[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24]

Chapter 1

1: Mheshimiwa Theofilo: Watu wengi wamejitahidi kuandika juu ya mambo yale yaliyotendeka kati yetu. 2: Waliandika kama tulivyoelezwa na wale walioyaona kwa macho yao tangu mwanzo, na waliotangaza ujumbe huo. 3: Inafaa nami pia, Mheshimiwa, baada ya kuchunguza kwa makini mambo yote tangu mwanzo, nikuandikie kwa mpango, 4: ili nawe uweze kujionea mwenyewe ukweli wa mambo yale uliyofundishwa. 5: Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha Abia. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni. 6: Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama. 7: Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana. 8: Siku moja, ilipokuwa zamu yake ya kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu, 9: Zakariya alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani. 10: Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani. 11: Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani. 12: Zakariya alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. 13: Lakini malaika akamwambia, "Zakariya, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane. 14: Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. 15: Atakuwa mkuu mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake. 16: Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao. 17: Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake." 18: Zakariya akamwambia huyo malaika, "Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu." 19: Malaika akamjibu, "Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu, na nimetumwa niseme nawe, nikuletee hii habari njema. 20: Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia." 21: Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakariya huku wakishangaa juu ya kukawia kwake Hekaluni. 22: Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono Hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu. 23: Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani. 24: Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema: 25: "Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu." 26: Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, 27: kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. 28: Malaika akamwendea, akamwambia, "Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe." 29: Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini? 30: Malaika akamwambia, "Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. 31: Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu. 32: Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. 33: Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho." 34: Maria akamjibu, "Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?" 35: Malaika akamjibu, "Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. 36: Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa. 37: Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu." 38: Maria akasema, "Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema." Kisha yule malaika akaenda zake. 39: Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yuda. 40: Huko, aliingia katika nyumba ya Zakariya, akamsalimu Elisabeti. 41: Mara tu Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifiu, 42: akasema kwa sauti kubwa, "Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa. 43: Mimi ni nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? 44: Nakwambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka kwa furaha. 45: Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokwambia." 46: Naye Maria akasema, 47: "Moyo wangu wamtukuza Bwana, roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu. 48: Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu. Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri. 49: Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu, jina lake ni takatifu. 50: Huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi. 51: Amefanya mambo makuu kwa mkono wake: amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao; 52: amewashusha wenye nguvu kutoka vitu vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu. 53: Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaacha waende mikono mitupu. 54: Amemsaidia Israeli mtumishi wake, akikumbuka huruma yake. 55: Kama alivyowaahidia wazee wetu Abrahamu na wazawa wake hata milele." 56: Maria alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani kwake. 57: Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume. 58: Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye. 59: Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakariya. 60: Lakini mama yake akasema, "La, sivyo, bali ataitwa Yohane." 61: Wakamwambia, "Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?" 62: Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani. 63: Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: "Yohane ndilo jina lake." Wote wakastaajabu. 64: Papo hapo midomo na ulimi wake Zakariya vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu. 65: Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea. 66: Wote waliosikia mambo hayo waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: "Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?" Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye. 67: Zakariya, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka ujumbe wa Mungu: 68: "Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli, kwani amekuja kuwasaidia na kuwakomboa watu wake. 69: Ametupatia Mwokozi shujaa, mzawa wa Daudi mtumishi wake. 70: Aliahidi hapo kale kwa njia ya manabii wake watakatifu, 71: kwamba atatuokoa mikononi mwa adui zetu na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia. 72: Alisema atawahurumia wazee wetu, na kukumbuka agano lake takatifu. 73: Kiapo alichomwapia Abrahamu baba yetu, ni kwamba atatujalia sisi 74: tukombolewe kutoka adui zetu, tupate kumtumikia bila hofu, 75: kwa unyofu na uadilifu mbele yake, siku zote za maisha yetu. 76: Nawe mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu, utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake; 77: kuwatangazia watu kwamba wataokolewa kwa kuondolewa dhambi zao. 78: Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma. Atasababisha pambazuko angavu la ukombozi litujie kutoka juu, 79: na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo, aongoze hatua zetu katika njia ya amani." 80: Mtoto akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionyesha rasmi kwa watu wa Israeli.