[1] [2] [3] [4] [5] [6]

Chapter 5

1: Kwa hiyo, mwigeni Mungu, maana ninyi ni watoto wake wapenzi. 2: Upendo uongoze maisha yenu, kama vile Kristo alivyotupenda, na kwa ajili yetu akajitoa mwenyewe kama dhabihu yenye harufu nzuri na tambiko impendezayo Mungu. 3: Kwa vile ninyi ni watu wa Mungu, basi uasherati, uchafu wowote ule au choyo visitajwe kamwe miongoni mwenu. 4: Tena maneno ya aibu, ya upuuzi au ubishi, yote hayo hayafai kwenu; maneno ya kumshukuru Mungu ndiyo yanayofaa. 5: Jueni wazi kwamba mwasherati yeyote au mchafu au mfisadi, (ufisadi ni sawa na kuabudu sanamu), au mtu yeyote wa aina hiyo hataambulia chochote katika Utawala wa Kristo na wa Mungu. 6: Msikubali kudanganywa na mtu kwa maneno matupu; maana, kwa sababu ya mambo kama hayo ghadhabu ya Mungu huwajia wote wasiomtii. 7: Basi, msishirikiane nao. 8: Zamani ninyi mlikuwa gizani, lakini sasa ninyi mko katika mwanga kwa kuungana na Bwana. Ishini kama watoto wa mwanga: 9: maana matokeo ya mwanga ni wema kamili, uadilifu na ukweli. 10: Jaribuni kujua yale yanayompendeza Bwana. 11: Msishiriki katika matendo yasiyofaa, ya giza bali yafichueni. 12: Mambo yanayotendwa kwa siri ni aibu hata kuyataja. 13: Lakini mambo yale yanayotendwa katika mwanga, ukweli wake hudhihirishwa; 14: na kila kilichodhihirishwa huwa mwanga. Ndiyo maana Maandiko yasema: "Amka wewe uliyelala, fufuka kutoka wafu, naye Kristo atakuangaza." 15: Basi, muwe waangalifu jinsi mnavyoishi: Msiishi kama wapumbavu, bali kama wenye hekima. 16: Tumieni vizuri muda mlio nao maana siku hizi ni mbaya. 17: Kwa hiyo, msiwe wapumbavu, bali jaribuni kujua matakwa ya Bwana. 18: Acheni kulewa divai maana hiyo itawaangamiza, bali mjazwe Roho Mtakatifu. 19: Zungumzeni kwa maneno ya Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Bwana nyimbo na zaburi kwa shukrani mioyoni mwenu. 20: Mshukuruni Mungu Baba daima kwa ajili ya yote, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo. 21: Kila mmoja amstahi mwenzake kwa sababu ya kumcha Kristo. 22: Wake wawatii waume zao kama kumtii Bwana. 23: Maana mume anayo mamlaka juu ya mkewe, kama vile Kristo alivyo na mamlaka juu ya kanisa; naye Kristo mwenyewe hulikomboa kanisa, mwili wake. 24: Kama vile kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo, wake wawatii waume zao katika mambo yote. 25: Nanyi waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda kanisa, akajitoa mwenyewe sadaka kwa ajili yake. 26: Alifanya hivyo, ili kwa neno lake, aliweke wakfu kwa Mungu, baada ya kulifanya safi kwa kuliosha katika maji, 27: kusudi ajipatie kanisa lililo takatifu na safu kabisa, kanisa lisilo na doa, kasoro au chochote cha namna hiyo. 28: Basi, waume wanapaswa kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. (( 29: Hakuna mtu yeyote auchukiaye mwili wake; badala ya kuuchukia, huulisha na kuuvika. Ndivyo naye Kristo anavyolitunza kanisa, 30: maana sisi ni viungo vya mwili wake.) 31: Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Kwa hiyo, mwanamume atawaacha baba na mama yake, ataungana na mkewe, nao wawili watakuwa mwili mmoja." 32: Kuna ukweli uliofichika katika maneno haya, nami naona kwamba yamhusu Kristo na kanisa lake. 33: Lakini yanawahusu ninyi pia: kila mume lazima ampende mkewe kama nafsi yake mwenyewe, naye mke anapaswa kumstahi mumewe.