[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13]

Chapter 5

1: Kila kuhani mkuu huchaguliwa kutoka miongoni mwa watu kwa ajili ya kumtumikia Mungu kwa niaba yao, kutolea zawadi na tambiko kwa ajili ya dhambi zao. 2: Maadamu yeye mwenyewe yu dhaifu anaweza kuwaonea huruma wale wasiojua kitu na wanaofanya makosa. 3: Na kwa vile yeye mwenyewe ni dhaifu, anapaswa kutolea dhabihu si tu kwa ajili ya watu, bali pia kwa ajili ya dhambi zake. 4: Hakuna mtu awezaye kujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu. Kila mmoja huteuliwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kama alivyokuwa Aroni. 5: Hali kadhalika naye Kristo hakujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu, bali Mungu alimwambia: "Wewe ni Mwanangu; mimi leo nimekuwa baba yako." 6: Alisema pia mahali pengine: "Wewe ni kuhani milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki." 7: Yesu alipokuwa anaishi hapa duniani, kwa kilio kikuu na machozi, alisali na kumwomba Mungu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwokoa kutoka kifo; naye alisikilizwa kwa sababu ya kumcha Mungu. 8: Lakini, ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, alijifunza kutii kwa njia ya mateso. 9: Na alipofanywa mkamilifu, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wale wote wanaomtii, 10: naye Mungu akamteua kuwa kuhani mkuu kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki. 11: Tunayo Mengi ya kusema juu ya jambo hili, lakini ni vigumu kuwaelezeni, kwa sababu ninyi si wepesi wa kuelewa. 12: Sasa mngalipaswa kuwa tayari walimu, lakini mnahitaji bado mtu wa kuwafundisheni mafundisho ya mwanzo ya ujumbe wa Mungu. Badala ya kula chakula kigumu, mnapaswa bado kunywa maziwa. 13: Kila anayepaswa kunywa maziwa huyo ni mtoto bado, hajui uadilifu ni nini. 14: Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu waliokomaa, ambao wanaweza kubainisha mema na mabaya.