[1] [2] [3] [4] [5] [6]

Chapter 4

1: Basi, nasema hivi: mrithi, akiwa bado mtoto, hawi tofauti na mtumwa ingawaje mali yote ni yake. 2: Wakati huo wote yuko chini ya walezi na wadhamini mpaka wakati ule uliowekwa na baba yake. 3: Hali kadhalika na sisi tulipokuwa bado watoto, tulikuwa watumwa wa pepo watawala wa ulimwengu. 4: Lakini wakati ule maalumu ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanawe aliyezaliwa na mwanamke, akaishi chini ya Sheria 5: apate kuwakomboa wale waliokuwa chini ya Sheria ili sisi tufanywe wana wa Mungu. 6: Kwa vile sasa ninyi ni wana, Mungu amemtuma Roho wa Mwanae mioyoni mwenu, Roho ambaye hulia "Aba," yaani "Baba." 7: Basi, wewe si mtumwa tena, bali mwana. Na ikiwa ni mwana, basi, wewe utapokea yote Mungu aliyowawekea watoto wake. 8: Zamani hamkumjua Mungu na hivyo mkatumikia miungu isiyo miungu kweli. 9: Lakini sasa, kwa vile mnamjua Mungu, au tuseme mnajulikana na Mungu, mnawezaje tena kurudi kwa wale pepo maskini na dhaifu hata kutaka kuwatumikia tena? 10: Bado mnaadhimisha siku, miezi na miaka! 11: Nahofu kwamba labda kazi niliyoifanya kwa ajili yenu imepotea bure! 12: Ndugu, nawasihi muwe kama mimi, kwa vile hata mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunitendea ubaya wowote. 13: Mnajua kwamba ugonjwa wangu ndio ulionipatia fursa ya kuwahubirieni Habari Njema kwa mara ya kwanza. 14: Hata hivyo, wakati ule hamkunidharau wala kunikataa kwa sababu ya udhaifu wangu ingawa mlishawishiwa kufanya hivyo; lakini mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama vile ningekuwa Kristo Yesu mwenyewe. 15: Mlikuwa wenye furaha; sasa kumetokea nini? Naapa kwamba wakati ule mngaliweza hata kuyang`oa macho yenu na kunipa mimi. 16: Je, sasa nimekuwa adui yenu kwa sababu ya kuwaambieni ukweli? 17: Hao watu wengine wanawahangaikia ninyi, lakini nia zao si njema. Wanataka kuwatenganisha nami ili ninyi muwahangaikie wao. 18: Kwa kweli ni jambo jema daima kuwahangaikia wengine katika mambo mema, na si tu wakati mimi nipo pamoja nanyi. 19: Watoto wangu, kama vile mama mja mzito anavyotaabika wakati wa kujifungua, mimi nataabika tena kwa ajili yenu mpaka hapo hali yake Kristo itakapoundwa ndani yenu. 20: Laiti ningekuwa pamoja nanyi sasa, maana ningalipata msimamo ufaao juu yenu! Nina wasiwasi sana nanyi! 21: Niambieni, enyi mnaopenda kutawaliwa na sheria: Je, mnasikia isemavyo Sheria? 22: Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Abrahamu alikuwa na watoto wawili: mmoja kwa mwanamke mtumwa, na wa pili kwa mwanamke huru. 23: Yule wa mwanamke mtumwa alizaliwa kama kawaida, lakini yule wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu. 24: Mambo hayo yamekuwa mfano; mama hao wawili ni mfano wa maagano mawili; la kwanza ni lile lililofanyika mlimani Sinai, mwakilishi wake ni Hagari, na watoto wake wanazaliwa utumwani. 25: Hagari anawakilisha mlima Sinai ulioko Arabia, na ni mfano wa Yerusalemu ya sasa, ulio mtumwa pamoja na watoto wake. 26: Lakini Yerusalemu ya juu mbinguni ni mji ulio huru, nao ni mama yetu. 27: Maana imeandikwa: "Furahi, ewe uliye tasa usiyezaa; paaza sauti wewe usiyepata kujifungua mtoto; maana watoto wa yule aliyeachwa ni wengi zaidi kuliko wa yule aliye na mume." 28: Sasa, basi, ndugu zangu, ninyi ni watoto wa Mungu kutokana na ahadi yake kama alivyokuwa Isaka. 29: Lakini kama vile siku zile yule mtoto aliyezaliwa kwa njia ya kawaida alimdhulumu yule aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho wa Mungu, vivyo hivyo na siku hizi. 30: Lakini Maandiko Matakatifu yasemaje? Yasema: "Mfukuze mama mtumwa pamoja na mwanawe; maana mtoto wa mtumwa hatarithi pamoja na mtoto wa mama huru." 31: Kwa hiyo, basi, ndugu, sisi si watoto wa mtumwa bali wa mama huru.