[1]
[2]
[3]
[4]
[5]
[6]
[7]
[8]
[9]
[10]
[11]
[12]
[13]
[14]
[15]
[16]
[17]
[18]
[19]
[20]
[21]
Chapter 101:
Yesu alisema "Kweli nawaambieni, yeyote yule asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia mlangoni, bali hupenya na kuingia kwa njia nyingine, huyo ni mwizi na mnyang`anyi.
2:
Lakini anayeingia kwa kupitia mlangoni, huyo ndiye mchungaji wa kondoo.
3:
Mngoja mlango wa zizi humfungulia, na kondoo husikia sauti yake, naye huwaita kondoo wake kila mmoja kwa jina lake na kuwaongoza nje.
4:
Akisha watoa nje huwatangulia mbele nao kondoo humfuata, kwani wanaijua sauti yake.
5:
Kondoo hao hawawezi kumfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti yake."
6:
Yesu aliwaambia mfano huo, lakini wao hawakuelewa alichotaka kuwaambia.
7:
Basi, akasema tena, "Kweli nawaambieni, mimi ni mlango wa kondoo.
8:
Wale wengine wote waliokuja kabla yangu ni wezi na wanyang`anyi, nao kondoo hawakuwasikiliza.
9:
Mimi ni mlango. Anayeingia kwa kupitia kwangu ataokolewa; ataingia na kutoka, na kupata malisho.
10:
Mwizi huja kwa shabaha ya kuiba, kuua na kuharibu. Mimi nimekuja mpate kuwa na uzima--uzima kamili.
11:
"Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake.
12:
Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, anapoona mbwa mwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia. Kisha mbwa mwitu huwakamata na kuwatawanya.
13:
Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa mshahara tu.
14:
Mimi ni mchungaji mwema. Nawajua walio wangu, nao walio wangu wananijua mimi,
15:
kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Mimi nayatoa maisha yangu kwa ajili yao.
16:
Tena ninao kondoo wengine ambao hawamo zizini humu. Inanibidi kuwaleta hao pia, nao wataisikia sauti yangu, na kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.
17:
"Baba ananipenda kwani nautoa uhai wangu ili nipate kuupokea tena.
18:
Hakuna mtu anayeninyang`anya uhai wangu; mimi na nautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa na uwezo wa kuuchukua tena. Hivi ndivyo Baba alivyoniamuru nifanye."
19:
Kukawa tena na mafarakano kati ya Wayahudi kwa sababu ya maneno haya.
20:
Wengi wao wakasema, "Ana pepo; tena ni mwendawazimu! Ya nini kumsikiliza?"
21:
Wengine wakasema, "Haya si maneno ya mwenye pepo. Je, pepo anaweza kuyafumbua macho ya vipofu?"
22:
Huko Yerusalemu kulikuwa na sikukuu ya Kutabaruku. Wakati huo ulikuwa wa baridi.
23:
Naye Yesu akawa anatembea Hekaluni katika ukumbi wa Solomoni.
24:
Basi, Wayahudi wakamzunguka, wakamwuliza, "Utatuacha katika mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo, basi, tuambie wazi."
25:
Yesu akawajibu, "Nimewaambieni, lakini hamsadiki. Kazi ninazozifanya mimi kwa jina la Baba yangu zinanishuhudia.
26:
Lakini ninyi hamsadiki kwa sababu ninyi si kondoo wangu.
27:
Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao hunifuata.
28:
Mimi nawapa uzima wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu.
29:
Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wale hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba.
30:
Mimi na Baba, tu mmoja."
31:
Basi, Wayahudi wakachukua mawe ili wamtupie.
32:
Yesu akawaambia, "Nimewaonyesheni kazi nyingi kutoka kwa Baba. Ni ipi kati ya hizo inayowafanya mnipige mawe?"
33:
Wayahudi wakamjibu, "Hatukupigi mawe kwa ajili ya tendo jema, ila kwa sababu ya kukufuru! Maana wajifanya kuwa Mungu hali wewe ni binadamu tu."
34:
Yesu akawajibu, "Je, haikuandikwa katika Sheria yenu: `Mimi nimesema, ninyi ni miungu?`
35:
Mungu aliwaita miungu wale waliopewa neno lake; nasi twajua kwamba Maandiko Matakatifu yasema ukweli daima.
36:
Je, yeye ambaye Baba alimweka wakfu na kumtuma ulimwenguni, mnamwambia: `Unakufuru`, eti kwa sababu nilisema: `Mimi ni Mwana wa Mungu?`
37:
Kama sifanyi kazi za Baba yangu msiniamini.
38:
Lakini ikiwa ninazifanya, hata kama hamniamini, walau ziaminini hizo kazi mpate kujua na kutambua kwamba Baba yuko ndani yangu, nami niko ndani yake."
39:
Wakajaribu tena kumkamata lakini akachopoka mikononi mwao.
40:
Yesu akaenda tena ng`ambo ya mto Yordani, mahali Yohane alipokuwa akibatiza, akakaa huko.
41:
Watu wengi walimwendea wakasema, "Yohane hakufanya ishara yoyote. Lakini yale yote Yohane aliyosema juu ya mtu huyu ni kweli kabisa."
42:
Watu wengi mahali hapo wakamwamini.
|