[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24]

Chapter 16

1: Yesu aliwaambia wanafunzi wake: "Tajiri mmoja alikuwa na karani wake. Huyu karani alichongewa kwamba alitumia ovyo mali ya tajiri wake. 2: Yule tajiri akamwita akamwambia: `Ni mambo gani haya ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya mapato na matumizi ya mali yangu, kwa maana huwezi kuwa karani tena.` 3: Yule karani akafikiri: `Bwana wangu amenifukuza kazi ya ukarani; nitafanya nini? Kwenda kulima siwezi; kwenda kuombaomba kama maskini ni aibu. 4: Naam, najua la kufanya, ili nitakapofukuzwa kazi, watu waweze kunikaribisha nyumbani kwao.` 5: Basi, akawaita wadeni wa bwana wake, mmoja mmoja, akamwambia yule wa kwanza: `Unadaiwa kiasi gani na bwana wangu?` 6: Yeye akamjibu: `Mapipa mia ya mafuta ya zeituni.` Yule karani akamwambia: `Chukua hati yako ya deni, keti haraka, andika hamsini.` 7: Kisha akamwuliza mdeni mwingine: `Wewe unadaiwa kiasi gani?` Yeye akamjibu: `Magunia mia ya ngano.` Yule karani akamwambia: `Chukua hati yako ya deni, andika themanini.` 8: "Basi, yule bwana akamsifu huyo karani asiye mwaminifu, kwa kuwa alitumia busara. Kwa maana watu wa dunia hii wana busara zaidi na mambo yao kuliko watu wa mwanga." 9: Naye Yesu akaendelea kusema, "Nami nawaambieni, jifanyieni marafiki kutokana na mali ya dunia, ili zitakapowaishieni, mweze kupokewa nao katika makao ya milele. 10: Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, atakuwa mwaminifu katika mambo makubwa; na yeyote asiye mwaminifu katika mambo madogo, hatakuwa mwaminifu katika mambo makubwa. 11: Kama basi, ninyi si hamjawa waaminifu mali mbaya za dunia, ni nani atakayewakabidhi zile mali za kweli? 12: Na kama hamjakuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewakabidhi mali yenu wenyewe? 13: "Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia mmoja na kumpenda mwingine, au ataambatana na mmoja na kumdharau mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali." 14: Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, kwa vile wao walikuwa wanapenda sana fedha, wakamdharau Yesu. 15: Hapo akawaambia, "Ninyi mnajifanya wema mbele ya watu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana kile kinachoonekana kuwa kitukufu mbele ya watu, Mungu anakiona kuwa takataka. 16: "Sheria na maandishi ya manabii vilikuweko mpaka wakati wa Yohane mbatizaji. Tangu hapo, Ufalme wa Mungu unahubiriwa, na kila mmoja anauingia kwa nguvu. 17: Lakini ni rahisi zaidi mbingu na dunia kupita, kuliko hata herufi moja ya Sheria kufutwa. 18: "Yeyote anayemwacha mke wake na kuoa mwingine, anazini; na yeyote anayemwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini. 19: "Palikuwa na mtu mmoja tajiri, ambaye alikuwa anavaa mavazi ya bei kubwa sana ya rangi ya zambarau, na ya kitani safi, na kufanya sherehe kila siku. 20: Kulikuwa pia na maskini mmoja jina lake Lazaro, aliyekuwa amejaa vidonda na alikuwa analazwa mlangoni pa nyumba ya huyo tajiri. 21: Lazaro alitamani kula makombo yaliyoanguka kutoka meza ya tajiri; na zaidi ya hayo, mbwa walikuwa wanakuja na kulamba vidonda vyake! 22: "Ikatokea kwamba huyo maskini akafa, malaika wakamchukua, wakamweka karibu na Abrahamu. Na yule tajiri pia akafa, akazikwa. 23: Huyo tajiri, alikuwa na mateso makali huko kuzimu, akainua macho yake, akamwona Abrahamu kwa mbali na Lazaro karibu naye. 24: Basi, akaita kwa sauti: `Baba Abrahamu, nionee huruma; umtume Lazaro angalau achovye ncha ya kidole chake katika maji, auburudishe ulimi wangu, maana ninateseka mno katika moto huu.` 25: Lakini Abrahamu akamjibu: `Kumbuka mwanangu, kwamba ulipokea mema yako katika maisha, naye Lazaro akapokea mabaya. Sasa lakini, yeye anatulizwa, nawe unateswa. 26: Licha ya hayo, kati yetu na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wanaotaka kuja kwenu kutoka huku wasiweze, wala wanaotaka kutoka kwenu kuja kwetu wasiweze.` 27: Huyo aliyekuwa tajiri akasema: `Basi baba, nakuomba umtume aende nyumbani kwa baba yangu, 28: maana ninao ndugu watano, ili awaonye wasije wakaja huku kwenye mateso.` 29: Lakini Abrahamu akamwambia: `Ndugu zako wanao Mose na manabii; waache wawasikilize hao.` 30: Lakini yeye akasema: `Sivyo baba Abrahamu, ila kama mtu atafufuka kutoka wafu na kuwaendea, watatubu.` 31: Naye Abrahamu akasema: `Kama hawawasikilizi Mose na manabii, hawatajali hata kama mtu angefufuka kutoka wafu."`