[1] [2] [3] [4]

Chapter 3

1: Kumbuka kwamba, katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za taabu. 2: watu watakuwa na ubinafsi, wenye tamaa ya fedha, wenye majivuno, wenye kujiona, wenye kumtukana Mungu, wasiowatii wazazi wao, wasio na shukrani na waovu; 3: watatokea watu wasio na upendo moyoni, wasio na huruma, wachongezi, walafi na wakali; watachukia chochote kilicho chema; 4: watakuwa wahaini, wakaidi na waliojaa kiburi; watapenda anasa kuliko kumpenda Mungu. 5: Kwa nje wataonekana kama watu wenye kumcha Mungu, lakini wataikana nguvu yake. Jiepushe kabisa na watu wa namna hiyo. 6: Baadhi yao huenda katika nyumba za watu na huwateka wanawake dhaifu waliolemewa mizigo ya dhambi na ambao wanaongozwa na tamaa za kila aina; 7: wanawake ambao wanajaribu daima kujifunza lakini hawawezi kuufikia ujuzi wa huo ukweli. 8: Watu hao huupinga ukweli kama vile Yane na Yambre walivyompinga Mose. 9: Lakini hawataweza kuendelea zaidi kwa maana upumbavu wao utaonekana wazi kwa wote. Ndivyo ilivyokuwa kwa akina Yane na Yambre. 10: Wewe lakini, umeyafuata mafundisho yangu, mwenendo wangu, makusudi yangu katika maisha, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo wangu, subira yangu, 11: udhalimu na mateso yangu. Unayajua mambo yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Lustra. Nilivumilia udhalimu mkubwa mno! Lakini Bwana aliniokoa katika mambo hayo yote. 12: Kila mtu anayetaka kuishi maisha ya kumcha Mungu katika kuungana na Kristo Yesu lazima adhulumiwe. 13: Watu waovu na wadanyanyifu watazidi kuwa waovu zaidi na zaidi kwa kuwadanganya wengine na kudanganyika wao wenyewe. 14: Lakini wewe dumu katika ukweli ule uliofundishwa, ukaukubali kabisa. Unawajua wale waliokuwa walimu wako. 15: Unakumbuka kwamba tangu utoto wako umeyajua Maandiko Matakatifu ambayo yaweza kukupatia hekima iletayo wokovu kwa njia ya imani kwa Kristo Yesu. 16: Maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufundishia ukweli, kuonya, kusahihisha makosa, na kuwaongoza watu waishi maisha adili, 17: ili mtu anayemtumikia Mungu awe mkamilifu, na tayari kabisa kufanya kila tendo jema.