[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24]

Chapter 2

1: Siku zile, tangazo rasmi lilitolewa na Kaisari Augusto kuwataka watu wote chini ya utawala wake wajiandikishe. 2: Kuandikishwa huku kulikuwa mara ya kwanza, wakati Kirenio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Siria. 3: Basi, wote waliohusika walikwenda kujiandikisha, kila mtu katika mji wake. 4: Yosefu pia alifanya safari kutoka mjini Nazareti mkoani Galilaya. Kwa kuwa alikuwa wa jamaa na ukoo wa Daudi alikwenda mjini Bethlehemu mkoani Yuda alikozaliwa Mfalme Daudi. 5: Alikwenda kujiandikisha pamoja na mchumba wake Maria ambaye alikuwa mja mzito. 6: Walipokuwa huko, siku yake ya kujifungua ikawadia, 7: akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. 8: Katika sehemu hizo, walikuwako wachungaji wakikesha usiku mbugani kulinda mifugo yao. 9: Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote. Wakaogopa sana. 10: Malaika akawaambia, "Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kuu kwa watu wote. 11: Kwa maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye Kristo Bwana. 12: Na hiki kitakuwa kitambulisho kwenu: mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa horini." 13: Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema: 14: "Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na amani duniani kwa watu aliopendezwa nao!" 15: Baada ya hao malaika kuondoka na kurudi mbinguni, wachungaji wakaambiana: "Twendeni moja kwa moja mpaka Bethlehemu tukalione tukio hili Bwana alilotujulisha." 16: Basi, wakaenda mbio, wakamkuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga amelazwa horini. 17: Hao wachungaji walipomwona mtoto huyo wakawajulisha wote habari waliyokuwa wamesikia juu yake. 18: Wote waliosikia hayo walishangaa juu ya habari walizoambiwa na wachungaji. 19: Lakini Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake. 20: Wale wachungaji walirudi makwao huku wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa yote waliyokuwa wamesikia na kuona; yote yalikuwa kama walivyokuwa wameambiwa. 21: Siku nane baadaye, wakati wa kumtahiri mtoto ulipofika, walimpa jina Yesu, jina ambalo alikuwa amepewa na malaika kabla hajachukuliwa mimba. 22: Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na Sheria ya Mose, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele ya Bwana. 23: Katika Sheria ya Bwana imeandikwa: "Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa wakfu kwa Bwana." 24: Pia walikwenda ili watoe sadaka: hua wawili au makinda wawili ya njiwa, kama ilivyotakiwa katika Sheria ya Bwana. 25: Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye. 26: Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Masiha wa Bwana. 27: Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia Hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta Hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na Sheria, 28: Simeoni alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu na kusema: 29: "Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako, waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa amani. 30: Maana kwa macho yangu nimeuona wokovu utokao kwako, 31: ambao umeutayarisha mbele ya watu wote: 32: Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa, na utukufu kwa watu wako Israeli." 33: Baba na mama yake Yesu walikuwa wakistaajabia maneno aliyosema Simeoni juu ya mtoto. 34: Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, "Mtoto huyu atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli. Naye atakuwa ishara itakayopingwa na watu; 35: na hivyo mawazo ya watu wengi yataonekana wazi. Nawe mwenyewe, uchungu ulio kama upanga mkali utauchoma moyo wako." 36: Palikuwa na nabii mmoja mwanamke, mzee sana, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa ameishi na mumewe kwa miaka saba tangu alipoolewa. 37: Halafu alibaki mjane hadi wakati huo akiwa mzee wa miaka themanini na minne. Wakati huo wote alikaa Hekaluni akifunga na kusali usiku na mchana. 38: Saa hiyohiyo alijitokeza mbele, akamshukuru Mungu, na akaeleza habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wanatazamia ukombozi wa Yerusalemu. 39: Hao wazazi walipokwisha fanya yote yaliyoamriwa na Sheria ya Bwana, walirudi makwao Nazareti, mkoani Galilaya. 40: Mtoto akakua, akazidi kupata nguvu, akajaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa pamoja naye. 41: Wazazi wa Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka. 42: Mtoto alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, wote walikwenda kwenye sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. 43: Baada ya sikukuu, walianza safari ya kurudi makwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kuwa na habari. 44: Walidhani alikuwa pamoja na kundi la wasafiri, wakaenda mwendo wa kutwa, halafu wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na marafiki. 45: Kwa kuwa hawakumwona, walirudi Yerusalemu wakimtafuta. 46: Siku ya tatu walimkuta Hekaluni kati ya walimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47: Wote waliosikia maneno yake walistaajabia akili yake na majibu yake ya hekima. 48: Wazazi wake walipomwona walishangaa. Maria, mama yake, akamwuliza, "Mwanangu, kwa nini umetutenda hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa huzuni." 49: Yeye akawajibu, "Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua kwamba inanipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?" 50: Lakini wazazi wake hawakuelewa maana ya maneno aliyowaambia. 51: Basi, akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii. Mama yake akaweka mambo hayo yote moyoni mwake. 52: Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu.