[1] [2] [3] [4] [5] [6]

Chapter 3

1: Enyi Wagalatia, mmekuwa wajinga kweli! Ni nani aliyewaloga? Habari juu ya kusulubiwa kwake Yesu Kristo ilielezwa waziwazi mbele ya macho yenu. 2: Napenda kujua tu kitu kimoja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa sababu ya kutimiza matakwa ya Sheria ama kwa sababu ya kuisikia na kuiamini Habari Njema? 3: Je, mu wajinga kiasi hicho? Ninyi mlianza yote kwa msaada wa Roho je, mnataka sasa kumaliza kwa nguvu zenu wenyewe? 4: Je, mambo yale yote yaliyowapata ninyi yamekuwa bure tu? Haiwezekani! 5: Je, Mungu huwajalia Roho na kutenda miujiza kati yenu ati kwa sababu mnatimiza yanayotakiwa na sheria, ama kwa sababu mnasikia Habari Njema na kuiamini? 6: Chukueni kwa mfano habari za Abrahamu: yeye alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu. 7: Sasa basi jueni kwamba watu wenye kumwamini ndio walio watoto halisi wa Abrahamu. 8: Maandiko Matakatifu yalionyesha kabla kwamba Mungu atawakubali watu wa mataifa kuwa waadilifu kwa njia ya imani. Hivyo Maandiko Matakatifu yalitangulia kumtangazia Abrahamu Habari Njema: "Katika wewe mataifa yote yatabarikiwa." 9: Basi, wale walio na imani wanabarikiwa pamoja na Abrahamu aliyeamini. 10: Lakini wote wanaotegemea tu kutimiza yanayotakiwa na Sheria, wako chini ya laana. Maana, Maandiko Matakatifu yasema: "Yeyote asiyeshika na kutimiza yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Sheria, yuko chini ya laana." 11: Ni dhahiri kwamba Sheria haiwezi kumfanya mtu akubaliwe kuwa mwadilifu; maana Maandiko Matakatifu yasema: "Mwadilifu kwa imani ataishi." 12: Lakini Sheria haitegemei imani, ila Maandiko yasema: "Mwenye kutimiza yanayotakiwa na Sheria ataishi." 13: Kristo alitukomboa kutoka katika laana ya Sheria kwa kujitwalia laana hiyo kwa ajili yetu; maana Maandiko yanasema: "Yeyote aliyetundikwa msalabani amelaaniwa." 14: Jambo hili lilifanyika kusudi ile baraka aliyopewa Abrahamu iwashukie watu wa mataifa mengine kwa njia ya Kristo, na ili kwa imani, tumpokee yule Roho ambaye Mungu alituahidia. 15: Ndugu, nitawapeni mfano kutoka maisha yetu ya kila siku. Fikirini juu ya mkataba kati ya watu wawili. Mkataba ukisha fanyika na kutiwa sahihi hapana mtu anayeuweka kando au kuuongezea kitu. 16: Basi, Abrahamu alipewa ahadi, yeye pamoja na mzawa wake. Maandiko hayasemi: "Na wazawa wake," yaani wengi, bali yasema, "Na mzawa wake," yaani mmoja, naye ndiye Kristo. 17: Ninachotaka kusema ni hiki: Mungu alifanya agano lake akalithibitisha; Sheria ambayo ilitokea miaka mia nne na thelathini baadaye, haiwezi kulitangua hilo agano wala kuibatilisha hiyo ahadi. 18: Maana, kama urithi ya Mungu inategemea Sheria, basi, haiwezi kutegemea tena ahadi ya Mungu. Kumbe, lakini Mungu alimkirimia Abrahamu kwa sababu aliahidi. 19: Ya nini basi, Sheria? Iliongezwa hapo ili kuonyesha uhalifu ni kitu gani, mpaka atakapokuja yule mzawa wa Abrahamu aliyepewa ile ahadi. Sheria ililetwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi. 20: Ama hakika, mpatanishi hahitajiwi ikiwa jambo lenyewe lamhusu mtu mmoja; na Mungu ni mmoja. 21: Je, Sheria inapingana na ahadi za Mungu? Hata kidogo! Maana, kama kungalitolewa sheria ambayo ingeweza kuwapa watu uzima, basi, tungeweza kukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Sheria. 22: Lakini sivyo; Maandiko Matakatifu yamekwisha sema kwamba ulimwengu wote upo chini ya utawala wa dhambi; na hivyo, kwa kumwamini Yesu Kristo, wenye kuamini watimiziwe ile ahadi. 23: Kabla ya kujaliwa imani, Sheria ilitufanya wafungwa mpaka imani hiyo iliyokuwa inakuja ifunuliwe. 24: Basi, hiyo Sheria ilikuwa kama mlezi wetu mpaka alipokuja Kristo, ili kwa njia ya imani, tukubaliwe kuwa waadilifu. 25: Tangu kufika kwa hiyo imani, Sheria si mlezi wetu tena. 26: Kwa njia ya imani, ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika kuungana na Kristo. 27: Ninyi nyote mliobatizwa mkaungana na Kristo ni kama vile mmemvaa Kristo. 28: Hivyo, hakuna tena tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, mtumwa na mtu huru, mwanamume na mwanamke. Nyote ni kitu kimoja katika kuungana na Kristo Yesu. 29: Ikiwa ninyi ni wa Kristo, basi ni wazawa wa Abrahamu, na mtapokea yale aliyoahidi Mungu.