[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13]

Chapter 3

1: Ndugu zangu watu wa Mungu ambao mmeitwa na Mungu, fikirini juu ya Yesu ambaye Mungu alimtuma awe Kuhani Mkuu wa imani tunayoiungama. 2: Yeye alikuwa mwaminifu kwa Mungu aliyemteua kufanya kazi yake kama vile Mose alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu. 3: Mjenzi wa nyumba hupata heshima zaidi kuliko hiyo nyumba yenyewe. Hali kadhalika naye Yesu anastahili heshima kubwa zaidi kuliko Mose. 4: Kila nyumba hujengwa na mjenzi fulani--na Mungu ndiye mjenzi wa vitu vyote. 5: Mose alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Bwana kama mtumishi, na alinena juu ya mambo ambayo Mungu atayasema hapo baadaye. 6: Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana mwenye mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. Sisi ni nyumba yake kama tukizingatia uhodari wetu na uthabiti wetu katika kile tunachotumainia. 7: Kwa hiyo, basi, kama asemavyo Roho Mtakatifu: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, 8: msiifanye mioyo yenu kuwa migumu kama wazee wenu walivyokuwa wakati walipomwasi Mungu; kama walivyokuwa siku ile kule jangwani, 9: Huko wazee wenu walinijaribu na kunichunguza, asema Bwana, ingawa walikuwa wameyaona matendo yangu kwa miaka arobaini. 10: Kwa sababu hiyo niliwakasirikia watu hao nikasema, `Fikira za watu hawa zimepotoka, hawajapata kamwe kuzijua njia zangu.` 11: Basi, nilikasirika, nikaapa: `Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko."` 12: Basi ndugu, jihadharini asije akawako yeyote miongoni mwenu aliye na moyo mbaya hivyo na asiyeamini hata kujitenga na Mungu aliye hai. 13: Maadamu hiyo "Leo" inayosemwa katika Maandiko bado inatuhusu sisi, mnapaswa kusaidiana daima, ili mtu yeyote miongoni mwenu asidanganywe na dhambi na kuwa mkaidi. 14: Maana sisi tunashirikiana na Kristo ikiwa tutazingatia kwa uthabiti tumaini tulilokuwa nalo mwanzoni. 15: Maandiko yasema hivi: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, msiifanye mioyo yenu kuwa migumu kama wazee wenu walivyokuwa wakati walipomwasi Mungu." 16: Ni akina nani basi, waliosikia sauti ya Mungu wakamwasi? Ni wale wote walioongozwa na Mose kutoka Misri. 17: Mungu aliwakasirikia akina nani kwa miaka arobaini? Aliwakasirikia wale waliotenda dhambi, maiti zao zikatapakaa kule jangwani. 18: Mungu alipoapa: "Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko," alikuwa anawasema akina nani? Alikuwa anasema juu ya hao walioasi. 19: Basi, twaona kwamba hawakuingia huko kwa sababu hawakuamini.