[1] [2] [3] [4] [5] [6]

Chapter 3

1: Kutokana na hayo, mimi Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu kwa ajili yenu, namwomba Mungu. 2: Bila shaka mmekwisha sikia kwamba Mungu, kwa neema yake, alinikabidhi kazi hii niifanye kwa faida yenu. 3: Mimi nilijulishwa kwa njia ya ufunuo mpango wake uliofichika. (Nimeandika kwa ufupi juu ya jambo hili, 4: nanyi mkiyasoma maneno yangu mtaweza kujua jinsi ninavyoielewa siri hiyo ya Kristo.) 5: Zamani watu hawakujulishwa siri hiyo; lakini sasa Mungu amewajulisha mitume na manabii wake watakatifu kwa njia ya Roho. 6: Siri yenyewe ni hii: kwa njia ya Habari Njema watu wa mataifa mengine wanapata sehemu yao pamoja na Wayahudi katika zile baraka za Mungu; wao ni viungo vya mwili uleule, na wanashiriki ahadi ileile aliyofanya Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. 7: Mimi nimefanywa kuwa mtumishi wa Habari Njema kwa neema ya pekee aliyonijalia Mungu kwa uwezo wake mkuu. 8: Mimi ni mdogo kuliko watu wote wa Mungu; lakini amenijalia neema yake, ili niwahubirie watu wa mataifa utajiri wake Kristo usiopimika, 9: tena niwaangazie watu wote waone jinsi mpango wa Mungu uliofichika unavyotekelezwa. Mungu aliye Muumba wa vitu vyote alificha siri hiyo yake tangu milele, 10: kusudi, sasa kwa njia ya kanisa, wakuu na wenye enzi wa mbinguni wapate kuitambua hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi. 11: Mungu alifanya jambo hilo kufuatana na azimio lake la milele ambalo amelifanya kwa njia ya Kristo Bwana wetu. 12: Basi, katika kuungana na Kristo, na kwa njia ya imani katika Kristo, sisi tunathubutu kumkaribia Mungu kwa uhodari. 13: Kwa hiyo, nawaombeni msife moyo kwa sababu ya mateso ninayopata kwa ajili yenu, maana hayo ni kwa ajili ya utukufu wenu. 14: Kwa sababu hiyo, nampigia magoti Baba, 15: aliye asili ya jamaa zote duniani na mbinguni. 16: Namwomba Mungu, kadiri ya utajiri wa utukufu wake, awajalieni kwa uwezo wa Roho wake, nguvu ya kuwa imara ndani yenu, 17: naye Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani. Namwomba mpate kuwa na mzizi na msingi katika mapendo 18: kusudi muweze kufahamu pamoja na watu wote wa Mungu jinsi upendo wa Kristo ueneavyo kwa mapana na marefu, kwa kimo na kina. 19: Naam, mpate kujua upendo wa Kristo upitao elimu yote, mjazwe kabisa utimilifu wote wa Mungu. 20: Kwake yeye ambaye kwa nguvu yake ifanyayo kazi ndani yetu, aweza kufanya mambo makuu zaidi ya yale tuwezayo kuomba au kufikiria; 21: kwake Mungu uwe utukufu katika kanisa na katika Kristo Yesu, nyakati zote, milele na milele! Amina.