[1]
[2]
[3]
[4]
[5]
[6]
[7]
[8]
[9]
[10]
[11]
[12]
[13]
[14]
[15]
[16]
[17]
[18]
[19]
[20]
[21]
[22]
[23]
[24]
Chapter 121:
Wakati watu kwa maelfu walipokuwa wamekusanyika hata wakawa wanakanyagana, Yesu aliwaambia kwanza wanafunzi wake, "Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani unafiki.
2:
Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, kila kilichofichika kitafichuliwa.
3:
Kwa hiyo, kila mliyosema gizani, watu watayasikia katika mwanga, na kila mliyonong`ona faraghani milango imefungwa, yatatangazwa juu ya nyumba.
4:
"Nawaambieni ninyi rafiki zangu: msiwaogope wale wanaoua mwili, wasiweze kufanya kitu kingine zaidi.
5:
Nitawaonyesheni yule ambaye ni lazima kumwogopa: mwogopeni yule ambaye baada ya kuua ana uwezo wa kumtupa mtu katika moto wa Jehanamu. Naam, ninawaambieni, mwogopeni huyo.
6:
Inajulikana kwamba shomoro watano huuzwa kwa senti kumi, au sivyo? Lakini mbele ya Mungu hasahauliki hata mmoja.
7:
Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope, basi, ninyi mna thamani zaidi kuliko shomoro wengi!
8:
"Nawaambieni kweli, kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, Mwana wa Mtu naye atakiri mbele ya malaika wa Mungu kwamba mtu huyo ni wake.
9:
Lakini, mtu yeyote anayenikana mbele ya watu, naye atakanwa mbele ya malaika wa Mungu.
10:
"Yeyote anayesema neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa; lakini anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.
11:
"Watakapowapeleka ninyi mbele ya masunagogi na mbele ya wakuu na watawala msiwe na wasiwasi juu ya jinsi mtakavyojitetea au jinsi mtakavyosema.
12:
Kwa maana wakati huo Roho Mtakatifu atawafundisheni kile mnachopaswa kusema."
13:
Mtu mmoja katika ule umati wa watu akamwambia, "Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane urithi aliotuachia baba."
14:
Yesu akamjibu, "Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi mwamuzi au msuluhishi kati yenu?"
15:
Basi, akawaambia wote, "Jihadharini na kila aina ya tamaa; maana uzima wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo."
16:
Kisha akawaambia mfano: "Kulikuwa na tajiri mmoja ambaye shamba lake lilizaa mavuno mengi.
17:
Tajiri huyo akafikiri moyoni mwake: `Nitafanyaje nami sina mahali pa kuhifadhia mavuno yangu?
18:
Nitafanya hivi: nitabomoa ghala zangu na kujenga kubwa zaidi, na humo nitahifadhi mavuno yangu yote na mali yangu.
19:
Hapo nitaweza kuiambia roho yangu: sasa unayo akiba ya matumizi kwa miaka na miaka. Ponda mali, ule, unywe na kufurahi.`
20:
Lakini Mungu akamwambia: `Mpumbavu wewe; leo usiku roho yako itachukuliwa. Na vitu vile vyote ulivyojilundikia vitakuwa vya nani?"`
21:
Yesu akamaliza kwa kusema "Ndivyo ilivyo kwa mtu anayejilundikia mali kwa ajili yake mwenyewe, lakini si tajiri mbele ya Mungu."
22:
Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kwa sababu hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu.
23:
Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni bora kuliko mavazi.
24:
Chukueni kwa mfano, kunguru: hawapandi, hawavuni wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Ninyi mna thamani zaidi kuliko ndege!
25:
Ni nani kati yenu kwa kuwa na wasiwasi anaweza kuongeza urefu wa maisha yake?
26:
Basi, kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini kuwa na wasiwasi juu ya yale mengine?
27:
Angalieni maua jinsi yanavyomea. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Hata hivyo, nawahakikishieni kwamba hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo.
28:
Lakini, kama Mungu hulivika vizuri jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, hatawafanyia ninyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba!
29:
"Basi, msivurugike akili, mkihangaika daima juu ya mtakachokula au mtakachokunywa.
30:
Kwa maana hayo yote ndiyo yanayohangaikiwa na watu wasiomjua Mungu. Baba yenu anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo.
