[1]
[2]
[3]
[4]
[5]
Chapter 21:
Ndugu zangu, mkiwa mnamwamini Bwana Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwabague watu kamwe.
2:
Tuseme mtu mmoja ambaye amevaa pete ya dhahabu na mavazi nadhifu anaingia katika mkutano wenu, na papo hapo akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi machafu.
3:
Ikiwa mtamstahi zaidi yule aliyevaa mavazi ya kuvutia na kumwambia: "Keti hapa mahali pazuri," na kumwambia yule maskini: "Wewe, simama huko," au "Keti hapa sakafuni miguuni pangu,"
4:
je, huo si ubaguzi kati yenu? Je, na huo uamuzi wenu haujatokana na fikira mbaya?
5:
Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni! Mungu amechagua watu ambao ni maskini katika ulimwengu huu ili wapate kuwa matajiri katika imani na kupokea Utawala aliowaahidia wale wanaompenda.
6:
Lakini ninyi mnawadharau watu maskini! Je, matajiri si ndio wanaowakandamizeni na kuwapeleka mahakamani?
7:
Je, si haohao wanaolitukana hilo jina lenu zuri mlilopewa?
8:
Kama mnaitimiza ile sheria ya Utawala kama ilivyoandikwa katika Maandiko Matakatifu: "Mpende binadamu mwenzako kama unavyojipenda wewe mwenyewe", mtakuwa mnafanya vema kabisa.
9:
Lakini mkiwabagua watu, basi, mwatenda dhambi, nayo Sheria inawahukumu ninyi kuwa mna hatia.
10:
Anayevunja amri mojawapo ya Sheria, atakuwa na hatia ya kuivunja Sheria yote.
11:
Maana yuleyule aliyesema: "Usizini," alisema pia "Usiue". Kwa hiyo, hata ikiwa hukuzini lakini umeua, wewe umeivunja Sheria.
12:
Basi, semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria iletayo uhuru.
13:
Maana, Mungu hatakuwa na huruma atakapomhukumu mtu asiyekuwa na huruma. Lakini huruma hushinda hukumu.
14:
Ndugu zangu, kuna faida gani mtu kusema ana imani, lakini haonyeshi kwa vitendo? Je, hiyo imani yawezaje kumwokoa?
15:
Tuseme kaka au dada hana nguo au chakula.
16:
Yafaa kitu gani ninyi kuwaambia hao: "Nendeni salama mkaote moto na kushiba," bila kuwapatia mahitaji yao ya maisha?
17:
Vivyo hivyo, imani peke yake bila matendo imekufa.
18:
Lakini mtu anaweza kusema: "Wewe unayo imani, mimi ninayo matendo!" Haya! Nionyeshe jinsi mtu anavyoweza kuwa na imani bila matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo yangu.
19:
Je, wewe unaamini kwamba yuko Mungu mmoja? Sawa! Lakini hata pepo huamini hilo, na hutetemeka kwa hofu.
20:
Mpumbavu wee! Je, wataka kuonyeshwa kwamba imani bila matendo imekufa?
21:
Je, Abrahamu baba yetu alipataje kukubalika mbele yake Mungu? Kwa matendo yake, wakati alipomtoa mwanae Isaka sadaka juu ya madhabahu.
22:
Waona basi, kwamba imani yake iliandamana na matendo yake; imani yake ilikamilishwa kwa matendo yake.
23:
Hivyo yakatimia yale Maandiko Matakatifu yasemayo: "Abrahamu alimwamini Mungu na kwa imani yake akakubaliwa kuwa mtu mwadilifu; na hivyo Abrahamu akaitwa rafiki wa Mungu."
24:
Mnaona basi, kwamba mtu hukubaliwa kuwa mwadilifu kwa matendo yake na si kwa imani peke yake.
25:
Ilikuwa vivyo hivyo kuhusu yule malaya Rahabu; yeye alikubaliwa kuwa mwadilifu kwa sababu aliwapokea wale wapelelezi na kuwasaidia waende zao kwa kupitia njia nyingine.
26:
Basi, kama vile mwili bila roho umekufa, vivyo hivyo imani bila matendo imekufa.
|