[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13]

Chapter 11

1: Laiti mngenivumilia kidogo, hata kama mimi ni mjinga kiasi fulani! Naam, nivumilieni kidogo. 2: Ninawaoneeni wivu lakini ni wivu wa Mungu; maana ninyi ni kama bikira safi niliyemposa kwa mwanamume mmoja tu ambaye ndiye Kristo. 3: Lakini naogopa kwamba, kama vile yule nyoka kwa hila zake za uongo alimdanganya Hawa, fikira zenu zaweza kupotoshwa, mkauacha uaminifu wenu wa kweli kwa Kristo. 4: Maana mtu yeyote ajaye na kumhubiri Yesu aliye tofauti na yule tuliyemhubiri, ninyi mwampokea kwa mikono miwili; au mnakubali roho au habari njema tofauti kabisa na ile mliyopokea kutoka kwetu! 5: Sidhani kwamba mimi ni mdogo kuliko hao "mitume wakuu." 6: Labda sina ufasaha wa lugha, lakini elimu ninayo; jambo hili tumelionyesha wazi kwenu, kila mahali na kila wakati. 7: Mimi niliihubiri kwenu Habari Njema ya Mungu bila kudai mshahara; nilijinyenyekeza ili nipate kuwakweza ninyi. Je, nilifanya vibaya? 8: Nilipofanya kazi kati yenu, mahitaji yangu yaligharimiwa na makanisa mengine. Kwa namna moja au nyingine niliwapokonya wao mali yao nipate kuwatumikia ninyi. 9: Nilipokuwa nanyi sikumsumbua mtu yeyote nilipohitaji fedha; ndugu waliotoka Makedonia waliniletea kila kitu nilichohitaji. Nilikuwa mwangalifu sana nisiwe mzigo kwa namna yoyote ile, na nitaendelea kufanya hivyo. 10: Naahidi kwa ule ukweli wa Kristo ulio ndani yangu, kwamba hakuna kitakachoweza kunizuia kujivunia jambo hilo popote katika Akaya. 11: Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu eti siwapendi ninyi? Mungu anajua kwamba nawapenda! 12: Nitaendelea kufanya kama ninavyofanya sasa, ili nisiwape nafasi wale wanaotafuta nafasi, nafasi ya kujivuna kwamba eti wanafanya kazi kama sisi. 13: Maana, hao ni mitume wa uongo, wafanyakazi wadanganyifu wanojisingizia kuwa mitume wa Kristo. 14: Wala si ajabu, maana hata Shetani mwenyewe hujisingizia kuwa malaika wa mwanga! 15: Kwa hiyo si jambo la kushangaza ikiwa na hao watumishi wake wanajisingizia kuwa watumishi wa haki. Mwisho wao watapata kile wanachostahili kufuatana na matendo yao. 16: Tena nasema: Mtu asinifikirie kuwa mpumbavu. Lakini kama mkifikiri hivyo, basi, nichukueni kama mpumbavu ili nami nipate kuwa na cha kujivunia angaa kidogo. 17: Ninachosema sasa si kile alichoniagiza Bwana; kuhusu jambo hili la kujivuna, nasema tu kama mtu mpumbavu. 18: Maadam wengi hujivuna kwa sababu za kidunia, nami pia nitajivuna. 19: Ninyi ni wenye busara, ndiyo maana hata mnawavumilia wapumbavu! 20: Mnamvumilia hata mtu anayewafanya ninyi watumwa, mtu mwenye kuwanyonya, mwenye kuwakandamiza, mwenye kuwadharau na kuwapiga usoni! 21: Kwa aibu nakubali kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Iwe iwavyo, lakini kama kuna mtu yeyote anayethubutu kujivunia kitu--nasema kama mtu mpumbavu--mimi nathubutu pia. 22: Je, wao ni Waebrania? Hata mimi. Je, wao ni Waisraeli? Hata mimi. Wao ni wazawa wa Abrahamu? Hata mimi. 23: Wao ni watumishi wa Kristo? Hata mimi--nanena hayo kiwazimu--ni mtumishi wa Kristo zaidi kuliko wao. Mimi nimefanya kazi ngumu zaidi, nimekaa gerezani mara nyingi zaidi, nimepigwa mara nyingi zaidi na nimekaribia kifo mara nyingi. 24: Mara tano nilichapwa vile viboko thelathini na tisa vya Wayahudi. 25: Nilipigwa viboko mara tatu, nilipigwa mawe mara moja; mara tatu nilivunjikiwa meli baharini, na humo nikakesha usiku kucha na kushinda mchana kutwa. 26: Kila mara safarini nimekabiliwa na hatari za mafuriko ya mito, na hatari za wanyama; hatari kutoka kwa wananchi wenzangu na kutoka kwa watu wa mataifa mengine; hatari za mjini, hatari za porini, hatari za baharini, hatari kutoka kwa ndugu wa uongo 27: Nimefanya kazi na kutaabika, nimekesha bila usingizi mara nyingi; nimekuwa na njaa na kiu; mara nyingi nimefunga na kukaa katika baridi bila nguo. 28: Na, licha ya mengine mengi, kila siku nakabiliwa na shughuli za makanisa yote. 29: Kama mtu yeyote ni dhaifu, nami pia ni dhaifu; mtu yeyote akikwazwa, nami pia huwa na wasiwasi. ic 30: Ikinilazimu kujivuna, basi, nitajivunia udhaifu wangu. 31: Mungu na Baba wa Bwana Yesu--jina lake litukuzwe milele--yeye anajua kwamba sisemi uongo. 32: Nilipokuwa Damasko, mkuu wa mkoa, aliyekuwa chini ya mfalme Areta, alikuwa akiulinda mji wa Damasko ili apate kunikamata. 33: Lakini, ndani ya kapu kubwa, niliteremshwa nje kupitia katika nafasi ukutani, nikachopoka mikononi mwake.