[1]
[2]
[3]
[4]
[5]
[6]
[7]
[8]
[9]
[10]
[11]
[12]
[13]
[14]
[15]
[16]
[17]
[18]
[19]
[20]
[21]
Chapter 141:
Yesu aliwaambia, "Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia.
2:
Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; la sivyo ningalikwisha waambieni. Sasa nakwenda kuwatayarishieni nafasi.
3:
Na nikienda na kuwatayarishieni nafasi, nitarudi na kuwachukueni kwangu, ili nanyi muwe pale nilipo mimi.
4:
Mnajua njia ya kwenda huko ninakokwenda."
5:
Thoma akamwuliza, "Bwana, hatujui unakokwenda, tutawezaje basi, kuijua hiyo njia?"
6:
Yesu akamjibu, "Mimi ni njia, na ukweli na uzima. Hakuna awezaye kwenda kwa Baba ila kwa kupitia kwangu.
7:
Ikiwa mnanijua mimi mnamjua na Baba yangu pia. Na tangu sasa, mnamjua, tena mmekwisha mwona."
8:
Filipo akamwambia, "Bwana, tuonyeshe Baba, nasi tutatosheka."
9:
Yesu akamwambia, "Filipo, nimekaa nanyi muda wote huu, nawe hujanijua? Aliyekwisha niona mimi amemwona Baba. Unawezaje basi, kusema: `Tuonyeshe Baba?`
10:
Je, huamini kwamba mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambieni nyote siyasemi kwa mamlaka yangu; Baba aliye ndani yangu anafanya kazi yake.
11:
Mnapaswa kuniamini ninaposema kwamba mimi niko ndani ya Baba naye Baba yuko ndani yangu. Ama sivyo, aminini kwa sababu ya mambo ninayofanya.
12:
Kweli nawaambieni, anayeniamini atafanya mambo ninayofanya mimi; naam, atafanya hata makuu zaidi, maana nakwenda kwa Baba.
13:
Na chochote mtakachoomba kwa jina langu nitafanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.
14:
Mkiniomba chochote kwa jina langu, nitawafanyieni.
15:
"Mkinipenda mtazishika amri zangu.
16:
Nami nitamwomba Baba naye atawapeni Msaidizi mwingine, atakayekaa nanyi milele.
17:
Yeye ni Roho wa kweli. Ulimwengu hauwezi kumpokea kwa sababu hauwezi kumwona wala kumjua. Lakini ninyi mnamjua kwa sababu anabaki nanyi na yu ndani yenu.
18:
"Sitawaacha ninyi yatima; nitakuja tena kwenu.
19:
Bado kidogo nao ulimwengu hautaniona tena, lakini ninyi mtaniona; na kwa kuwa mimi ni hai, nanyi pia mtakuwa hai.
20:
Siku ile itakapofika mtajua kwamba mimi niko ndani ya Baba, nanyi mko ndani yangu, nami ndani yenu.
21:
Azipokeaye amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake."
22:
Yuda (si yule Iskarioti) akamwambia, "Bwana, itawezekanaje wewe kujidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?"
23:
Yesu akamjibu, "Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kukaa naye.
24:
Asiyenipenda hashiki maneno yangu. Na neno mlilosikia si langu, bali ni lake Baba aliyenituma.
25:
"Nimewaambieni mambo haya nikiwa bado pamoja nanyi
26:
lakini Msaidizi, Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisheni kila kitu na kuwakumbusheni yote niliyowaambieni.
27:
"Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi ninyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike.
28:
Mlikwisha sikia nikiwaambieni: `Ninakwenda zangu, kisha nitarudi tena kwenu.` Kama mngalinipenda mngalifurahi kwa sababu ninakwenda kwa Baba, maana yeye ni mkuu kuliko mimi.
29:
Nimewaambieni haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini.
30:
Sitasema nanyi tena mambo mengi, maana mtawala wa ulimwengu huu anakuja. Kwangu mimi hawezi kitu;
31:
lakini ulimwengu unapaswa kujua kwamba nampenda Baba, na ndiyo maana nafanya kila kitu kama Baba alivyoniamuru. Simameni, tutoke hapa!"
|