[1]
[2]
[3]
Chapter 11:
Mimi Paulo, Silwano na Timotheo tunawaandikia ninyi jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambao ni watu wake Mungu Baba yetu na wa Bwana Yesu Kristo.
2:
Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
3:
Ndugu, tunapaswa kushukuru Mungu daima kwa ajili yenu. Inafaa kwetu kufanya hivyo kwani imani yenu inakua sana na kupendana kwenu kunaongezeka sana.
4:
Ndio maana sisi tunajivunia ninyi katika makanisa ya Mungu. Tunaona fahari juu ya jinsi mnavyoendelea kuamini na kustahimili katika udhalimu wote na mateso mnayopata.
5:
Hayo yote yanathibitisha kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na matokeo yake ninyi mtastahili Utawala wake ambao kwa ajili yake mnateseka.
6:
Mungu atafanya jambo la haki: atawalipa mateso wale wanaowatesa ninyi,
7:
na kuwapeni nafuu ninyi mnaoteseka, na sisi pia. Atafanya jambo hilo wakati Bwana atakapotokea kutoka mbinguni pamoja na malaika wake na wakuu
8:
na miali ya moto, kuwaadhibu wale wanaomkataa Mungu na wale wasiotii Habari Njema ya Bwana wetu Yesu.
9:
Adhabu yao itakuwa kuangamizwa milele na kutengwa mbali na utukufu wake mkuu,
10:
wakati atakapokuja Siku ile kupokea utukufu kutoka kwa watu wake na heshima kutoka kwa wote wanaoamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwao, kwani mmeuamini ule ujumbe tuliowaletea.
11:
Ndiyo maana tunawaombeeni daima. Tunamwomba Mungu wetu awawezeshe muyastahili maisha aliyowaitia myaishi. Tunamwomba, kwa uwezo wake, atimize nia yenu ya kutenda mema na kukamilisha kazi yenu ya imani.
12:
Kwa namna hiyo, jina la Bwana wetu Yesu litapata utukufu kutoka kwenu, nanyi mtapata utukufu kutoka kwake kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.
|