[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21]

Chapter 4

1: Mafarisayo walisikia kwamba Yesu alikuwa anabatiza na kuwapata wanafunzi wengi kuliko Yohane. 2: Lakini ukweli ni kwamba Yesu hakuwa anabatiza ila wanafunzi wake.) 3: Basi, Yesu aliposikia hayo, alitoka Yudea akarudi Galilaya; 4: na katika safari hiyo ilimbidi apitie Samaria. 5: Basi, akafika Sukari, mji mmoja wa Samaria, karibu na shamba ambalo Yakobo alikuwa amempa mwanawe, Yosefu. 6: Mahali hapo palikuwa na kisima cha Yakobo, naye Yesu, kutokana na uchovu wa safari, akaketi kando ya kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana. 7: Basi, mwanamke mmoja Msamaria akafika kuteka maji. Yesu akamwambia, "Nipatie maji ninywe." 8: (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.) 9: Lakini huyo mwanamke akamwambia, "Wewe ni Myahudi; mimi ni mwanamke Msamaria! Unawezaje kuniomba maji?" (Wayahudi hawakuwa na ushirikiano na Wasamaria katika matumizi ya vitu.) 10: Yesu akamjibu, "Kama tu ungalijua zawadi ya Mungu na ni nani anayekwambia: `Nipatie maji ninywe,` ungalikwisha mwomba, naye angekupa maji yaliyo hai." 11: Huyo mama akasema, "Mheshimiwa, wewe huna chombo cha kutekea maji, nacho kisima ni kirefu; utapata wapi maji yaliyo hai? 12: Au, labda wewe wajifanya mkuu kuliko babu yetu Yakobo? Yeye alitupa sisi kisima hiki; na yeye mwenyewe, watoto wake na mifugo yake walikunywa maji ya kisima hiki." 13: Yesu akamjibu, "Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena. 14: Lakini atakayekunywa maji nitakayompa mimi, hataona kiu milele. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji ya uzima na kumpatia uzima wa milele." 15: Huyo mwanamke akamwambia, "Mheshimiwa, nipe maji hayo ili nisione kiu tena; nisije tena mpaka hapa kuteka maji." 16: Yesu akamwambia, "Nenda ukamwite mumeo uje naye hapa." 17: Huyo mwanamke akamwambia, "Mimi sina mume." Yesu akamwambia, "Umesema kweli, kwamba huna mume. 18: Maana umekuwa na waume watano, na huyo unayeishi naye sasa si mume wako. Hapo umesema kweli." 19: Huyo Mwanamke akamwambia, "Mheshimiwa, naona ya kuwa wewe u nabii. 20: Babu zetu waliabudu juu ya mlima huu, lakini ninyi mwasema kwamba mahali pa kumwabudu Mungu ni kule Yerusalemu." 21: Yesu akamwambia, "Niamini; wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba juu ya mlima huu, wala kule Yerusalemu. 22: Ninyi Wasamaria mnamwabudu yule msiyemjua, lakini sisi tunamjua huyo tunayemwabudu, kwa maana wokovu unatoka kwa Wayahudi. 23: Lakini wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wanaoabudu kweli, watamwabudu Baba kwa nguvu ya Roho; watu wanaomwabudu hivyo ndio Baba anaotaka. 24: Mungu ni Roho, na watu wataweza tu kumwabudu kweli kwa nguvu ya Roho wake." 25: Huyo mama akamwambia, "Najua kwamba Masiha, aitwaye Kristo, anakuja. Atakapokuja atatujulisha kila kitu." 26: Yesu akamwambia, "Mimi ninayesema nawe, ndiye." 27: Hapo wanafunzi wake wakarudi, wakastaajabu sana kuona anaongea na mwanamke. Lakini hakuna mtu aliyesema: "Unataka nini?" au, "Kwa nini unaongea na mwanamke?" 28: Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda mjini na kuwaambia watu, 29: "Njoni mkamwone mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda! Je, yawezekana kuwa yeye ndiye Kristo?" 30: Watu wakatoka mjini, wakamwendea Yesu. 31: Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu: "Mwalimu, ule chakula." 32: Lakini Yesu akawaambia, "Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi." 33: Wanafunzi wake wakaulizana, "Je, kuna mtu aliyemletea chakula?" 34: Yesu akawaambia, "Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake. 35: Ninyi mwasema: `Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno utafika!` Lakini mimi nawaambieni, yatazameni mashamba; mazao yako tayari kuvunwa. 36: Mvunaji anapata mshahara wake, na anakusanya mavuno kwa ajili ya uzima wa milele; hivyo mpandaji na mvunaji watafurahi pamoja. 37: Kwa sababu hiyo msemo huu ni kweli: `Mmoja hupanda na mwingine huvuna.` 38: Mimi nimewatuma mkavune mavuno ambayo hamkuyatolea jasho, wengine walifanya kazi, lakini ninyi mnafaidika kutokana na jasho lao." 39: Wasamaria wengi wa kijiji kile waliamini kwa sababu ya maneno aliyosema huyo mama: "Ameniambia mambo yote niliyofanya." 40: Wasamaria walimwendea Yesu wakamwomba akae nao; naye akakaa hapo siku mbili. 41: Watu wengi zaidi walimwamini kwa sababu ya ujumbe wake. 42: Wakamwambia yule mama, "Sisi hatuamini tu kwa sababu ya maneno yako; sisi wenyewe tumesikia, na tunajua kwamba huyu ndiye kweli Mwokozi wa ulimwengu." 43: Baada ya siku mbili Yesu aliondoka hapo, akaenda Galilaya. 44: Maana Yesu mwenyewe alisema waziwazi kwamba, "Nabii hapati heshima katika nchi yake." 45: Basi, alipofika Galilaya, Wagalilaya wengi walimkaribisha. Maana nao pia walikuwa kwenye sikukuu ya Pasaka, wakayaona mambo yote Yesu aliyotenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu hiyo. 46: Yesu alifika tena huko mjini Kana, mkoani Galilaya, mahali alipogeuza maji kuwa divai. Kulikuwa na ofisa mmoja aliyekuwa na mtoto mgonjwa huko Kafarnaumu. 47: Basi, huyo ofisa aliposikia kuwa Yesu alikuwa ametoka Yudea na kufika Galilaya, alimwendea akamwomba aende kumponya mtoto wake aliyekuwa mgonjwa mahututi. 48: Yesu akamwambia, "Msipoona ishara na maajabu hamtaamini!" 49: Huyo ofisa akamwambia, "Mheshimiwa, tafadhali twende kabla mwanangu hajafa." 50: Yesu akamwambia, "Nenda tu, mwanao yu mzima." Huyo mtu akaamini maneno ya Yesu, akaenda zake. 51: Alipokuwa bado njiani, watumishi wake walikutana naye, wakamwambia kwamba mwanawe alikuwa mzima. 52: Naye akawauliza saa mtoto alipopata nafuu; nao wakamwambia, "Jana saa saba mchana, homa ilimwacha." 53: Huyo baba akakumbuka kwamba ilikuwa ni saa ileile ambapo Yesu alimwambia: "Mwanao yu mzima." Basi, yeye akaamini pamoja na jamaa yake yote. 54: Hii ilikuwa ishara ya pili aliyoifanya Yesu alipokuwa anatoka Yudea kwenda Galilaya.