31:
Shughulikieni kwanza Ufalme wa Mungu, na hayo yote mtapewa kwa ziada.
32:
"Msiogope, enyi kundi dogo! Maana Baba yenu amependa kuwapeni Ufalme.
33:
Uzeni mali yenu mkawape maskini misaada. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, na jiwekeeni hazina mbinguni ambako haitapungua. Huko wezi hawakaribii, wala nondo hawaharibu.
34:
Pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.
35:
"Muwe tayari! Jifungeni mkanda kiunoni, na taa zenu ziwe zinawaka;
36:
muwe kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka arusini, ili wamfungulie mara atakapobisha hodi.
37:
Heri yao watumishi wale ambao bwana wao atakaporudi atawakuta wanakesha! Nawaambieni hakika, huyo bwana atajifunga mkanda kiunoni, atawaketisha mezani na kuwahudumia.
38:
Heri yao watumishi hao ikiwa bwana wao atawakuta wanakesha hata ikiwa atarudi usiku wa manane au alfajiri.
39:
Jueni kwamba, kama mwenye nyumba angejua saa ambayo mwizi atakuja, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe.
40:
Nanyi, kadhalika muwe tayari, maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia."
41:
Petro akamwambia, "Bwana, mfano huo ni kwa ajili yetu tu, au ni kwa ajili ya watu wote?"
42:
Bwana akajibu, "Ni nani basi, mtumishi aliye mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watumishi wake ili awape chakula wakati ufaao?
43:
Heri yake mtumishi huyo ikiwa bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo.
44:
Hakika atampa madaraka juu ya mali yake yote.
45:
Lakini, kama mtumishi huyo atafikiri moyoni mwake: na kusema: `Bwana wangu amekawia sana kurudi` halafu aanze kuwapiga watumishi wenzake, wa kiume au wa kike, na kula, kunywa na kulewa,
46:
bwana wake atarudi siku asiyoitazamia na saa asiyoijua; atamkatilia mbali na kumweka fungu moja na wasioamini.*fb*
47:
Mtumishi ambaye anajua matakwa ya bwana wake lakini hajiweki tayari kufanya anavyotakiwa, atapigwa sana.
48:
Lakini yule afanyaye yanayostahili adhabu bila kujua, atapigwa kidogo. Aliyepewa vingi atatakiwa vingi; aliyekabidhiwa vingi zaidi atatakiwa kutoa vingi zaidi.
49:
"Nimekuja kuwasha moto duniani, laiti ungekuwa umewaka tayari!
50:
Ninao ubatizo ambao inanipasa niupokee; jinsi gani ninavyohangaika mpaka ukamilike!
51:
Mnadhani nimekuja kuleta amani duniani? Hata kidogo; si amani bali utengano.
52:
Na tangu sasa, jamaa ya watu watano itagawanyika; watatu dhidi ya wawili, na wawili dhidi ya watatu.
53:
Baba atakuwa dhidi ya mwanawe, mwana dhidi ya baba yake; mama dhidi ya bintiye, binti dhidi ya mama yake; mama mkwe dhidi ya mke wa mwanawe na huyo dhidi ya mama mkwe wake."
54:
Yesu akayaambia tena makundi ya watu, "Mnapoona mawingu yakitokea upande wa magharibi, mara mwasema: `Mvua itanyesha`, na kweli hunyesha.
55:
Mnapoona upepo wa kusi unavuma, mwasema `Kutakuwa na hali ya joto` na ndivyo inavyokuwa.
56:
Enyi wanafiki! Mnajua kutabiri hali ya hewa kwa kuangalia dunia na anga; kwa nini basi, hamwezi kujua maana ya nyakati hizi?
57:
"Na kwa nini hamwezi kujiamulia wenyewe jambo jema la kufanya?
58:
Maana kama mshtaki wako anakupeleka mahakamani, ingekuwa afadhali kwako kupatana naye mkiwa bado njiani, ili asije akakupeleka mbele ya hakimu, naye hakimu akakutoa kwa polisi, nao wakakutia ndani.
59:
Hakika hutatoka huko nakwambia, mpaka utakapomaliza kulipa senti ya mwisho."
|