[1]
[2]
[3]
[4]
[5]
[6]
[7]
[8]
[9]
[10]
[11]
[12]
[13]
[14]
[15]
[16]
[17]
[18]
[19]
[20]
[21]
[22]
[23]
[24]
Chapter 151:
Siku moja, watoza ushuru na wahalifu wengi walikwenda kumsikiliza Yesu.
2:
Mafarisayo na walimu wa Sheria wakaanza kunung`unika: "Mtazameni mtu huyu! Anawakaribisha wenye dhambi, na tena anakula nao."
3:
Yesu akawajibu kwa mfano:
4:
"Hivi, mtu akiwa na kondoo mia, akigundua kwamba mmoja wao amepotea, atafanya nini? Atawaacha wale tisini na tisa mbugani, na kwenda kumtafuta yule aliyepotea mpaka ampate.
5:
Akimpata, atambeba mabegani kwa furaha.
6:
Anapofika nyumbani, atawaita rafiki zake akiwaambia, `Furahini pamoja nami, kwa sababu nimempata yule kondoo wangu aliyepotea.`
7:
Kadhalika nawaambieni, ndivyo kutakavyokuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya kutubu kwa mwenye dhambi mmoja, kuliko kwa ajili ya watu tisini na tisa wanaojiona kuwa wema, wasiohitaji kutubu. ic
8:
"Au mwaonaje? Tuseme mwanamke fulani ana sarafu kumi za fedha, akipoteza moja, atafanya nini? Atawasha taa, aifagie nyumba na kuitafuta kwa uangalifu mpaka aipate.
9:
Akiipata, atawaita rafiki na jirani zake akisema, `Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata ile sarafu yangu iliyopotea.`
10:
Kadhalika nawaambieni, ndivyo watakavyofurahi malaika wa Mungu kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja anayetubu."
11:
Yesu akaendelea kusema, "Kulikuwa na mtu mmoja mwenye wana wawili.
12:
Yule mdogo, alimwambia baba yake: `Baba, nipe urithi wangu.` Naye akawagawia mali yake.
13:
Baada ya siku chache, yule mdogo aliuza urithi wake, akasafiri na fedha aliyopata, akaenda nchi ya mbali ambako aliitumia ovyo.
14:
Alipomaliza kutumia kila kitu, kukatokea njaa kali katika nchi ile, naye akaanza kuhangaika.
15:
Akaomba kazi kwa mwananchi mtu mmoja wa huko naye akampeleka shambani mwake kulisha nguruwe.
16:
Alitamani kula maganda waliyokula wale nguruwe, ila hakuna mtu aliyempa kitu.
17:
Alipoanza kupata akili akafikiri: `Mbona kuna wafanyakazi wengi wa baba yangu wanaokula na kusaza, nami ninakufa njaa?
18:
Nitarudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia.
19:
Sistahili hata kuitwa mwanao. Nifanye kama mmoja wa wafanyakazi wako.`
20:
Basi, akaanza safari ya kurudi kwa baba yake. Alipokuwa bado yu mbali, baba yake alimwona, na kwa moyo wa huruma alimkimbilia, akamkumbatia na kumbusu.
21:
"Mwanawe akamwambia: `Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao.`
22:
Lakini baba yake akawaambia watumishi wake: `Haraka! Leteni nguo nzuri mkamvike! Mvisheni pete na viatu!
23:
Mchinjeni ndama mnono; tule kusherehekea!
24:
Kwa sababu huyu mwanangu alikuwa amekufa, kumbe yu mzima alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.` Wakaanza kufanya sherehe.
25:
"Wakati huo kaka yake alikuwa bado shambani. Alipokuwa akirudi na kukaribia nyumbani akasikia vifijo na ngoma.
26:
Akamwita mmoja wa watumishi, akamwuliza: `Kuna nini?`
27:
Huyo mtumishi akamwambia: `Ndugu yako amerudi nyumbani, na baba yako amemchinjia ndama mnono kwa kuwa amempata akiwa salama salimini.`
28:
Huyo kijana mkubwa akawaka hasira hata akakataa kuingia nyumbani. Baba yake akatoka nje na kumsihi aingie.
29:
Lakini yeye akamjibu: `Kumbuka! Miaka yote nimekutumikia, sijavunja amri yako hata mara moja. Umenipa nini? Hujanipa hata mwana mbuzi mmoja nikafanye sherehe pamoja na rafiki zangu!
30:
Lakini mtoto wako huyu aliyekula mali yako pamoja na makahaba, mara tu alipokuja umemchinjia yule ndama mnono.`
31:
Baba yake akamjibu: `Mwanangu, wewe uko pamoja nami siku zote, na kila nilicho nacho ni chako.
32:
Ilitubidi kufanya sherehe na kufurahi, kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa, kumbe yu mzima; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana."`
|