[1] [2] [3]

Chapter 2

1: Sasa yahusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanywa kwetu pamoja tukae naye. Ndugu, tunawaombeni sana 2: msifadhaike upesi moyoni, na wala msitiwe wasiwasi kwa sababu ya madai kwamba Siku ya Bwana imekwisha fika. Labda inadhaniwa kwamba jambo hili limetokana na uaguzi fulani, mahubiri au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu. 3: Msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa namna yoyote ile. Maana Siku hiyo haitakuja mpaka kwanza ule Uasi Mkuu utokee na yule Mwovu aonekane ambaye mwisho wake ni kuangamizwa kabisa. 4: Yeye atapinga kila kitu wanachokiona watu kuwa ni mungu, au wanachokiabudu. Naam, hata ataingia na kuketi ndani ya Hekalu la Mungu akijidai kuwa Mungu. 5: Je, hamkumbuki kwamba niliwaambieni haya yote wakati nilipokuwa pamoja nanyi? 6: Lakini kuna kitu kinachomzuia sasa, nanyi mwakijua kitu hicho. Basi, huyo Mwovu ataonekana wakati wake ufaao. 7: Hata hivyo, Mwovu huyo aliyefichika anafanya kazi sasa, lakini hataonekana mpaka yule anayemzuia aondolewe. 8: Hapo ndipo Mwovu atakapotokea; lakini Bwana Yesu anapokuja atamuua kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kwa mng`ao wa kuja kwake. 9: Huyo Mwovu atakuja na nguvu za Shetani na kufanya kila namna ya miujiza na maajabu ya uongo, 10: na kutumia udanganyifu wa kila namna kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea. Hao watapotea kwa sababu hawakuupokea na kuupenda ule ukweli ili waokolewe. 11: Ndiyo maana Mungu amewaweka chini ya nguvu ya upotovu, wauamini uongo. 12: Matokeo yake ni kwamba wote wasioamini ukweli, ila wafurahia dhambi, watahukumiwa. 13: Tunapaswa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu ninyi ndugu, ninyi mnaopendwa na Bwana, kwa maana Mungu amewateua tangu mwanzo mpate kuokolewa kwa nguvu ya Roho mfanywe watu wake watakatifu kwa imani yenu katika ukweli. 14: Mungu aliwaitieni jambo hili kwa njia ya Habari Njema tuliyowahubirieni; aliwaiteni mpate kupokea sehemu yenu katika utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. 15: Basi, ndugu, simameni imara na zingatieni yale mafundisho tuliyowafundisheni kwa mahubiri yetu na barua zetu. 16: Tunamwomba Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu ambaye alitupenda, na kwa neema yake akatujalia faraja ya milele na tumaini jema, 17: aifariji mioyo yenu na kuwaimarisheni ili mweze daima kutenda na kusema yaliyo mema.