[1] [2] [3] [4] [5] [6]

Chapter 6

1: Enyi watoto, watiini wazazi wenu Kikristo maana hili ni jambo jema. 2: "Waheshimu Baba na mama yako," hii ndiyo amri ya kwanza ambayo imeongezewa ahadi, yaani, 3: "Upate fanaka na miaka mingi duniani." 4: Nanyi akina baba, msiwachukize watoto wenu ila waleeni katika nidhamu na mafundisho ya Kikristo. 5: Enyi watumwa, watiini mabwana zenu hapa duniani kwa hofu na tetemeko; fanyeni hivyo kwa unyofu wa moyo kana kwamba mnamtumikia Kristo. 6: Fanyeni hivyo si tu wakati wanapowatazama ili mjipendekeze kwao, bali tumikieni kwa moyo kama atakavyo Mungu kwa sababu ninyi ni watumishi wa Kristo. 7: Muwe radhi kutumikia kwa ajili ya Bwana na si kwa ajili ya watu. 8: Kumbukeni kwamba kila mtu mwenye kutenda mema, awe mtumwa au mtu huru, atapokea tuzo lake kutoka kwa Bwana. 9: Nanyi mnaotumikiwa, watendeeni vivyo hivyo watumwa wenu, na acheni kutumia vitisho. Kumbukeni kwamba ninyi pia kama vile wao, mnaye Bwana yuleyule mbinguni, kwake cheo cha mtu si kitu. 10: Hatimaye, nawatakeni muwe imara katika kuungana na Bwana na kwa msaada wa nguvu yake kuu. 11: Vaeni silaha anazowapeni Mungu mpate kuzipinga mbinu mbaya za Ibilisi. 12: Maana vita vyenu si vita kati yetu na binadamu, bali ni vita dhidi ya jeshi ovu la ulimwengu wa roho; tunapigana na watawala, wakuu na wenye nguvu wanaomiliki ulimwengu huu wa giza. 13: Kwa sababu hiyo, vaeni silaha za Mungu ili siku ile itakapofika muweze kuyapinga mashambulio ya adui; na mkisha pigana mpaka mwisho, muwe bado thabiti. 14: Basi, simameni imara! Ukweli uwe kama ukanda kiunoni mwenu, uadilifu uwe kama vazi la kujikinga kifuani, 15: na hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani iwe kama viatu miguuni mwenu. 16: Zaidi ya hayo yote, imani iwe daima kama ngao mikononi mwenu, iwawezeshe kuizima mishale ya moto ya yule Mwovu. 17: Upokeeni wokovu kama kofia yenu ya chuma, na neno la Mungu kama upanga mnaopewa na Roho Mtakatifu. 18: Salini daima, mkiomba msaada wa Mungu. Salini kila wakati kwa nguvu ya Roho. Kesheni bila kuchoka mkisali kwa ajili ya watu wote wa Mungu. 19: Niombeeni nami pia ili niongeapo Mungu anijalie cha kusema, niweze kuwajulisha watu fumbo la Habari Njema kwa uthabiti. 20: Mimi ni balozi kwa ajili ya Habari Njema hiyo ingawa sasa niko kifungoni. Ombeni, basi, ili niweze kuwa hodari katika kuitangaza kama inipasavyo. 21: Tukiko, ndugu yetu mpenzi na mtumishi mwaminifu wa Bwana, atawapeni habari zangu zote mpate kujua ninachofanya. 22: Namtuma kwenu awapeni habari zetu mpate kuwa na moyo. 23: Ninawatakieni ninyi ndugu amani, upendo na imani kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo. 24: Nawatakia neema ya Mungu wote wanaompenda Bwana wetu Yesu Kristo kwa mapendo yasiyo na mwisho.