[1]
[2]
[3]
[4]
[5]
[6]
[7]
[8]
[9]
[10]
[11]
[12]
[13]
[14]
[15]
[16]
[17]
[18]
[19]
[20]
[21]
Chapter 211:
Baada ya hayo Yesu aliwatokea tena wanafunzi wake kando ya ziwa Tiberia. Aliwatokea hivi:
2:
Simoni Petro, Thoma (aitwaye Pacha), na Nathanieli mwenyeji wa Kana Galilaya, wana wawili wa Zebedayo na wanafunzi wake wengine wawili, walikuwa wote pamoja.
3:
Simoni Petro aliwaambia, "Nakwenda kuvua samaki." Nao wakamwambia, "Nasi tutafuatana nawe." Basi, wakaenda, wakapanda mashua, lakini usiku huo hawakupata chochote.
4:
Kulipoanza kupambazuka, Yesu alisimama kando ya ziwa, lakini wanafunzi hawakujua kwamba alikuwa yeye.
5:
Basi, Yesu akawauliza, "Vijana, hamjapata samaki wowote sio?" Wao wakamjibu, "La! Hatujapata kitu."
6:
Yesu akawaambia, "Tupeni wavu upande wa kulia wa mashua nanyi mtapata samaki." Basi, wakatupa wavu lakini sasa hawakuweza kuuvuta tena kwa wingi wa samaki.
7:
Hapo yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, "Ni Bwana!" Simoni Petro aliposikia ya kuwa ni Bwana, akajifunga vazi lake (maana hakuwa amelivaa), akarukia majini.
8:
Lakini wale wanafunzi wengine walikuja pwani kwa mashua huku wanauvuta wavu uliojaa samaki; hawakuwa mbali na nchi kavu, ila walikuwa yapata mita mia moja kutoka ukingoni.
9:
Walipofika nchi kavu waliona moto wa makaa umewashwa na juu yake pamewekwa samaki na mkate.
10:
Yesu akawaambia, "Leteni hapa baadhi ya samaki mliovua."
11:
Basi, Simoni Petro akapanda mashuani, akavuta hadi nchi kavu ule wavu uliokuwa umejaa samaki wakubwa mia moja na hamsini na watatu. Na ingawa walikuwa wengi hivyo wavu haukukatika.
12:
Yesu akawaambia, "Njoni mkafungue kinywa." Hakuna hata mmoja wao aliyethubutu kumwuliza: "Wewe ni nani?" Maana walijua alikuwa Bwana.
13:
Yesu akaja, akatwaa mkate akawapa; akafanya vivyo hivyo na wale samaki.
14:
Hii ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka kutoka wafu.
15:
Walipokwisha kula, Yesu alimwuliza Simoni Petro, "Simoni, mwana wa Yohane! Je, wanipenda mimi zaidi kuliko hawa?" Naye akajibu, "Naam, Bwana; wajua kwamba mimi nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza wana kondoo wangu."
16:
Kisha akamwambia mara ya pili, "Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?" Petro akamjibu, "Naam, Bwana; wajua kwamba nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza kondoo wangu."
17:
Akamwuliza mara ya tatu, "Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?" Hapo Petro akahuzunika kwa sababu alimwuliza mara ya tatu: "Wanipenda?" akamwambia, "Bwana, wewe wajua yote; wewe wajua kwamba mimi nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza kondoo wangu!
18:
Kweli nakwambia, ulipokuwa kijana ulizoea kujifunga mshipi na kwenda kokote ulikotaka. Lakini utakapokuwa mzee utanyosha mikono yako, na mtu mwingine atakufunga na kukupeleka usikopenda kwenda."
19:
(Kwa kusema hivyo, alionyesha jinsi Petro atakavyokufa na kumtukuza Mungu.) Kisha akamwambia, "Nifuate."
20:
Hapo Petro akageuka, akamwona yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda, anafuata (Huyu mwanafunzi ndiye yule ambaye wakati wa chakula cha jioni, alikaa karibu sana na Yesu na kumwuliza: "Bwana ni nani atakayekusaliti?")
21:
Basi, Petro alipomwona huyo akamwuliza Yesu, "Bwana, na huyu je?"
22:
Yesu akamjibu, "Kama nataka abaki mpaka nitakapokuja, yakuhusu nini? Wewe nifuate mimi."
23:
Basi, habari hiyo ikaenea miongoni mwa wale ndugu kwamba mwanafunzi huyo hafi. Lakini Yesu hakumwambia kwamba mwanafunzi huyo hafi, ila, "Kama nataka abaki mpaka nitakapokuja, yakuhusu nini?"
24:
Huyo ndiye yule aliyeshuhudia mambo haya na kuyaandika. Nasi twajua kwamba aliyoyasema ni kweli.
25:
Kuna mambo mengine mengi aliyofanya Yesu, ambayo kama yangeandikwa yote, moja baada ya lingine, nadhani hata ulimwengu wenyewe usingetosha kuviweka vitabu ambavyo vingeandikwa.
|