[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21]

Chapter 16

1: "Nimewaambieni hayo kusudi msiiache imani yenu. 2: Watu watawatenga ninyi na masunagogi yao. Tena, wakati unakuja ambapo kila atakayewaua ninyi atadhani anamhudumia Mungu. 3: Watawatendeeni mambo hayo kwa sababu hawamjui Baba, wala hawanijui mimi. 4: Basi, nimewaambieni mambo haya ili saa yake itakapofika mkumbuke kwamba niliwaambieni. "Sikuwaambieni mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi. 5: Lakini sasa namwendea yule aliyenituma; na hakuna hata mmoja wenu anayeniuliza: `Unakwenda wapi?` 6: Kwa kuwa nimewaambieni mambo hayo mmejaa huzuni mioyoni mwenu. 7: Lakini, nawaambieni ukweli: afadhali kwenu mimi niende zangu, maana nisipokwenda Msaidizi hatakuja kwenu. Lakini nikienda, basi, nitamtuma kwenu. 8: Naye atakapokuja atawathibitishia walimwengu kwamba wamekosea kuhusu dhambi, uadilifu na hukumu ya Mungu. 9: Wamekosea kuhusu dhambi kwa sababu hawaniamini; 10: kuhusu uadilifu, kwa sababu naenda zangu kwa Baba, nanyi hamtaniona tena; 11: kuhusu hukumu kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu amekwisha hukumiwa. 12: "Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili. 13: Lakini atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza kwenye ukweli wote; maana hatasema kwa mamlaka yake mwenyewe, bali atawaambieni yote atakayosikia, na atasema mambo yatakayokuwa yanakuja. 14: Yeye atanitukuza mimi kwa kuwa atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu. 15: Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu; ndiyo maana nimesema kwamba huyo Roho Mtakatifu atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu. 16: "Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona!" 17: Hapo baadhi ya wanafunzi wake wakaulizana, "Ana maana gani anapotwambia: `Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?` Tena anasema: `Kwa kuwa ninakwenda kwa Baba!"` 18: Basi, wakawa wanaulizana, "Ana maana gani anaposema: `Bado kitambo kidogo?` Hatuelewi anaongelea nini." 19: Yesu alijua kwamba walitaka kumwuliza, basi akawaambia, "Je, mnaulizana juu ya yale niliyosema: `Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?` 20: Nawaambieni kweli, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi: mtaona huzuni lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. 21: Wakati mama anapojifungua huona huzuni kwa sababu saa ya maumivu imefika; lakini akisha jifungua hayakumbuki tena maumivu hayo kwa sababu ya furaha kwamba mtu amezaliwa duniani. 22: Ninyi pia mna huzuni sasa; lakini nitawajieni tena, nanyi mtajaa furaha mioyoni mwenu, na furaha hiyo hakuna mtu atakayeiondoa kwenu. 23: Siku hiyo hamtaniomba chochote. Kweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba Baba kwa jina langu, atawapeni. 24: Mpaka sasa hamjaomba chochote kwa jina langu. Ombeni nanyi mtapata ili furaha yenu ikamilike. 25: "Nimewaambieni mambo hayo kwa mafumbo. Lakini wakati utakuja ambapo sitasema tena nanyi kwa mafumbo, bali nitawaambieni waziwazi juu ya Baba. 26: Siku hiyo mtaomba kwa jina langu, na siwaambii kwamba nitamwomba Baba kwa niaba yenu; 27: maana yeye mwenyewe anawapenda ninyi, kwa sababu ninyi mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu. 28: Mimi nilitoka kwa Baba, nikaja ulimwenguni; na sasa nauacha ulimwengu na kurudi kwa Baba." 29: Basi, wanafunzi wake wakamwambia, "Ahaa! Sasa unasema waziwazi kabisa bila kutumia mafumbo. 30: Sasa tunajua kwamba wewe unajua kila kitu, na huna haja ya kuulizwa maswali na mtu yeyote; kwa hiyo tunaamini kwamba umetoka kwa Mungu." 31: Yesu akawajibu, "Je, mnaamini sasa? 32: Wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo ninyi nyote mtatawanyika kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Kumbe, lakini mimi siko peke yangu, maana Baba yu pamoja nami. 33: Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!"