[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21]

Chapter 2

1: Siku ya tatu kulikuwa na arusi mjini Kana, mkoani Galilaya. Mama yake Yesu alikuwapo, 2: naye Yesu alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. 3: Divai ilipokwisha, mama yake akamwambia, "Hawana divai!" 4: Yesu akamjibu, "Mama, usiniambie la kufanya. Saa yangu bado." 5: Hapo mama yake akawaambia watumishi, "Lolote atakalowaambieni, fanyeni." 6: Hapo palikuwa na mitungi sita ya mawe, ambayo kila mmoja uliweza kuchukua kiasi cha madebe mawili au matatu. Ilikuwa imewekwa hapo kufuatana na desturi ya Kiyahudi ya kutawadha. 7: Yesu akawaambia, "Ijazeni mitungi hiyo maji." Nao wakaijaza mpaka juu. 8: Kisha akawaambia, "Sasa choteni mkampelekee mkuu wa karamu." 9: Mkuu wa karamu alipoonja hayo maji, kumbe yalikuwa yamegeuka kuwa divai. Yeye hakujua ilikotoka, (lakini wale watumishi waliochota maji walijua). Mkuu wa karamu akamwita bwana arusi, 10: akamwambia, "Kila mtu huandaa divai nzuri kwanza hata wakisha tosheka huandaa ile hafifu. Lakini wewe umeiweka divai nzuri mpaka sasa!" 11: Yesu alifanya ishara hii ya kwanza huko Kana, Galilaya, akaonyesha utukufu wake; nao wanafunzi wake wakamwamini. 12: Baada ya hayo, Yesu alishuka pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, wakaenda Kafarnaumu ambako walikaa kwa siku chache. 13: Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa imekaribia; hivyo Yesu akaenda Yerusalemu. 14: Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ng`ombe, kondoo na njiwa, na wavunja fedha walikuwa wamekaa kwenye meza zao. 15: Akatengeneza mjeledi wa kamba, akawafukuza wote nje ya Hekalu pamoja na kondoo na ng`ombe wao, akazimwaga sarafu za wenye kuvunja fedha na kupindua meza zao. 16: Akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, "Ondoeni vitu hivi hapa. Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa soko!" 17: Wanafunzi wake wakakumbuka kwamba Maandiko yasema: "Upendo wangu kwa nyumba yako waniua." 18: Baadhi ya Wayahudi wakamwuliza Yesu, "Utafanya muujiza gani kuonyesha kwamba unayo haki kufanya mambo haya?" 19: Yesu akawaambia, "Vunjeni Hekalu hili, nami nitalijenga kwa siku tatu." 20: Hapo Wayahudi wakasema, "Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita. Je, wewe utalijenga kwa siku tatu?" 21: Lakini Yesu alikuwa anaongea juu ya Hekalu ambalo ni mwili wake. 22: Basi, alipofufuliwa kutoka wafu, wanafunzi wake walikumbuka kwamba alikuwa amesema hayo, wakaamini Maandiko Matakatifu na yale maneno aliyokuwa akisema Yesu. 23: Yesu alipokuwa Yerusalemu kwa sikukuu ya Pasaka, watu wengi walimwamini walipoona ishara alizozifanya. 24: Lakini Yesu hakuwa na imani nao kwa sababu aliwajua wote. 25: Hakuhitaji kuambiwa chochote juu ya watu, maana aliyajua barabara mambo yote yaliyomo mioyoni mwao.