[1]
[2]
[3]
[4]
[5]
[6]
[7]
[8]
[9]
[10]
[11]
[12]
[13]
[14]
[15]
[16]
[17]
[18]
[19]
[20]
[21]
Chapter 81:
lakini Yesu akaenda kwenye mlima wa Mizeituni.
2:
Kesho yake asubuhi na mapema alikwenda tena Hekaluni. Watu wote wakamwendea, naye akaketi akawa anawafundisha.
3:
Basi, walimu wa Sheria na Mafarisayo wakamletea mwanamke mmoja aliyefumaniwa katika uzinzi. Wakamsimamisha katikati yao.
4:
Kisha wakamwuliza Yesu, "Mwalimu! Mwanamke huyu alifumaniwa katika uzinzi.
5:
Katika Sheria yetu Mose alituamuru mwanamke kama huyu apigwe mawe. Basi, wewe wasemaje?"
6:
Walisema hivyo kumjaribu, wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akainama chini, akaandika ardhini kwa kidole.
7:
Walipozidi kumwuliza, Yesu akainuka, akawaambia, "Mtu asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe."
8:
Kisha akainama tena, akawa anaandika ardhini.
9:
Waliposikia hivyo, wakaanza kutoweka mmojammoja, wakitanguliwa na wazee. Yesu akabaki peke yake, na yule mwanamke amesimama palepale.
10:
Yesu alipoinuka akamwuliza huyo mwanamke, "Wako wapi wale watu? Je, hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?"
11:
Huyo mwanamke akamjibu, "Mheshimiwa, hakuna hata mmoja!" Naye Yesu akamwambia, "Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; na tangu sasa usitende dhambi tena."*fb* mahali pengine.
12:
Yesu alipozungumza nao tena, aliwaambia, "Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu. Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uzima."
13:
Basi, Mafarisayo wakamwambia, "Wewe unajishuhudia mwenyewe; kwa hiyo ushahidi wako si halali."
14:
Yesu akawajibu, "Hata kama ninajishuhudia mwenyewe, ushahidi wangu ni wa kweli kwa sababu mimi najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda.
15:
Ninyi mnahukumu kwa fikira za kibinadamu, lakini mimi simhukumu mtu.
16:
Hata nikihukumu, hukumu yangu ni ya haki kwa sababu mimi siko peke yangu; Baba aliyenituma yuko pamoja nami.
17:
Imeandikwa katika Sheria yenu ya kwamba ushahidi wa watu wawili ni halali.
18:
Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma, ananishuhudia pia."
19:
Hapo wakamwuliza, "Baba yako yuko wapi?" Yesu akawajibu "Ninyi hamnijui mimi wala hamumjui Baba. Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba yangu pia."
20:
Yesu alisema maneno hayo kwenye chumba cha hazina alipokuwa anafundisha Hekaluni. Wala hakuna mtu aliyemtia nguvuni, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.
21:
Yesu akawaambia tena, "Naenda zangu nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi,ninyi hamwezi kufika."
22:
Basi, viongozi wa Wayahudi wakasema, "Je, atajiua? Mbona anasema: `Niendako ninyi hamwezi kufika?"`
23:
Yesu akawaambia, "Ninyi mmetoka papa hapa chini, mimi nimetoka juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.
24:
Ndiyo maana niliwaambieni mtakufa katika dhambi zenu. Kama msipoamini kwamba `Mimi ndimi`, mtakufa katika dhambi zenu."
25:
Nao wakamwuliza, "Wewe ni nani?" Yesu akawajibu, "Nimewaambieni tangu mwanzo!
26:
Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu. Lakini yule aliyenituma ni kweli; nami nauambia ulimwengu mambo yale tu niliyoyasikia kutoka kwake."
27:
Hawakuelewa kwamba Yesu alikuwa akisema nao juu ya Baba.
28:
Basi, Yesu akawaambia, "Mtakapokwisha mwinua Mwana wa Mtu hapo ndipo mtakapojua kwamba `Mimi ndimi`, na kwamba sifanyi chochote mimi mwenyewe, ila nasema tu yale Baba aliyonifundisha.
29:
Yule aliyenituma yuko pamoja nami; yeye hakuniacha peke yangu kwani nafanya daima yale yanayompendeza."
30:
Baada ya kusema hayo watu wengi walimwamini.
