[1]
[2]
[3]
[4]
[5]
[6]
[7]
[8]
[9]
[10]
[11]
[12]
[13]
[14]
[15]
[16]
[17]
[18]
[19]
[20]
[21]
[22]
[23]
[24]
Chapter 181:
Basi, Yesu aliwasimulia mfano kuonyesha kwamba ni lazima kusali daima bila kukata tamaa.
2:
Alisema: "Katika mji mmoja kulikuwa na hakimu ambaye hakuwa anamcha Mungu wala kumjali binadamu.
3:
Katika mji huohuo, kulikuwa pia na mama mmoja mjane, ambaye alimwendea huyo hakimu mara nyingi akimwomba amtetee apate haki yake kutoka kwa adui yake.
4:
Kwa muda mrefu huyo hakimu hakupenda kumtetea huyo mjane; lakini, mwishowe akajisemea: `Ingawa mimi simchi Mungu wala simjali binadamu,
5:
lakini kwa vile huyu mjane ananisumbua, nitamtetea; la sivyo ataendelea kufika hapa, na mwisho atanichosha kabisa!"`
6:
Basi, Bwana akaendelea kusema, "Sikieni jinsi alivyosema huyo hakimu mbaya.
7:
Je, ndio kusema Mungu hatawatetea wale aliowachagua, ambao wanamlilia mchana na usiku? Je, atakawia kuwasikiliza?
8:
Nawaambieni atawatetea upesi. Hata hivyo, je, kutakuwako na imani duniani wakati Mwana wa Mtu atakapokuja?"
9:
Halafu Yesu aliwaambia pia mfano wa wale ambao walijiona kuwa wema na kuwadharau wengine.
10:
"Watu wawili walipanda kwenda Hekaluni kusali: mmoja Mfarisayo, na mwingine mtoza ushuru.
11:
Huyo Mfarisayo akasimama, akasali kimoyomoyo: `Ee Mungu, nakushukuru kwa vile mimi si kama watu wengine: walafi, wadanganyifu au wazinzi. Nakushukuru kwamba mimi si kama huyu mtoza ushuru.
12:
Nafunga mara mbili kwa juma, natoa zaka sehemu ya kumi ya pato langu.`
13:
Lakini yule mtoza ushuru, akiwa amesimama kwa mbali bila hata kuinua macho yake mbinguni, ila tu akijipiga kifua kwa huzuni, alisema: `Ee Mungu, unionee huruma mimi mwenye dhambi.`
14:
Nawaambieni, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amesamehewa. Lakini yule mwingine, sivyo. Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, na kila anayejishusha atakwezwa."
15:
Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono yake. Wanafunzi walipowaona, wakawazuia kwa maneno makali.
16:
Lakini Yesu akawaita kwake akisema: "Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu kama hawa.
17:
Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hataingia katika Ufalme huo."
18:
Kiongozi mmoja, Myahudi, alimwuliza Yesu, "Mwalimu mwema, nifanye nini ili niweze kuupata uzima wa milele?"
19:
Yesu akamwambia, "Mbona waniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake.
20:
Unazijua amri: `Usizini; usiue; usiibe; usitoe ushahidi wa uongo; waheshimu baba yako na mama yako."`
21:
Yeye akasema, "Hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu."
22:
Yesu aliposikia hayo akamwambia, "Unatakiwa bado kufanya kitu kimoja: uza kila ulicho nacho, wagawie maskini, na hivyo utakuwa na hazina yako mbinguni; halafu njoo unifuate."
23:
Lakini huyo mtu aliposikia hayo, alihuzunika sana kwa sababu alikuwa tajiri sana.
24:
Yesu alipoona akihuzunika hivyo, akasema, "Jinsi gani ilivyo vigumu kwa matajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!
25:
Naam, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu."
26:
Wale watu waliposikia hayo, wakasema, "Nani basi, atakayeokolewa?"
27:
Yesu akajibu, "Yasiyowezekana kwa binadamu, yanawezekana kwa Mungu."
28:
Naye Petro akamwuliza, "Na sisi je? Tumeacha vitu vyote tukakufuata!"
29:
Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, mtu yeyote aliyeacha nyumba au mke au kaka au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu,
30:
atapokea mengi zaidi wakati huu wa sasa, na kupokea uzima wa milele wakati ujao."
31:
Yesu aliwachukua kando wale kumi na wawili, akawaambia, "Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu na huko kila kitu kilichoandikwa na manabii kuhusu Mwana wa Mtu kitakamilishwa.
32:
Kwa maana atakabidhiwa kwa watu wa mataifa nao watamtendea vibaya na kumtemea mate.
33:
Watampiga mijeledi, watamuua; lakini siku ya tatu atafufuka."
34:
Lakini wao hawakuelewa hata kidogo jambo hilo; walikuwa wamefichwa maana ya maneno hayo, na hawakutambua yaliyosemwa.
35:
Wakati Yesu alipokaribia Yeriko, kulikuwa na mtu mmoja kipofu ameketi njiani akiomba.
36:
Aliposikia umati wa watu ukipita aliuliza, "Kuna nini?"
37:
Wakamwambia, "Yesu wa Nazareti anapita."
38:
Naye akapaza sauti akisema, "Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!"
39:
Wale watu waliotangulia wakamkemea wakimwambia anyamaze; lakini yeye akazidi kupaza sauti: "Mwana wa Daudi, nihurumie;"
40:
Yesu alisimama, akaamuru wamlete mbele yake. Yule kipofu alipofika karibu, Yesu akamwuliza,
41:
"Unataka nikufanyie nini?" Naye akamjibu, "Bwana, naomba nipate kuona tena."
42:
Yesu akamwambia, "Ona! Imani yako imekuponya."
43:
Na mara yule aliyekuwa kipofu akapata kuona, akamfuata Yesu akimtukuza Mungu. Watu wote walipoona hayo, wakamsifu Mungu.
|