[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24]

Chapter 19

1: Yesu aliingia mjini Yeriko, akawa anapita katika njia za mji huo. 2: Kulikuwa na mtu mmoja mjini, jina lake Zakayo ambaye alikuwa mkuu wa watoza ushuru tena mtu tajiri. 3: Alitaka kuona Yesu alikuwa nani, lakini kwa sababu ya umati wa watu, na kwa vile alikuwa mfupi, hakufaulu. 4: Hivyo, alitangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu ili aweze kumwona Yesu, kwa maana alikuwa apitie hapo. 5: Basi, Yesu alipofika mahali pale, aliangalia juu akamwambia, "Zakayo, shuka upesi, maana leo ni lazima nishinde nyumbani mwako." 6: Zakayo akashuka haraka, akamkaribisha kwa furaha. 7: Watu wote walipoona hayo, wakaanza kunung`unika wakisema, "Amekwenda kukaa kwa mtu mwenye dhambi." 8: Lakini Zakayo akasimama akamwambia Yesu, "Sikiliza Bwana! Mimi nitawapa maskini nusu ya mali yangu, na kama nimenyang`anya mtu yeyote kitu, nitamrudishia mara nne." 9: Yesu akamwambia, "Leo wokovu umefika katika nyumba hii, kwa vile huyu pia ni wa ukoo wa Abrahamu. 10: Kwa maana Mwana wa Mtu amekuja kutafuta na kuokoa waliopotea." ic 11: Wakati watu walipokuwa bado wanasikiliza hayo, Yesu akawaambia mfano. (Hapo alikuwa anakaribia Yerusalemu, na watu wale walidhani kwamba muda si muda, Ufalme wa Mungu ungefika.) 12: Hivyo akawaambia, "Kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa kifalme aliyefanya safari kwenda nchi ya mbali ili apokee madaraka ya ufalme, halafu arudi. 13: Basi, kabla ya kuondoka aliwaita watumishi wake kumi, akawapa kiasi cha fedha kila mmoja na kumwambia: `Fanyeni nazo biashara mpaka nitakaporudi.` 14: Lakini wananchi wenzake walimchukia na hivyo wakatuma wajumbe waende wakaseme: `Hatumtaki huyu atutawale.` 15: "Huyo mtu mashuhuri alirudi nyumbani baada ya kufanywa mfalme, na mara akaamuru wale watumishi aliowapa zile fedha waitwe ili aweze kujua kila mmoja amepata faida gani. 16: Mtumishi wa kwanza akatokea, akasema: `Mheshimiwa, faida iliyopatikana ni mara kumi ya zile fedha ulizonipa.` 17: Naye akamwambia: `Vema; wewe ni mtumishi mwema. Kwa kuwa umekuwa mwaminifu katika jambo dogo, utakuwa na madaraka juu ya miji kumi!` 18: Mtumishi wa pili akaja, akasema: `Mheshimiwa, faida iliyopatikana ni mara tano ya zile fedha ulizonipa.` 19: Naye akamwambia pia: `Nawe utakuwa na madaraka juu ya miji mitano.` 20: "Mtumishi mwingine akaja, akasema: `Chukua fedha yako; niliificha salama katika kitambaa, 21: kwa maana niliogopa kwa sababu wewe ni mtu mkali. Wewe ni mtu ambaye huchukua yasiyo yako, na huchuma ambacho hukupanda.` 22: Naye akamwambia: `Nakuhukumu kutokana na msemo wako, ewe mtumishi mbaya! Ulijua kwamba mimi ni mtu mkali, ambaye huchukua yasiyo yangu na kuchuma nisichopanda. 23: Kwa nini basi, hukuiweka fedha yangu benki, nami ningeichukua pamoja na faida baada ya kurudi kwangu?` 24: Hapo akawaambia wale waliokuwa pale: `Mnyang`anyeni hizo fedha, mkampe yule aliyepata faida mara kumi.` 25: Nao wakamwambia: `Lakini Mheshimiwa, huyo ana faida ya kiasi hicho mara kumi!` 26: Naye akawajibu: `Kila aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa. 27: Na sasa, kuhusu hao maadui wangu ambao hawapendi niwe mfalme wao, waleteni hapa, mkawaue papa hapa mbele yangu."` 28: Yesu alisema hayo, kisha akatangulia mbele yao kuelekea Yerusalemu. 29: Alipokaribia kufika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, 30: akawaambia: "Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwana punda amefungwa ambaye hajatumiwa na mtu. Mfungeni, mkamlete hapa. 31: Kama mtu akiwauliza, kwa nini mnamfungua, mwambieni, `Bwana ana haja naye."` 32: Basi, wakaenda, wakakuta sawa kama alivyowaambia. 33: Walipokuwa wanamfungua yule mwana punda, wenyewe wakawauliza, "Kwa nini mnamfungua mwana punda huyu?" 34: Nao wakawajibu, "Bwana anamhitaji." 35: Basi, wakampelekea Yesu yule mwana punda. Kisha wakatandika mavazi yao juu yake wakampandisha Yesu. 36: Yesu akaendelea na safari, na watu wakatandaza mavazi yao barabarani. 37: Alipofika karibu na Yerusalemu, katika mteremko wa mlima wa Mizeituni, umati wote na wanafunzi wake, wakaanza kushangilia na kumtukuza Mungu kwa sauti kubwa, kwa sababu ya mambo makuu waliyoyaona; 38: wakawa wanasema: "Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana. Amani mbinguni, na utukufu juu mbinguni!" 39: Hapo baadhi ya Mafarisayo waliokuwako katika lile kundi la watu, wakamwambia Yesu, "Mwalimu, wanyamazishe wanafunzi wako!" 40: Yesu akawajibu, "Nawaambieni, kama hawa wakinyamaza, hakika hayo mawe yatapaza sauti." 41: Alipokaribia zaidi na kuuona ule mji, Yesu aliulilia 42: akisema: "Laiti ungelijua leo hii yale yaletayo amani! Lakini sasa yamefichika machoni pako. 43: Maana siku zaja ambapo adui zako watakuzungushia maboma, watakuzingira na kukusonga pande zote. 44: Watakupondaponda wewe pamoja na watoto wako ndani ya kuta zako; hawatakuachia hata jiwe moja juu jingine, kwa sababu hukuutambua wakati Mungu alipokujia kukuokoa." 45: Kisha, Yesu aliingia Hekaluni, akaanza kuwafukuzia nje wafanyabiashara 46: akisema, "Imeandikwa: `Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala`; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang`anyi." 47: Yesu akawa anafundisha kila siku Hekaluni. Makuhani wakuu, walimu wa Sheria na viongozi wa watu walitaka kumwangamiza, 48: lakini hawakuwa na la kufanya, maana watu wote walikuwa wakimsikiliza kwa makini kabisa.