31:
Basi, Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, "Kama mkiyazingatia mafundisho yangu mtakuwa kweli wanafunzi wangu.
32:
Mtaujua ukweli, nao ukweli utawapeni uhuru."
33:
Nao wakamjibu, "Sisi ni wazawa wa Abrahamu, na hatujapata kamwe kuwa watumwa wa mtu yeyote yule. Una maana gani unaposema: `mtakuwa huru?"`
34:
Yesu akawajibu, "Kweli nawaambieni, kila mtu anayetenda dhambi ni mtumwa wa dhambi.
35:
Mtumwa hana makao ya kudumu nyumbani, lakini mwana anayo makao ya kudumu.
36:
Kama mwana akiwapeni uhuru mtakuwa huru kweli.
37:
Najua kwamba ninyi ni wazawa wa Abrahamu. Hata hivyo, mnataka kuniua kwa sababu hamuyakubali mafundisho yangu.
38:
Mimi nasema yale aliyonionyesha Baba, lakini ninyi mwafanya yale aliyowaambieni baba yenu."
39:
Wao wakamjibu, "Baba yetu ni Abrahamu!" Yesu akawaambia, "Kama ninyi mngekuwa watoto wa Abrahamu, mngefanya kama alivyofanya Abrahamu,
40:
Mimi nimewaambieni ukweli niliousikia kwa Mungu; hata hivyo, ninyi mwataka kuniua. Abrahamu hakufanya hivyo!
41:
Ninyi mnafanya mambo yaleyale aliyofanya babu yenu." Wao wakamwambia, "Sisi si watoto haramu! Tunaye baba mmoja tu, yaani Mungu."
42:
Yesu akawaambia, "Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi, maana mimi nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila yeye alinituma.
43:
Kwa nini hamwelewi hayo ninayosema? Ni kwa kuwa hamwezi kuusikiliza ujumbe wangu.
44:
Ninyi ni watoto wa baba yenu Ibilisi na mnataka tu kutekeleza tamaa za baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; hana msimamo katika ukweli, kwani ukweli haumo ndani yake. Kila asemapo uongo, husema kutokana na hali yake ya maumbile, maana yeye ni mwongo na baba wa uongo.
45:
Mimi nasema ukweli, na ndiyo maana ninyi hamniamini.
46:
Nani kati yenu awezaye kuthibitisha kuwa mimi nina dhambi? Ikiwa basi nasema ukweli, kwa nini hamniamini?
47:
Aliye wa Mungu husikiliza maneno ya Mungu. Lakini ninyi hamsikilizi kwa sababu ninyi si (watu wa) Mungu."
48:
Wayahudi wakamwambia, "Je, hatukusema kweli kwamba wewe ni Msamaria, na tena una pepo?"
49:
Yesu akajibu, "Mimi sina pepo; mimi namheshimu Baba yangu, lakini ninyi hamniheshimu.
50:
Mimi sijitafutii utukufu wangu mwenyewe; yuko mmoja mwenye kuutafuta utukufu huo, naye ni hakimu.
51:
Kweli nawaambieni, anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele."
52:
Basi, Wayahudi wakasema, "Sasa tunajua kweli kwamba wewe ni mwendawazimu! Abrahamu alikufa, na manabii pia walikufa, nawe wasema ati, `Anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele!`
53:
Je, unajifanya mkuu zaidi kuliko baba yetu Abrahamu ambaye alikufa? Hata na manabii walikufa. Wewe unajifanya kuwa nani?"
54:
Yesu akawajibu, "Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu. Baba yangu ambaye ninyi mwasema ni Baba yenu, ndiye anayenitukuza.
55:
Ninyi hamjapata kumjua, lakini mimi namjua. Na, nikisema simjui, nitakuwa mwongo kama ninyi. Mimi namjua na ninashika neno lake.
56:
Abrahamu, baba yenu, alishangilia aione siku yangu; naye aliiona, akafurahi."
57:
Basi, Wayahudi wakamwambia, "Wewe hujatimiza miaka hamsini bado, nawe umemwona Abrahamu?"
58:
Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, kabla Abrahamu hajazaliwa, mimi niko."
59:
Hapo wakaokota mawe ili wamtupie, lakini Yesu akajificha, akatoka Hekaluni.
|