[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24] [25] [26] [27] [28]

Chapter 11

1: Mitume na ndugu kule Yudea walisikia kwamba watu wa mataifa mengine pia walikuwa wamelipokea neno la Mungu. 2: Basi, Petro aliporudi Yerusalemu, wale Wayahudi waumini waliopendelea watu wa mataifa mengine watahiriwe, walimlaumu wakisema: 3: "Wewe umekwenda kukaa na watu wasiotahiriwa na hata umekula pamoja nao! 4: Hapo Petro akawaeleza kinaganaga juu ya yale yaliyotendeka tangu mwanzo: 5: "Siku moja nikiwa nasali mjini Yopa, niliona maono; niliona kitu kama shuka kubwa likishushwa chini kutoka mbinguni likiwa limeshikwa pembe zake nne, likawekwa kando yangu. 6: Nilichungulia ndani kwa makini nikaona wanyama wenye miguu minne, wanyama wa mwituni, wanyama watambaao na ndege wa angani. 7: Kisha nikasikia sauti ikiniambia: `Petro amka, chinja, ule.` 8: Lakini mimi nikasema: `La, Bwana; maana chochote kilicho najisi au kichafu hakijapata kamwe kuingia kinywani mwangu.` 9: Ile sauti ikasikika tena kutoka mbinguni: `Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa.` 10: Jambo hilo lilifanyika mara tatu, na mwishowe vyote vilirudishwa juu mbinguni. 11: Ghafla, watu watatu waliokuwa wametumwa kwangu kutoka Kaisarea waliwasili kwenye nyumba niliyokuwa nakaa. 12: Roho aliniambia niende pamoja nao bila kusita. Hawa ndugu sita waliandamana nami pia kwenda Kaisarea na huko tuliingia nyumbani mwa Kornelio. 13: Yeye alitueleza jinsi alivyokuwa amemwona malaika amesimama nyumbani mwake na kumwambia: `Mtume mtu Yopa akamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro. 14: Yeye atakuambia maneno ambayo kwayo wewe na jamaa yako yote mtaokolewa.` 15: Na nilipoanza tu kuongea, Roho Mtakatifu aliwashukia kama alivyotushukia sisi pale awali. 16: Hapo nilikumbuka yale maneno Bwana aliyosema: `Yohane alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.` 17: Basi, kama Mungu amewapa pia watu wa mataifa mengine zawadi ileile aliyotupa sisi tulipomwamini Bwana Yesu Kristo, je, mimi ni nani hata nijaribu kumpinga Mungu?" 18: Waliposikia hayo, waliacha ubishi, wakamtukuza Mungu wakisema, "Mungu amewapa watu wa mataifa mengine nafasi ya kutubu na kuwa na uzima!" 19: Kutokana na mateso yaliyotokea wakati Stefano alipouawa, waumini walitawanyika. Wengine walikwenda mpaka Foinike, Kupro na Antiokia wakihubiri ule ujumbe kwa Wayahudi tu. 20: Lakini baadhi ya waumini waliotoka Kupro na Kurene, walikwenda Antiokia wakautangaza huo ujumbe kwa watu wa mataifa mengine wakiwahubiria ile Habari Njema juu ya Bwana Yesu. 21: Bwana aliwasaidia na idadi kubwa ya watu iliamini na kumgeukia Bwana. 22: Habari ya jambo hilo ikasikika kwa lile kanisa la Yerusalemu. Hivyo wakamtuma Barnaba aende Antiokia. 23: Alipofika huko na kuona jinsi Mungu alivyowaneemesha wale watu, alifurahi na kuwahimiza wote wadumu katika uaminifu wao kwa Bwana. 24: Barnaba alikuwa mtu mwema na mwenye kujaa Roho Mtakatifu na imani. Kundi kubwa la watu lilivutwa kwa Bwana. 25: Kisha, Barnaba alikwenda Tarso kumtafuta Saulo 26: Alipompata, alimleta Antiokia. Nao wote wawili walikaa na lile kanisa kwa mwaka wote mzima wakifundisha kundi kubwa la watu. Huko Antiokia, ndiko, kwa mara ya kwanza, wafuasi waliitwa Wakristo. ic 27: Wakati huohuo, manabii kadhaa walikuja Antiokia kutoka Yerusalemu. 28: Basi, mmoja wao aitwaye Agabo alisimama, na kwa uwezo wa Roho akabashiri kwamba kutakuwa na njaa kubwa katika nchi yote (Njaa hiyo ilitokea wakati Klaudio alipokuwa akitawala). 29: Wale wanafunzi waliamua kila mmoja kwa kadiri ya uwezo wake apeleke chochote ili kuwasaidia wale ndugu waliokuwa wanaishi Yudea. 30: Basi, wakafanya hivyo na kupeleka mchango wao kwa wazee wa kanisa kwa mikono ya Barnaba na Saulo.