[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13]

Chapter 10

1: Sheria ya Wayahudi si picha kamili ya mambo yale halisi: ni kivuli tu cha mema yanayokuja. Dhabihu zilezile hutolewa daima, mwaka baada ya mwaka. Sheria yawezaje, basi, kwa njia ya dhabihu hizo, kuwafanya wale wanaoabudu wawe wakamilifu? 2: Kama hao watu wanaomwabudu Mungu wangekuwa wametakaswa dhambi zao kweli, hawangejisikia tena kuwa na dhambi, na dhabihu hizo zote zingekoma. 3: Lakini dhabihu hizo hufanyika kila mwaka kuwakumbusha watu dhambi zao. 4: Maana damu ya fahali na mbuzi haiwezi kamwe kuondoa dhambi. 5: Ndiyo maana Kristo alipokuwa anakuja ulimwenguni, alimwambia Mungu: "Hukutaka dhabihu wala sadaka, lakini umenitayarishia mwili. 6: Sadaka za kuteketezwa au za kuondoa dhambi hazikupendezi. 7: Hapo nikasema: `Niko hapa ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako kama ilivyoandikwa juu yangu katika kitabu cha Sheria."` 8: Kwanza alisema: "Hutaki, wala hupendezwi na dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za kuondoa dhambi." Alisema hivyo ingawa sadaka hizi zote hutolewa kufuatana na Sheria. 9: Kisha akasema: "Niko hapa, ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako." Hivyo Mungu alibatilisha dhabihu za zamani na mahali pake akaweka dhabihu nyingine moja. 10: Kwa kuwa Yesu Kristo alitimiza mapenzi ya Mungu, sisi tunatakaswa dhambi zetu kwa ile dhabihu ya mwili wake aliyotoa mara moja tu, ikatosha. 11: Kila kuhani Myahudi humhudumia Mungu kila siku, akitoa dhabibu zilezile mara nyingi, dhabibu ambazo haziwezi kuondoa dhambi. 12: Lakini Kristo alitoa dhabihu moja tu kwa ajili ya dhambi, dhabihu ifaayo milele, kisha akaketi upande wa kulia wa Mungu. 13: Huko anangoja mpaka adui zake watakapowekwa kama kibao chini ya miguu yake. 14: Basi, kwa dhabihu yake moja tu, amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wanaotakaswa dhambi zao. 15: Naye Roho Mtakatifu anatupa ushahidi wake. Kwanza anasema: 16: "Hili ndilo agano nitakalofanya nao, katika siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika akilini mwao." 17: Kisha akaongeza kusema: "Sitakumbuka tena dhambi zao, wala vitendo vyao vya uhalifu." 18: Basi, dhambi zikisha ondolewa, hakutakuwa na haja tena ya kutoa dhabihu za kuondoa dhambi. 19: Basi, ndugu, kwa damu ya Yesu tunapewa moyo thabiti wa kuingia Mahali Patakatifu. 20: Yeye ametufungulia njia mpya na yenye uzima kupitia lile pazia, yaani kwa njia ya mwili wake mwenyewe. 21: Basi, tunaye kuhani maarufu aliye na mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. 22: Kwa hiyo tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu na imani timilifu, kwa mioyo iliyotakaswa dhamiri mbaya, na kwa miili iliyosafishwa kwa maji safi. 23: Tushikilie imara tumaini lile tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu. 24: Tujitahidi kushughulikiana kwa ajili ya kuongezeana bidii ya kupendana na kutenda mema. 25: Tusiache ile desturi ya kukutana pamoja, kama vile wengine wanavyofanya. Bali tunapaswa kusaidiana kwani, kama mwonavyo, Siku ile ya Bwana inakaribia. 26: Maana, tukiendelea kutenda dhambi makusudi baada ya kufahamu ukweli, hakuna dhabihu iwezayo kutolewa tena kwa ajili ya kuondoa dhambi. 27: Linalobaki ni kungojea tu kwa hofu hukumu ya Mungu na moto mkali utakaowaangamiza wote wanaompinga. 28: Mtu yeyote asiyeitii Sheria ya Mose, huuawa bila ya huruma kukiwa na ushahidi wa watu wawili au watatu. 29: Je, mtu yule anayempuuza Mwana wa Mungu na kuidharau damu ya agano la Mungu iliyomtakasa, mtu anayemtukana Roho wa Mungu, anastahili kupata adhabu kali ya namna gani? 30: Maana tunamfahamu yule aliyesema, "Mimi nitalipiza kisasi, mimi nitalipiza," na ambaye alisema pia, "Bwana atawahukumu watu wake." 31: Kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai ni jambo la kutisha mno! 32: Kumbukeni yaliyotokea siku zile za kwanza mlipoangaziwa mwanga wa Mungu. Ingawa siku zile mlipatwa na mateso mengi, ninyi mlistahimili. 33: Mara nyingine mlitukanwa na kufedheheshwa hadharani; mara nyingine mlikuwa radhi kuungana na wale walioteswa namna hiyohiyo. 34: Mlishiriki mateso ya wafungwa, na mliponyang`anywa mali yenu mlistahimili kwa furaha, maana mlijua kwamba mnayo mali bora zaidi na ya kudumu milele. 35: Basi, msipoteze uhodari wenu, maana utawapatieni tuzo kubwa. 36: Mnahitaji kuwa na uvumilivu, ili mweze kufanya anayotaka Mungu na kupokea kile alichoahidi. 37: Maana kama yasemavyo Maandiko: "Bado kidogo tu, na yule anayekuja, atakuja, wala hatakawia. 38: Lakini mtu wangu aliye mwadilifu ataamini na kuishi; walakini akirudi nyuma, mimi sitapendezwa naye." 39: Basi, sisi hatumo miongoni mwa wale wanaorudi nyuma na kupotea, ila sisi tunaamini na tunaokolewa.