokee kwanza, lakini mwisho wa yote, bado." 10: Halafu akaendelea kusema: "Taifa moja litapigana na taifa lingine, na ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. 11: Kila mahali kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, kutakuwa na njaa na tauni. Kutakuwa na vituko vya kutisha na ishara kubwa angani. 12: Lakini kabla ya kutokea hayo yote, watawatieni nguvuni, watawatesa na kuwapelekeni katika masunagogi na kuwatia gerezani; mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya jina langu. 13: Hii itawapeni fursa ya kushuhudia Habari Njema. 14: Muwe na msimamo huu mioyoni mwenu: hakuna kufikiria kabla ya wakati juu ya jinsi mtakavyojitetea, 15: kwa sababu mimi mwenyewe nitawapeni ufasaha wa maneno na hekima, hivyo kwamba zenu hawataweza kustahimili wala kupinga. 16: Wazazi wenu, ndugu, jamaa na rafiki zenu watawasaliti ninyi; na baadhi yenu mtauawa. 17: Watu wote watawachukieni kwa sababu ya jina langu. 18: Lakini, hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea. 19: Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu. 20: "Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo mtambue ya kwamba wakati umefika ambapo mji huo utaharibiwa. 21: Hapo walioko Yudea wakimbilie milimani; wale walio mjini watoke; na wale walio mashambani wasirudi mjini. 22: Kwa maana siku hizo ni siku za adhabu, ili yote yaliyoandikwa yatimie. 23: Ole wao waja wazito na wanyonyeshao siku hizo! Kwa maana kutakuwa na dhiki kubwa katika nchi, na hasira ya Mungu itawajia watu hawa. 24: Wengine watauawa kwa upanga, wengine watachukuliwa mateka katika nchi zote; na mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa mataifa mengine, hadi nyakati zao zitakapotimia. 25: "Kutakuwa na ishara katika jua na mwezi na nyota. Mataifa duniani yatakuwa na dhiki kwa sababu ya wasiwasi kutokana na mshindo wa mawimbi ya bahari. 26: Watu watazirai kwa sababu ya uoga, wakitazamia mambo yatakayoupata ulimwengu; kwa maana nguvu za mbingu zitatikiswa. 27: Halafu, watamwona Mwana wa Mtu akija katika wingu, mwenye nguvu na utukufu mwingi. 28: Wakati mambo hayo yatakapoanza kutukia, simameni na kuinua vichwa vyenu juu, kwa maana ukombozi wenu umekaribia." 29: Kisha akawaambia mfano: "Angalieni mtini na miti mingine yote. 30: Mnapoona kwamba imeanza kuchipua majani, mwatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. 31: Vivyo hivyo, mtakapoona mambo hayo yanatendeka, mtatambua kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia. 32: Nawaambieni hakika, kizazi hiki cha sasa hakitapita kabla ya hayo yote kutendeka. 33: Mbingu na dunia vitapita, lakini maneno yangu hayatapita. 34: "Muwe macho, mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na shughuli za maisha haya. La sivyo, Siku ile itawajieni ghafla. 35: Kwa maana itawajia kama mtego, wote wanaoishi duniani pote. 36: Muwe waangalifu basi, na salini daima ili muweze kupata nguvu ya kupita salama katika mambo haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele ya Mwana wa Mtu." 37: Wakati wa mchana, siku hizo, Yesu alikuwa akifundisha watu Hekaluni; lakini usiku alikuwa akienda katika mlima wa Mizeituni na kukaa huko. 38: Watu wote walikuwa wanakwenda Hekaluni asubuhi na mapema, wapate kumsikiliza.