[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24]

Chapter 4

1: Yesu alitoka katika mto Yordani akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akaongozwa na Roho mpaka jangwani. 2: Huko alijaribiwa na Ibilisi kwa muda wa siku arubaini. Wakati huo wote hakula chochote, na baada ya siku hizo akasikia njaa. 3: Ndipo Ibilisi akamwambia, "Kama wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate." 4: Yesu akamjibu, "Imeandikwa: `Mtu haishi kwa mkate tu."` 5: Kisha Ibilisi akamchukua hadi mahali pa juu, akamwonyesha kwa mara moja falme zote za ulimwengu. Huyo Shetani akamwambia, 6: "Nitakupa uwezo juu ya falme zote hizi na fahari zake, kwa maana nimepewa hivi vyote; nikitaka kumpa mtu ninaweza. 7: Hivi vyote vitakuwa mali yako wewe, kama ukiniabudu." 8: Yesu akamjibu, "Imeandikwa: `Utamwabudu Bwana Mungu wako, na utamtumikia yeye peke yake."` 9: Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, kwenye mnara wa Hekalu, akamwambia, "Kama wewe ni Mwana wa Mungu, 10: kwa maana imeandikwa: `Atawaamuru malaika wake wakulinde,` 11: na tena, `Watakuchukua mikononi mwao usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe."` 12: Lakini Yesu akamjibu, "Imeandikwa: `Usimjaribu Bwana Mungu wako."` 13: Ibilisi alipokwishamjaribu kwa kila njia, akamwacha kwa muda. 14: Yesu alirudi Galilaya akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, na habari zake zikaenea katika sehemu zote za jirani. 15: Naye akawa anawafundisha watu katika masunagogi yao, akasifiwa na wote. 16: Basi, Yesu alikwenda Nazareti, mahali alipolelewa, na siku ya Sabato, aliingia katika sunagogi, kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome Maandiko Matakatifu kwa sauti. 17: Akapokea kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na akakuta mahali palipoandikwa: 18: "Roho wa Bwana yu juu yangu, kwani amenipaka mafuta niwahubirie maskini Habari Njema. Amenituma niwatangazie mateka watapata uhuru, vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa, 19: na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana." 20: Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi, kisha akaketi; watu wote wakamkodolea macho. 21: Naye akaanza kuwaambia, "Andiko hili mlilosikia likisomwa, limetimia leo." 22: Wote wakavutiwa sana naye, wakastaajabia maneno mazuri aliyosema. Wakanena, "Je, huyu si mwana wa Yosefu?" 23: Naye akawaambia, "Bila shaka mtaniambia msemo huu: `Mganga jiponye mwenyewe`, na pia mtasema: `Yote tuliyosikia umeyafanya kule Kafarnaumu, yafanye hapa pia katika kijiji chako."` 24: Akaendelea kusema, "Hakika nawaambieni, nabii hatambuliwi katika kijiji chake. 25: Lakini, sikilizeni! Kweli kulikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli nyakati za Eliya. Wakati huo mvua iliacha kunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu; kukawa na njaa kubwa katika nchi yote. 26: Hata hivyo, Eliya hakutumwa kwa mjane yeyote ila kwa mwanamke mjane wa Sarepta, Sidoni. 27: Tena, katika nchi ya Israeli nyakati za Elisha kulikuwa na wenye ukoma wengi. Hata hivyo, hakuna yeyote aliyetakaswa ila tu Naamani, mwenyeji wa Siria." 28: Wote waliokuwa katika lile sunagogi waliposikia hayo walikasirika sana. 29: Wakasimama, wakamtoa nje ya mji wao uliokuwa umejengwa juu ya kilima, wakampeleka mpaka kwenye ukingo wa kilima hicho ili wamtupe chini. 30: Lakini Yesu akapita katikati yao, akaenda zake. 31: Kisha Yesu akashuka mpaka Kafarnaumu katika mkoa wa Galilaya, akawa anawafundisha watu siku ya Sabato. 32: Wakastaajabia uwezo aliokuwa nao katika kufundisha. 33: Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na roho ya pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio: 34: "We! Yesu wa Nazareti! Kwa nini unatuingilia? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni mjumbe Mtakatifu wa Mungu!" 35: Lakini Yesu akamkemea huyo pepo akisema: "Nyamaza! Mtoke mtu huyu!" Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo. 36: Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, "Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!" 37: Habari zake zikaenea mahali pote katika mkoa ule. 38: Yesu alitoka katika lile sunagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa na homa kali; wakamwomba amponye. 39: Yesu akaenda akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, nayo ikamwacha. Mara yule mama akainuka, akawatumikia. 40: Jua lilipokuwa linatua, wote waliokuwa na wagonjwa wao mbalimbali waliwaleta kwake; naye akaweka mikono yake juu ya kila mmoja wao, akawaponya wote. 41: Pepo waliwatoka watu wengi, wakapiga kelele wakisema: "Wewe u Mwana wa Mungu!" Lakini Yesu akawakemea, wala hakuwaruhusu kusema, maana walimfahamu kwamba yeye ndiye Kristo. 42: Kesho yake asubuhi Yesu aliondoka akaenda mahali pa faragha. Watu wakawa wanamtafuta, na walipofika mahali alipokuwa, wakajaribu kumzuia ili asiondoke kwao. 43: Lakini yeye akawaambia, "Ninapaswa kuhubiri Habari Njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, maana nilitumwa kwa ajili hiyo." 44: Akawa anahubiri katika masunagogi ya Yudea.