[1] [2] [3]

Chapter 3

1: Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili ujumbe wa Bwana uzidi kuenea upesi na kupokelewa kwa heshima kama vile ulivyo kati yenu. 2: Ombeni pia ili Mungu atuokoe na watu wapotovu na waovu, maana si wote wanaoamini ujumbe huu. 3: Lakini Bwana ni mwaminifu. Yeye atawaimarisheni na kuwalinda salama na yule Mwovu. 4: Naye Bwana anatupatia tumaini kubwa juu yenu, na hatuna shaka kwamba mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaambieni. 5: Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika uvumilivu tunaopewa na Kristo. 6: Ndugu, tunawaamuru kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, mjiepushe na ndugu wote walio wavivu na ambao hawafuati maagizo tuliyowapa. 7: Ninyi wenyewe mnajua kwamba mnapaswa kufuata mfano wetu. Sisi tulipokuwa nanyi hatukuwa wavivu; 8: hatukula chakula kwa mtu yeyote bila ya kumlipa. Tulifanya kazi kwa bidii na taabu mchana na usiku ili tusiwe mzigo kwa mtu yeyote kati yenu. 9: Tulifanya hivyo si kwa kuwa hatuna haki ya kutaka msaada wenu, ila kwa sababu tunataka kuwapeni mfano. 10: Tulipokuwa pamoja nanyi tulikuwa tukiwaambieni, "Mtu asiyefanya kazi, asile." 11: Tunasema mambo hayo kwa sababu tumesikia kwamba wako baadhi yenu ambao ni wavivu na ambao hawafanyi chochote, isipokuwa tu kujiingiza katika mambo ya watu wengine. 12: Kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo tunawaamuru na kuwaonya watu hao wawe na nidhamu na kufanya kazi ili wajipatie maslahi yao wenyewe. 13: Lakini ninyi ndugu, msichoke kutenda mema. 14: Huenda kwamba huko kuna mtu ambaye hatautii huu ujumbe tunaowapelekeeni katika barua hii. Ikiwa hivyo, basi, mfichueni mtu huyo na msiwe na uhusiano wowote naye kusudi aone aibu. 15: Lakini msimtendee mtu huyo kama adui, bali mwonyeni kama ndugu. 16: Bwana mwenyewe ndiye chanzo cha amani, awajalieni amani siku zote kwa kila namna. Bwana awe nanyi nyote. 17: Kwa mkono wangu mwenyewe naandika hivi: Salamu kutoka kwa Paulo! Hivi ndivyo ninavyotia sahihi kila barua; ndivyo ninavyoandika. 18: Tunawatakieni nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.